Kukopa Gari Benki Kwa Ribaa Ikiwa Hakuna Taasisi Za Kukopesha Waislam

 

SWALI:

 

Asalam aleykum mi nauliza kama nimekopa gari bank na nalipa pamoja na riba je inafaa kwa mwislam kukopa bank? Je na kama hakuna taasisi ya kukopa bila riba tufanyeje naomba msaada kwa hilo.


 

JIBU:

 

AlhamduliLlaah - Himdi Na Sifa Zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kukopa mkopo bank na kulipa pamoja na ribaa.

Haifai kabisa kwa Muislamu kukopa kutoka katika benki yenye kulipisha ribaa kwa hali yoyote ile isipokuwa ikiwa ni dharura kubwa sana ya uhai au kifo.

 

Gari si vyombo muhimu sana katika maisha ya mwanaadamu, naye hivyo anaweza kuishi bila kuwa na gari kama wengi wanavyoishi. Kwa hiyo, ikiwa hakuna mtu au taasisi inayoweza kumkopesha bila ya ribaa ni afadhali akae bila ya gari kuliko kupigana vita na Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Allaah Aliyetukuka Anasema:

Basi mkitofanya jitangazieni vita na Allaah na Mtume Wake” (al-Baqarah [2]: 279).

Na madhara yake ni kama Anavyosema Aliyetukuka:

Wale walao ribaa hawasimami ila kama anavyosimama aliyezugwa na Shaytwaan kwa kumgusa” (al-Baqarah [2]: 275).

 

Dharura ambayo inaweza kukubalika kisheria ni kama vile mfano wa mtu aliyekosa chakula kabisa na hakuna ila nyama ya nguruwe. Anasema Aliyetukuka:

Amekuharimishieni nyamafu tu, na damu, na nyama ya nguruwe, na mnyama aliyechinjwa kwa ajili isiyokuwa ya Allaah. Lakini anayelazimishwa bila ya kuasi, wala kuruka mipaka, basi hakika Allaah ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu” (an-Nahl [16]: 115).

 

Hapo sheria imemruhusu ale kidogo tu cha kumuwezesha kubaki katika uhai. Na kukopesha kwa ribaa nayo ni hivyo hivyo, kuokoa maisha.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share