012-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Kuweka Mikono Juu Ya Kifua, Kutazama Mahali Pa Kusujudu, Na Khushuu (Unyenyekevu) Katika Swalah
KUWEKA MIKONO JUU YA KIFUA
"Alikuwa akiweka mkono wa kulia nyuma ya kitanga cha mkono wa kushoto, kiwiko na kigasha"[1] "na aliwaamrisha Maswahaba wake kufanya hivyo"[2] na (mara nyingine) "akiushika mkono wa kushoto kwa mkono wake wa kulia"[3]
"Alikuwa akiiweka juu ya kifua chake"[4]
Pia, alikuwa akikataza mtu kuweka mkono juu ya kiuno wakati wa Swalah na aliweka mkono wake juu ya kiuno (kuonyesha makosa hayo)[5] Na hii ndio swilb aliyokuwa akikataza.[6]
KUTAZAMA MAHALI PA KUSUJUDU
"Alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akiinamisha kichwa chake wakati wa Swalah na kukongomeza (kuyaelekeza) macho yake katika ardhi[7]
"Alipoingia katika Kaabah, hakuacha jicho lake kutazama sehemu ya kusujudu hadi alipotoka nje"[8] na alisema: ((Haipasi kuweko na kitu chochote katika Nyumba kitakachomshawishi mwenye kuswali))"[9]
"Alikuwa akikataza kuinua macho kutazama mbinguni"[10] na alishikilia makatazo haya sana hadi alisema: ((Watu lazima waache kutazama juu mbinguni katika Swalah au macho yao hayatorudi kwao)) [na katika riwaaya nyingine] ((…au macho yao yatapofushwa))[11]
Katika Hadiyth nyingine: ((Mnaposwali msiangaze huku na kule kwani Allaah Huelekeza Uso Wake mbele ya uso wa mja Wake madamu mja hatoangaza kwengine)).[12] Akasema pia kuhusu kuangaza huku na kule: ((Ni kunyakuliwa ambako Shaytwaan hunyakuwa katika Swalah ya mja anaposwali))[13]
Akasema pia (صلى الله عليه وآله وسلم): ((Allaah Haachi kuelekea kwa mja katika Swalah madamu tu mja haangazi huku na kule, anapogeuza uso wake mbali, Allaah Hugeuka mbali naye))[14] na "Akakataza mambo matatu; kudonoa kama jogoo, kuchutama kama mbawa na kuangaza kama fisi",[15] vile vile alikuwa akisema: ((Swalini Swalah ya kuaga (dunia) kama kwamba mnamuona Yeye (Allaah) na kama hamumuoni, hakika Yeye Anakuoneni))[16], na (akisema), ((Mtu yeyote anayefikwa na Swalah ya fardhi akatawadha vizuri, akakamilisha khushuu (unyenyekevu) zake, na rukuu zake, hakika itakuwa ni kafara ya dhambi alizotenda kabla ya Swalah hiyo madamu hajatenda dhambi kubwa, hali hiyo ni kwa mwaka wote))[17]
Mara moja yeye (صلى الله عليه وآله وسلم) aliswali katika khamiysah[18] (na alipokuwa akiswali) alizitazama alama zake. Alipomaliza akasema: ((Ipelekeeni khamiysah hii yangu kwa Abu Jahm na nileteeni (badala yake) anbijaaniyyah[19] kwani imenipotezea umakini wangu katika Swalah)) [katika usimulizi mmoja] ((…kwani nimetazama alama zake wakati wa Swalah ilikaribia kunitia katika mtihani))[20]
Pia Mama wa Waumini 'Aaishah (رضي الله عنها) alikuwa na kitambaa cha picha kilichotandazwa mbele ya sahwah[21] ambayo Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) aliswali mbele yake, akasema: ((Iondoshelee mbali, [kwani picha zake hazikuacha kunishawishi katika Swalah]))[22]
Alikuwa akisema pia: ((Hakuna kuswali chakula kinapokuwa tayari, wala mtu anapotaka kukidhi haja kubwa na ndogo))[23]
[1] Abu Daawuud, An-Nasaaiy na Ibn Khuzaymah (1/54/2) ikiwa na isnaad Swahiyh na Ibn Hibbaan amekiri usahihi wake (485).
[2] Maalik, Al-Bukhaariy na Abu 'Awaanah.
[3] An-Nasaaiy na Ad-Daraqutwniy ikiwa na isnaad Swahiyh. Katika Hadiyth hii kuna ushahidi kwamba kuishikilia ni Sunnah na katika Hadiyth nyingine, kuwekea tu, hivyo yote ni Sunnah. Ama kuunga baina ya kuweka na kushikilia ambayo baadhi ya Mahanafi waliotangulia wameona ni vizuri, hivyo ni bid'ah; mfumo wake ni kama walivyotaja kuwa ni kuweka mkono wa kulia juu ya mkono wa kushoto, kushikilia kiwiko kwa kidole kidogo na cha gumba, na kuviweka bapa vidole vitatu vengine, kama ilivyoelezewa katika tanbihi za Ibn 'Aabidiyn kwenye Durr Al-Mukhtaar (1/454) kwa hiyo usibabaike na wasemayo.
