Kusoma Halal Badiri au Albadiri (Ahlul-Badr) Kwa Ajili Ya Kinga Na Kuapiza Ni Shirki Na Dhambi Kuu!

 

Kusoma Halal Badiri  au Albadiri (Ahlul-Badr) Kwa

Ajili Ya Kinga Na Kuapiza  Ni Shirki Na Dhambi Kuu!

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalama Alaykum Warahmatullah T'aalaa  Wabarakatu.

 

Napenda kuanza kwa kumshukuru Rabb mlezi wa ulimwengu kwa kuwapa nguvu, afya na uwezo ndugu zetu wa alhidaaya kwa kutuelimisha sisi ndugu zenu Waislam katika musuala mengi yanayohusu dini yetu ya haki.  Rabb awape kheir, baraka na pepo In Shaa Allaah. Ameen.

 

Na suali langu ni kutaka kujua kama kusoma halal badr ni sawa au si sawa katika uislam? Kuwa kama kinga na kuomba Allaah akuhukumie kwa anetaka kukudhuru au kukufania ubaya.

Asanteni....assalam aleykum.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Awali twataka kurekebisha ibara hiyo kwani sivyo inavyokusudiwa au inavyotamkwa au kuandikwa. Ibara hiyo imetoka katika lugha ya Kiarabu lakini kupotolewa au kuandikwa na kusomwa makosa katika Kiswahili. Wapo wanaosema Alibadiri lakini makusudio ni Ahlul-Badr, yenye maana watu wa Badr (wale waliopigana vita vya Badr). Badr ni sehemu iliyo karibu na Madiynah na ndio iliyokuwa sehemu ambayo Waislamu wakiongozwa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) walipambana na mushirikina wa Makkah katika vita vya kwanza baina ya pande hizo mbili. Waislamu waliohudhuria walikuwa baina ya 313 – 317, lakini pamoja na idadi yao ndogo hiyo waliweza kuwashinda washirikina waliokuwa na idadi kubwa ipatayo mara sita yao.

 

 

Kisomo cha Ahlul Badri inakuwa ni kutaja majina ya Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) mmoja baada ya mwingine. Katika kutaja huko ni Imani ya mwenye kusoma hao Maswahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) wanamsaidia kwa njia moja au nyingine. Ima kupata kitu alichopoteza au kilichoibiwa au kulaaniwa aliyefanya. Na hii katika Uislamu ni njia moja ya shirki ambayo Allaah Aliyetukuka na Nabiy Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wameikema na kuipiga vita sana. Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدِ افْتَرَىٰ إِثْمًا عَظِيمًا ﴿٤٨﴾

Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amezua dhambi kuu. [An-Nisaa: 48]. 

 

 

Ingia Katika Kiungo Kifuatacho pia upate maelezo yam as-ala haya:

 

 

Wazazi Wangu Wako Kwenye Maasi,Ushirikina Wa Waganga Na Albadiri (Ahlul-Badr)

 

 

Ikiwa unataka kinga basi kinga ni nyingi sana tulizopatiwa na Uislamu ni nyingi. Qur-aan yenyewe ni ponyo na kinga ya mambo mengi na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) naye hakutuacha hivi hivi ila ametupatia kinga nyingi katika Surah na Aayah za Qur-aan na du’aa alizotuachia. Miongoni mwa kinga ni Muislamu kusoma Surah 112, 113 na 114 mara tatu tatu asubuhi, jioni na wakati wa kulala. Hiswnul Muslim ni kijitabu kizuri cha du’aa na adhkaar katika mas-ala haya.

 

 

Utakipata kitabu hicho ndani ya Alhidaaya kwenye kiungo hiki:

 

Hiswnul Muslim

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share