Msimamizi Wa Kampuni Na Kila Ninapowapa Kazi Vibarua Hunipa Posho Ni Sawa Kupokea?

 

SWALI:

 

Asalaam alaikum, mimi nina fanya kazi kama supervisor ambaye hugawa na kusimamia kazi mbali mbali, lakini kuna kitu ambacho kinanitia shaka katika kazi yangu kwani kila ninapotoa kazi kuwapa jamaa wafanye wakimaliza wanaamuwa kunipa sehemu fulani ya ujira wao eti kama hela ya soda mimi hukataa kwani kazi wanayofanya wao ni ngumu halafu  wanachopata ni kidogo bado wanataka nipokee. Sasa je kupokea pesa hiyo ni halali kwangu, je haifanani na kile kisa cha yule swahaba aliyekwenda kukusanya kodi akapewa zawadi ambayo rasulullah aliiona kama haikumstahili. Naogopa nisije nikachafua chumo langu nshallah.


 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukran zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kupatiwa marupurupu katika kazi unayofanya. Bila shaka yoyote ni kuwa suala lako na la Swahaba uliyemtaja halifanani wala kulingana. Tofauti iko wazi kuwa yule Swahaba alijigawanyia cha kwake na cha dola ambapo wewe hukujigawanyia wala kuchukua kitu maalumu wala kuwaambia kuwa mkifanya basi mnipatie changu kiasi kadhaa. Kwa hiyo, pesa unayopata ni halali.

 

Mbali na kusema hayo ni lazima uwe mwanadamu na uwe na utu wa kutazama yanayowafika vibaruwa. Kulingana na swali lako umejitokeza ubinadamu na utu kwa kuwafikiria wenye kupata pato la chini. Kwa rai yetu ni kuwa uwe na msimamo huo wa kuwasaidia Waislamu na hata wasiokuwa Waislamu kupata kibarua na kutochukua chochote kutoka kwao. Hii ni njia moja ya Da‘wah kwani muamala wako huo wa Kiislamu unaweza kuwavutia wasio Waislamu, na wale Waislamu wasiotekeleza Uislamu wao vyema, na pia kuwazidisha Imani wale ambao wana udhaifu kiasi Fulani na kuwapatia moyo wale walio na Imani barabara.

 

Tunakupatia hongera kwa msimamo wako huo na endelea hivyo hivyo kutochukua kutoka kwao pesa hizo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share