017-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Aamiyn - Imaam Kunyanyua Sauti Yake Anapoileta
AAMIYN, IMAAM KUNYANYUA SAUTI YAKE ANAPOILETA
Kisha alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) anapomaliza kusoma Al-Faatihah husema:
‘Aamiyn’
kwa sauti na huku akiirefusha sauti yake[1]
Pia alikuwa akiwaamrisha wenye kumfuata Mamuumiyn waseme Aamiyn, kwa kusema: ((Imaam ataposema:
“Ghayril Magh-dhuubi ‘alayhim waladh dhwaaaaaalliyyyyyyn”
“Sio waliokasirikiwa wala waliopotea”
basi semeni: ‘Aamiyn’ [kwani Malaika na wao pia huwa wanasema: ‘Aamiyn’ na hakika Imaam anasema: 'Aamiyn']))
Katika usemi mwengine: ((Imaam atakaposema ‘Aamiyn’ basi na nyinyi semeni: ‘Aamiyn’ - kwani itakayeafiki ‘Aamiyn’ yake na ‘Aamiyn’ ya Malaika - [katika usemi mwengine] ((Anaposema Mmoja wenu katika Swalah ‘Aamiyn’ na Malaika mbinguni wakasema ‘Aamiyn’, zikaafikiana moja na nyingine, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia))[2]
Na Katika Hadiyth nyingine, ((Semeni: Aamiyn, Allaah Atakujibuni))[3]
Na alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: ((Mayahudi hawakuoneeni choyo kwa jambo lo lote lile zaidi kama wanavyoona choyo kwa kutoleana saalam na kuitikia Aamiyn [nyuma ya Imaam]))[4]
[1] Al-Bukhaairy katika Juz' Al-Qiraah na Abu Daawuud kwa isnaad Swahiyh.
[2] Ash-Shaykhaan na An-Nasaaiy na Ad-Daarimy. Maneno yaliyozidi yameripotiwa na wawili wa mwisho na ni dalili kuwa Hadiyth hii haiwezi kuthibitisha kuwa Imaam hasemi ‘Aamiyn’ kama ilivyoripotiwa na Maalik, hivyo Ibn Hajar anasema katika Fat-h Al-Baariy: "Inaonyesha dhahiri kwamba Imaam anasema ‘Aamiyn’ ". Ibn 'Abdil Barr anasema katika Tamhiyd (7/13), "Ni rai ya Waislamu wengi pamoja na Maalik kama watu wa Madiynah walivyosimulia kutoka kwake, kwani ni Swahiyh kutoka kwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) kutokana na Hadiyth ya Abu Hurayrah (ambayo ni hii) na ile ya Waail Ibn Hujr (yaani ya nyuma yake)"
[3] Muslim na Abu Aawaanah.
[4] Al-Bukhaariy katika Al-Adaab Al-Mufrad, Ibn Maajah, Ibn Khuzaymah, Ahmad na Siraaj kwa isnaad mbili na zote ni Swahiyh.
TANBIHI:
‘Aamiyn’ ya Maamuumiyn nyuma ya Imaam inakuwa kwa sauti na inakuwa inaletwa pamoja na ‘Aamiyn’ ya Imaam, na wala hawamtangulii kama wafanyavyo waswaliji wengi, na wala hawaicheleweshi na ‘Aamiyn’ ya Imaam. Hii ndio iliyokuwa Raajih (na nguvu kwangu) kama nilivyoihakiki katika baadhi ya vitabu vyangu; miongoni mwake ni ‘Silsilat al-Ahaadityh Adh-Dhwa'iyfah’ (Namba. 952 Mjalada 2) ambayo imechapishwa kwa Fadhila Zake Allaah, na Swahiyh At-Targhiyb wat-Tarhiyb (1.205). Taz. Kiambatisho 6.