Mkopo Wa Nyumba Wa Benki (Mortgage) Ni Halaal?
SWALI:
Assalaam Alykum,
Jina langu ni ………. na punde tu nimejaza uanachama wa Alhidaaya ili niwe napokea jarida la Alhidaaya. Kwa bahati nzuri ni miongoni mwa Waislamu waishio ughaibuni na kwa sasa niko Marekani. Nimejaaliwa kuoa muislamu aliyezaliwa na kulelewa katika maisha haya na Alhamdulillah namshukuru Allah kwani kuwa kwetu pamoja kumeniongeza imani na kujua mengi. Allah aidumishe ndoa yetu na tuendelee kupata kizazi chema.
Katika kutafuta maisha na kujitayarishia makazi ya hapa nimepata ushawishi wa karibu wa kutaka kununua nyumba. Hasa kwa vile ikhwaan wengi ninao wafahamu hapa wameingia kwenye biashara hiyo ya kujitafutia makazi wao na ahli zao. Baada ya maswali mengi niliyowauliza nimeona kuwa katika ununuaji wa nyumba hizi kuna ribaa kubwa sana na kwa ufupi hili limenirudisha nyuma kwani kwa ninavyofahamu mimi na familia yangu na waislamu wengi ninaowafahamu ribaa ni ribaa tu hata ikiwa ndogo au kubwa.
Wengi niliozungumza nao majibu yao yalikuwa haya; hapa tulipo huwezi kupata benki ya Kiislamu ikakupa mkopo wa nyumba. Na baadhi ya majibu yao yalikuwa ni haya; kama ni ribaa ipo kila kona unapolipa tax unalipa ribaa, unapokaa kwenye apartment unalipa ribaa na hata unapofanya shoping ya vitu vyako vya kawaiada unalipa ribaa. Sikutaka kuuliza zaidi hizi ribaa walizozitaja wao zinapatikana vipi kwani niliona nijiweke mbali kidogo ili wapunguze jazba waliyokuwa nayo wakati wa kuuliza maswali yangu. Na jibu la mwisho lilikuwa ni hili sisi tuna kizazi hapa ni lazima tuwatayarishie makazi yao baadae kwa hiyo kununua nyumba ni lazima kwani si kwa ajili yetu tu bali kwa wao na kwa kizazi kinachokuja.
Swali langu liko hapa je kama mimi na wengine walioko ughaibuni wanataka kununua nyumba ni njia gani tufanye ili tuepuke na ribaa. Na je hawa ndugu zetu wanaonunua nyumba wako sawa kwa mujibu wa maelezo yao.
Nashukuru kwa muda wenu na natanguliza shukrani za dhati.
Nduguyo katika Uislam
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Ni hakika kuwa Uislamu umeruhusu kukuzwa kwa mali kwa njia ya biashara. Amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَأْكُلُوا أَمْوَالَكُم بَيْنَكُم بِالْبَاطِلِ إِلَّا أَن تَكُونَ تِجَارَةً عَن تَرَاضٍ مِّنكُمْ ۚ وَلَا تَقْتُلُوا أَنفُسَكُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِكُمْ رَحِيمًا ﴿٢٩﴾
Enyi walioamini! Msiliane mali zenu kwa ubatilifu, isipokuwa iwe biashara kwa kuridhiana baina yenu. Wala msijiue. Hakika Allaah ni Mwenye kuwarehemuni. [An-Nisaa: 29]
Lakini Uislamu umeziba njia mbele ya kila anayejaribu kuikuza mali yake kwa njia ya ribaa au haramu nyingine. Ukaharamisha uchache na wingi wake na kuwakarapia Mayahudi kuchukua kwao ribaa japokuwa wamekatazwa. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:
وَأَخْذِهِمُ الرِّبَا وَقَدْ نُهُوا عَنْهُ وَأَكْلِهِمْ أَمْوَالَ النَّاسِ بِالْبَاطِلِ ۚ وَأَعْتَدْنَا لِلْكَافِرِينَ مِنْهُمْ عَذَابًا أَلِيمًا ﴿١٦١﴾
Na kuchukua kwao ribaa na hali walikatazwa kuichukua; na kula kwao mali za watu kwa ubatilifu. Na Tumeandalia kwa makafiri miongoni mwao adhabu iumizayo. [An-Nisaa: 161]
Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ameteremsha Aayah kali sana kuhusiana na wanaochukua ribaa:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَذَرُوا مَا بَقِيَ مِنَ الرِّبَا إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ﴿٢٧٨﴾
Enyi walioamini! Mcheni Allaah na acheni yaliyobakia katika ribaa ikiwa nyinyi ni Waumini.
