018-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Kisomo Chake (صلى الله عليه وآله وسلم) Baada Ya Al-Faatihah

 

 

KISOMO CHAKE (صلى الله عليه وآله وسلم) BAADA YA AL-FAATIHAH

 

Kisha, alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akisoma Surah nyingine baada ya al-Faatihah, na alikuwa akikirefusha hicho kisomo mara nyingine, na mara nyingine akikifupisha kwa sababu ya safari, au kikohozi, au maradhi au kilio cha mtoto.

 

Kama alivyosema Anas Ibn Maalik (رضي الله عنه): "Alifupisha[1] Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) siku moja katika Swalah ya Alfajiri" (Na Katika Hadiyth nyingine, "Aliswali (صلى الله عليه وآله وسلم) Swalah ya Asubuhi akasoma Surah mbili zilizo fupi sana katika Qur-aan)". Pakaulizwa: "Ewe Mjumbe wa Allaah, kwa nini umefupisha?" Akasema: ((Nimesikia kilio cha mtoto hivyo nimehisi kwamba mama yake yu pamoja na sisi anaswali, kwa hiyo nikataka kumpa wasaa mama yake kwa ajili yake))[2]

 

Na alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: ((Hakika mimi huingia katika Swalah hali ya kuwa ninataka kuirefusha, ninaposikia kilio cha mtoto, hufupisha Swalah yangu kwa kuelewa machungu makubwa ya mama yake kwa kilio chake))[3]

 

"Alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akianza kusoma kutoka mwanzo wa Surah, na aghlabu huimaliza"[4]    

 

Alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: ((Ipeni kila Surah sehemu yake katika Rukuu na Sujuud))[5]

 

Katika usemi mwengine: ((Kwa Kila Surah Raka’ah))[6]

 

Mara nyingine huigawa Surah katika Rakaa mbili[7] na mara nyingine huirudia yote nzima katika Raka’ah ya pili.[8]

 

Mara nyingine alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akiunganisha katika Rakaah baina  Surah mbili au zaidi.[9]

 

Mtu Mmoja katika Answaar alikuwa akiswalisha katika Msikiti wa Qubaa, na alikuwa kila anapoanza kuwasomea Surah[10] katika Swalah baada ya al-Faatihah, huanza kwa ‘Qul Huwa Llaahu Ahad’ [Suratul-Ikhlaasw: 112] hadi mwisho, kisha anasoma Surah nyingine pamoja nayo, na alikuwa akifanya hivyo katika kila Raka’ah. wenzake walimuuliza kwa kusema: "Unaanza na Surah hii, kisha huoni kama inakutosheleza mpaka unasoma nyingine, basi chagua moja; isome hiyo pekee au iache na uisome nyingine". Akasema: "Sitoiacha, ikiwa mtapenda mimi nikuswalisheni (niwe Imaam wenu) kwayo, nitaendelea, lakini ikiwa mtachukiwa, sitokuswalisheni tena", na walikuwa wakimuona kuwa yeye ni mbora miongoni mwao, na pia hawakuwa wanapendekezewa kuswalishwa na mwenginewe. Na pindi alipokuja Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) wakamuelezea habari hiyo, Akasema (صلى الله عليه وآله وسلم): ((Ewe fulani, kipi kinachokuzuia kutekeleza wanayokuomba watu wako? Na Kipi kinachokupelekea kuwa lazima uisome Surah hii katika kila Raka’ah?)) Akasema: "Hakika Naipenda Surah hii" akasema (صلى الله عليه وآله وسلم): ((Mapenzi yako kwayo yatakuingiza Peponi))[11]

 

 

 



[1] Alifupisha Swalah kwa maana kuwa hakuirefusha, na katika Hadiyth hii na nyingine kama hii zinaonyesha kuruhusiwa watoto wadogo kuingia Misikitini. Ama Hadiyth iliyozagaa na kueleweka na wengi hadi kufikia kuwa inasemwa na kila mtu: "Watengeni mbali watoto wenu na Misikiti… "ni hadiyth dhwa'iyf na haiwezi kuwa ni dalili kabisa kwa mawafikiano yaliyopo. Na Miongoni mwa walisema kuwa ni dhwa'iyf ni: Ibn Al-Jawziy, Al-Mundhiriy, Al-Haythamiy, Ibn Hajar Al-'Asqalaaniy na Al-Buuswiyriy. Na akasema 'Abdul-Haqq Al-Ishbiyliy: "Haina asili"

[2] Ahmad kwa isnaad Swahiyh. Na Hadiyth nyingine imepokelewa na Ibn Abi Daawuud katika al-Maswaahif (4/14/2).

[3] Al-Bukhaariy Na Muslim   

[4] Linathibitishwa hili na Hadiyth nyingi zilizotajwa mbele.

[5] Ibn Abi Shaybah (1/100/1), Ahmad na 'Abdul-Ghaniy Al-Maqdisiy katika Sunan (9/2) kwa isnaad Swahiyh.

[6] Ibn Naswr na At-Twahaawiy kwa isnaad Swahiyh. Maana ya Hadiyth kwangu ni: Jaaliyeni kwa kila Rakaa Surah kamili, ili Rakaa iwe na hadhi yake kamili kwa hiyo Surah! Amri hii ni pendekezo na sio lazima utekelezaji wake kutokana na dalili inayofuatia.

[7] Ahmad na Abu Ya'ala kutoka njia mbili. Pia tazama "kisomo katika Swalah ya Alfajiri'

[8] Kama alivyofanya katitka Swalah ya Alfajiri, kama itakavyofuatia.

[9] Maelezo yake na vyanzo vyake vitafuatia karibuni.

[10] Yaani miongoni mwa Surah baada ya al-Faatihah.

[11] Al-Bukhaairy ameipokea ta'liyqan (ni hadiyth inayoondoshwa mwanzo wa isnaad yake Msimulizi mmoja au zaidi kwa mfululizo); na At-Tirmidhiy ameipokea Mawswuulan (ni hadiyth inayoungana isnaad yake, iwe imemalizika kwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) au kwa Swahaba), na At-Tirmidhiy akasema: ni Swahiyh.

Share