Kutoa Rushwa Kwa Ajili Ya Kupata Nyumba Ya Serikali

 

 

SWALI:

huku tunakoishi kuna watu hujiandikisha katika shirika la njumba kwa siku nyingi it ili zikitoka nyumba wapewe wao kwa jili ya kodi zao ni rahisi. Kulinganisha na nyumba ya mtu bi nafsi ni ghali. sasa wamitokea watu hutowa pesa mahali hapo kwa watu wanofanya kazi. ili wawaandikishe wao kama wamejiunga na wao zamani. ili zikitoka nyumba nzuri wapate wao. je his rushwa na naomba kujua muda wamtu atakapo laaniwa kwa mada hii.

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Hakika hili ni tatizo kubwa la kijamii katika nchi zetu kwa kuwa matajiri na wenye vyeo ndio wenye kutajirika zaidi na walio masikini kubaki katika ufukara wao. Hii ni njia moja ya kudhumu watu wanaostahiki kupata huduma fulani kama hiyo ya kuweza kununua viwanja kwa bei iliyo nafuu.

Ni maarufu kuwa katika Uislamu haramu haiwi halali ila iwe ni mas-ala ya kuokoa maisha au kujiokoa na kifo. Kuchukua rushwa ni mojawapo ya njia za kula mali za watu kwa batili, nayo ni kile kinachotolewa katika mali kupewa mwenye cheo au kazi serikalini ili ampe haki isiyokuwa yake. Uislamu umemharamishia Muislamu kutoa rushwa (hongo) kuwapa viongozi na wasaidizi wao kama vile ilivyoharamisha hao viongozi kuchukua mlungura (rushwa) kwa njia yoyote ile. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema: “Wala msiliane mali zenu kwa batili na kuzipeleka kwa mahakimu ili mpate kula sehemu ya mali ya watu kwa dhambi na hali mnajua” (2: 188).

 Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Allaah Amemlaani mwenye kuhonga na mwenye kuhongwa katika hukumu” (Ahmad, at-Tirmidhiy a Ibn Hibbaan). Pia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewalaani: “Mtoa rushwa na mlaji rushwa na tarishi baina yao” (Ahmad na al-Haakim).

Kwa hivyo, tunawanasihi ndugu zetu wasiwe ni wenye kutoa wala kupokea rushwa kwani aliyelaaniwa na Allaah Aliyetukuka hatapata mafanikio yoyote hapa dunia na atakosa rehma za Allaah Aliyetukuka Kesho Akhera. Tujihadhari sana katika hilo.

 Na Allaah Anajua zaidi

 

Share