[4] Abu Daawuud, Ibn Khuzaymah katika Swahiyh yake (1/54/2) Ahmad na Abu Shaykh katika Taariykh Iswbahaan (Uk.125), At-Tirmidhiy amekiri moja ya isnaad ni hasan (njema) na maana yake inapatikana katika Al-Muwattwaa na Swahiyh Al-Bukhaariy ikichukuliwa kwa makini. Nimenukuu isnaad kamili ya Hadiyth hii katika kitabu changu Ahkaam al-Janaaiz (Uk. 118).
TANBIHI:
Kuiweka katika kifua ndivyo ilivyothibiti katika Sunnah, na kinyume chake ni aidha dhaifu au haina msingi. Na Imaam Is-haaq Ibn Raahawayh alifanya Sunnah hii kama alivyosema Al-Marwazy katika Masaail (Uk. 222). "Is-haaq alikuwa akiswali Witr pamoja na sisi … alikuwa akinyanyua mikono yake katika Qunuut na akileta Qunuut kabla ya kurukuu na kuweka mikono yake kifuani mwake au chini yake". Ni sawa na usemi wa Qaadhwiy 'Iyaadh Al-Maalikiy katika Mustahabbaat As-Swalah kitabu chake Al-I'laam (Uk. 15, chapa ya 3, Ar-Rabaatw) "Mkono wa kulia uwekwe juu ya mkono wa kushoto sehemu ya juu ya kifua". Na karibu na hii ni kama alivyohusisha 'Abdullaah bin Ahmad bin Hanbal katika Masaail yake (Uk. 62): "Niliona wakati wa kuswali, baba yangu akiweka mikono yake mmoja juu ya mwenziwe juu ya kitovu (chini ya kifua kidogo)" Tazama Kiambatisho 4.
[5] Al-Bukhaariy na Muslim.
[6] Abu Daawuud, An-Nasaaiy na wengineo.
[7] Al-Bayhaaqiy na al-Haakim ambaye amekiri kuwa ni Swahiyh kama alivyosema. Pia ina Hadiyth iliyotilia nguvu iliyoripotiwa na Maswahaba kumi: iliyosimuliwa na Ibn 'Asaakir' (17/202/2) Taz. Al-Irwaa (354).
TANBIHI:
Hadiyth hizi mbili zinaonyesha kwamba Sunnah ni kukaza macho yake mtu mahali pa kusujudu ardhini, hivyo kufunga macho katika Swalah kama wafanyavo baadhi ya watu ni ukosefu ya uchaji Mungu, kwani uongofu bora kabisa ni uongofu wa Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم).
[8] Al-Bayhaaqiy na al-Haakim.
[9] Abu Daawuud na Ahmad ikiwa ni isnaad ya Swahiyh (Al-Irwaa 1771); iliyokusudiwa hapa 'Nyumba' ni Kaabah kama inavyoonyesha yaliyomo katika Hadiyth.
[10] Al-Bukhaary Abu Daawuud.
[11] Al-Bukhariy, Muslim na Siraaj.
[12] At-Tirmidhiy na al-Haakim ambaye amekiri ni Swahiyh – (Swahiyh At-Targhiyb Namba: 353).
[13] Al-Bukhaariy na Abu Daawuud.
[14] Imesimuliwa na Abu Daawuud na wengineo. Ibn Khuzayma na Ibn Hibbaan wamekiri usahihi wake. Taz. Swahiyh At-Targhiyb (Namba 555).
[15] Ahmad na Abu Ya'laa. Taz Swahiyh At-Targhiyb (Na,ba 556)
[16] Al-Mukhlisw katika Ahaadityh Muntaqaa, At-Twabaraaniy, Ar-Ruuyaaniy, Adh-Dwiyaa katika Al-Mukhtaarah, Ibn Maajah, Ahamd na Ibn 'Asaakir. Al-Hayatamy amekiri ni Swahiyh kaitka Asnan Al-Matwaalib
[17] Muslim.
[18] Nguo ya sufi iliyo na alama.
[19] Nguo ya kukwaruza isiyo na alama.
[20] Al-Bukhaariy, Muslim na Maalik imetolewa katika Al-Irwaa (376)
[21] Chumba kidogo kilichobanwa kidogo katika ardhi kama chemba au kabati. (Nihaayah)
[22] Al-Bukhaariy, Muslim na Abu 'Awaanah. Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) hakuamrisha kufutwa au kuchana picha bali aliziondosha kwa sababu. Na Allaah Anajua zaidi- hazikuwa ni picha zenye roho. Ushahidi wa hili ni kwamba yeye (صلى الله عليه وآله وسلم) alichana picha nyinginezo kama ilivyothibiti katika usimulizi mwingi katika Al-Bukhaariy na Muslim na yeyote apendaye kutafiti zaidi atazame Fat-h Al-Baariy (10/321) na Ghaayah Al-maraam fiy Takhriyj Ahaadiyth Al-Halaal wal-Haraam (Namba: 131-145).
[23]Al-Bukhaariy na Muslim.