فَإِن لَّمْ تَفْعَلُوا فَأْذَنُوا بِحَرْبٍ مِّنَ اللَّـهِ وَرَسُولِهِ ۖ وَإِن تُبْتُمْ فَلَكُمْ رُءُوسُ أَمْوَالِكُمْ لَا تَظْلِمُونَ وَلَا تُظْلَمُونَ ﴿٢٧٩﴾
Na msipofanya basi tangazeni vita kutoka kwa Allaah na Rasuli Wake. Na mkitubu basi mtapata rasilimali zenu msidhulumu na wala msidhulumiwe. [Al-Baqarah: 278-279]
Hukumu ya ribaa ni kuwa imeharamishwa kwa kauli ya Aliyetukuka:
الَّذِينَ يَأْكُلُونَ الرِّبَا لَا يَقُومُونَ إِلَّا كَمَا يَقُومُ الَّذِي يَتَخَبَّطُهُ الشَّيْطَانُ مِنَ الْمَسِّ ۚ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَالُوا إِنَّمَا الْبَيْعُ مِثْلُ الرِّبَا ۗ وَأَحَلَّ اللَّـهُ الْبَيْعَ وَحَرَّمَ الرِّبَا ۚ فَمَن جَاءَهُ مَوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّهِ فَانتَهَىٰ فَلَهُ مَا سَلَفَ وَأَمْرُهُ إِلَى اللَّـهِ ۖ وَمَنْ عَادَ فَأُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ ۖ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿٢٧٥﴾
Wale wanaokula ribaa hawatosimama (Siku ya Qiyaamah) ila kama anavyosimama yule aliyezugwa na shaytwaan kwa kuguswa na kupatwa. Hivyo kwa sababu wao wamesema: “Hakika biashara ni kama ribaa.” Na Allaah Amehalalisha biashara na Ameharamisha ribaa. Basi atakayefikiwa na mawaidha kutoka kwa Rabb wake akakoma; basi ni yake yale yaliyopita, na hukumu yake iko kwa Allaah. Na atakayerudia basi hao ni watu wa motoni, wao humo ni wenye kudumu. [Al-Baqarah: 275]
Pia amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
“Allaah Amelaani mwenye kula ribaa, mwenye kuitoa, mashahidi wake na mwandishi wake” [Ahmad, Abu Daawuud, At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy na Ibn Maajah]
Amesema tena Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
“Dirhamu moja ya ribaa anayokula mtu naye anajua ni mbaya zaidi kuliko kuzini mara 36” [Ahmad kwa Isnadi sahihi]
Na pia: ((Ribaa ina milango 73, iliyo nyepesi zaidi ni mtu kumuoa mamake)) (Al-Haakim, naye akaisahihisha).
Na kauli yake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Jiepusheni na maangamivu saba”. Pakasemwa: Ee Mjumbe wa Allaah! ni yepi hayo? Akasema: “kula ribaa” [Al-Bukhaariy na Muslim]
Hekima ya kuharamishwa:
Kwa hekima zilizo dhahiri katika kuharamishwa ribaa ni ziada kwa hekima za kijumla katika amali zote za kisheria nao ni mtihani wa Imani kwa mja katika utiifu wake. Na katika hilo ni kuchunga maslahi ya wanaadamu katika mwenendo wake. Wanachuoni wametaja sababu za kiakili za kuharamishwa kwa ribaa, zilizodhihirika kwa elimu za kisasa kuthibitishwa juu ya zile zilizotajwa na Allaah. miongoni mwazo ni:
1. Kuhifadhi mali ya Muislam ili isiliwe kwa batili.
2. Inamtaka mtu achukue mali ya mwenzake bila kumpa chochote badili yake, kwani mwenye kutoa dirhamu moja apate mbili huwa amejipatia dirhamu moja zaidi bila ya kutoa chochote.
