Masuala Kumi Yanayoeleweka Vibaya Katika Uislam - 10
Masuala Kumi Yanayoeleweka Vibaya Katika Uislaam - 10
Imefasiriwa na: Naaswir Haamid
Suala Nambari 10 Linaloeleweka Vibaya
Uislaam unazalisha jamii iliyo vivu, isiyoelimika kwa sababu:
- Vitu vyote vinatokana na Allaah na hivyo nis awa kuamini hakuna hiari ya mwanadamu – ‘Fatalism’
- Teknolojia na sayansi ya sasa haikubaliwi
Hoja zilizotolewa kwa suala hili linaloeleweka vibaya ni za uongo, na hilo suala wenyewe hakika limekanushwa moja kwa moja na Qur-aan na Sunnah. Wakati ni kweli kwamba Allaah ni chanzo cha kila kitu juu yetu, lakini sio kweli kwamba hili linaweza kutumika kuwa ni udhuru wa binaadamu kujificha kama aya zifuatazo kutoka Qur-aan zinavyoeleza:
وَقَالَ الَّذِينَ أَشْرَكُوا لَوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا عَبَدْنَا مِن دُونِهِ مِن شَيْءٍ نَّحْنُ وَلَا آبَاؤُنَا وَلَا حَرَّمْنَا مِن دُونِهِ مِن شَيْءٍ ۚ كَذَٰلِكَ فَعَلَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ ۚ فَهَلْ عَلَى الرُّسُلِ إِلَّا الْبَلَاغُ الْمُبِينُ﴿٣٥﴾
Na wale washirikina wakasema: Kama Angelitaka Allaah tusingeliabudu chochote pasi Naye, sisi wala baba zetu; wala tusingeliharamisha chochote bila (ya amri) Yake. Hivyo ndivyo walivyofanya wale wa kabla yao. Basi je, kuna lolote juu ya Rusuli isipokuwa ubalighisho bayana? [An-Nahl: 35]
وَقَالُوا لَوْ شَاءَ الرَّحْمَـٰنُ مَا عَبَدْنَاهُم ۗ مَّا لَهُم بِذَٰلِكَ مِنْ عِلْمٍ ۖ إِنْ هُمْ إِلَّا يَخْرُصُونَ﴿٢٠﴾
Na wakasema: Angelitaka Ar-Rahmaan tusingeliyaabudu (miungu ya uongo). Hawana elimu yoyote ya hayo, hawana isipokuwa wanabuni uongo. [Az-Zukhruf: 20]
Allaah Ametufundisha kupitia kwa Qur-aan na Sunnah kwamba sote tuna kiwango fulani cha uhuru. Uhuru huu ni lazima ufanyiwe kazi sawa sawa kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah ili kumridhisha Allaah. Hii ni hamasa iliyo kubwa kwa Waislamu wote kuwasukuma kuwa ni wenye ujuzi ulio bora, wanaweza kuwa Waislamu walio imara kabisa. Kama jamii ya Waisalmu leo hawawezi kusuluhisha matatizo yao, basi sio kwasababu ya uelewa wao wa Uislaam, isipokuwa ni kwasababu ya ujinga wao wa njia hii ya maisha. Umuhimu wa kutafuta elimu na kufanya kazi yanaelezwa wazi ndani ya Sunnah.
Kutokana na Sunnah, hususan ndani ya somo la Sunnah linaloitwa Sunnah ya [Abuu-Daawuud], tunaona:
Amesimulia Anas bin Maalik: “Mtu wa Answaar alikuja kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuomba, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuuliza: Jee una chochote ndani ya nyumba yako? Akajibu: Ndio, kipande cha nguo, sehemu ambayo tunavaa na sehemu ambayo tunatandika (katika sakafu), na bakuli la mbao ambalo tunakunywia maji. Alisema: Vilete kwangu. Baadaye alivileta vitu hivi kwake na yeye (Nabiy) alivichukua kwenye mkono wake na kuuliza: Ni nani atakayevinunua hivi? Mtu mmoja akasema: Mimi nitavinunua kwa dirham moja, Alisema mara mbili au mara tatu: Nani atajitolea zaidi ya dirham moja? Mtu mmoja akasema: Mimi nitanunua kwa dirham mbili. Alimpatia vitu hivi na kuchukua dirham mbili, na kumpatia Answaari, alisema: Nunua chakula kwa moja yake na wafikishie ukoo wako, na nunua shoka na lilete kwangu. Baadaye alilileta kwake. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliliunganisha mpini pamoja nalo kwa mikono yake na kusema: Nenda, tafuta kuni na uziuze, na nisikuone kwa wiki mbili. Mtu yule alikwenda zake na kutafuta kuni na kuuza. Alipopata dirham kumi, alikuja kwake na kumnunulia guo na baadhi yake kwa chakula. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Hili ni bora kwako (kuliko) lile, kuomba kutakuja kama ni alama kwenye uso wako Siku ya Hukumu. Kuomba ni ruhusa kwa watu watatu tu: Yule ambaye anakufa kwa njaa, yule ambaye ana deni lililokuwa baya mno, au yule ambaye anahusika na kulipa fidia na anapata tabu kulipa”.
Pia kutokana na Sunnah, hususan ndani ya somo la Sunnah linaloitwa Suna ya [Ibn Majah], tunaona kwamba Rasuli wa Allaah amesema:
“Kutafuta elimu ni wajibu kwa kila Muislamu”.
Ujuzi wa Qur-aan na Sunnah ndio aina za elimu zilizo bora kabisa, na elimu inayonufaisha binaadamu pia ni nzuri. Qur-aan na Sunnah hazizuii usomaji wa dunia hii na ukweli Allaah Anatuhimiza kuuchunguza ulimwengu tunaoishi kwa mujibu wa aya ifuatayo kutoka kwenye Qur-aan:
إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لَآيَاتٍ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ ﴿١٩٠﴾ الَّذِينَ يَذْكُرُونَ اللَّـهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِهِمْ وَيَتَفَكَّرُونَ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَـٰذَا بَاطِلًا سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّارِ ﴿١٩١﴾
Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi, na mabadiliko ya mfuatano wa usiku na mchana; bila shaka ni Aayaat (ishara, zingatio) kwa wenye akili. Ambao wanamdhukuru Allaah kwa kusimama na kwa kukaa na kwa kulala ubavuni mwao na wanatafakari katika kuumbwa mbingu na ardhi (wakisema): Rabb wetu, Hukuumba haya bure, Utakasifu ni Wako tukinge na adhabu ya moto. [Aal-‘Imraan: 190-191]
Chochote kilicho kizuri ndani ya makala hii kinatokana na Allaah, na kilicho kibaya ndani yake kinatokana na sisi.