3. Kutegemea ribaa kunawazuia watu wasishughulike na kutafuta mapato. Huu ni katika upande wa kiuchumi.
4. Huondosha hisani iliyopo baina ya watu kutokana na kukopeshana. Huu ni upande wa akhlaaq na tabia njema.
5. Ribaa inawaendeleza matajiri kuzidi kuwanyonya masikini, hivyo tajiri huzidi kuwa tajiri na masikini huzidi kuwa masikini.
6. Kufunga njia za kueneza uadui na mashaka baina ya Waislam walio ndugu na kuwasababishia ghadhabu na chuki baina yao.
7. Kumuepusha Muislam katika kuzalisha mali yake katika njia ya ya mkato na udanganyifu.
8. Kumuepusha Muislamu na kinachompelekea katika kuhiliki. Anapokula ribaa anaingia katika dhulma na mwisho wake unakuwa mbaya sana. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Iogopeni dhulma, kwani dhulma itampelekea mwenye kuifanya kuwa katika kiza Siku ya Qiyaamah” (Muslim).
9. Kukopesha bila ribaa kunafungua milango ya wema baina ya Waislamu, hivyo kujikurubisha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala). Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:
وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖ وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ ۚ
Na shirikianeni katika wema na taqwa, na wala msishirikiane katika dhambi na uadui. [Al-Maaidah: 2]
Tufahamu kuwa haramu ni haramu, ndio Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:
“Kileweshacho wingi wake basi uchache wake ni haramu” [Ahmad, Abu Daawuud na At-Tirmidhiy]
Hivyo, ribaa inapokuwa kidogo au nyingi yote inaingia katika uharamu ambao Waislam hawafai kuingia ndani yake.
Sisi wanaadamu tumeumbwa tukiwa dhaifu sana. Kwa hiyo, huwa ima tunatafuta vipengele vya kuhalalisha haramu au kuona jambo hilo halina shida yoyote. Ni jambo linaloeleweka kuwa tax (ushuru), ijara ya nyumba, unaponunua vitu dukani hakuna ribaa yoyote kabisa unayolipa. Huenda vitu hivyo vikaongezewa tax ambayo inarudishwa kwa serikali na wala sio ribaa. Inafaa tutafautishe baina ya ribaa na ushuru. Hivi ni vitu viwili tofauti kabisa. Ushuru mara nyingi hata kwa serikali za kwetu Afrika Mashariki huwa inatumiwa na serikali kuboresha huduma za wakaazi wake wa nchi hiyo. Na katika nchi za kimagharibi huwa ushuru unatumika hata kuwasaidia watu ambao si wananchi lakini wamekimbilia huko kwa sababu moja au nyengine na pia kuwasaidia wasio na kazi n.k.. Ribaa si huduma bali ni unyonyaji wa hali ya juu dhidi ya mafukara.
Hakika ni kuwa baadhi ya Waislam wameingia katika ribaa pindi wanapochukua mkopo kutoka benki au taasisi nyengine yoyote inayotoa mikopo kwa ribaa ili kufanyia shughuli yoyote, au kununua nyumba kwa udundulizi au rehani (mortgage). Katika hilo wamechukua fatwa kutoka kwa wenye kusahilisha na kudai kuwa hilo linaruhusiwa kwa wasiokuwa na nyumba kwa sababu za dharura na kwa sababu eti kulipa kodi ya nyumba kunamdhuru Muislam maana pesa yake inapotea lakini mogeji pesa inahifadhika!
Wakalinganisha (Qiyaas) hilo na kula nyamafu kwa kuhofia mauti kwa nafsi yake. Hali hizo mbili zipo mbali sana baina ya mbingu na ardhi. Mwenye njaa anahofia umauti ameruhusiwa kula nyamafu ili kuondoa mauti ambayo yamemkabili kwa nafsi yake. Ama yule ambaye hana maskani hana khofu kuwa atakufa kwa kukosa nyumba. Anaweza kuishi katika nyumba ya kuajiri (kukodisha), kijijini au mjini, nyumba ndogo au kubwa kulingana na uwezo wake, au akarudi alipotoka katika nchi yake na si lazima ajing'ang'anize Ulaya au Marekani kwa kukhofia maisha ya Afrika.
Hakika ni kuwa kuna watu wanaishi hata katika mahema. Na kufanya hivyo ni kheri kwake mtu kuliko kuchukua mkopo wa ribaa na kujiweka katika kupigana vita na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na Mtume Wake.
Huenda huyu mdaiwa akashindwa kulipa deni, hivyo deni kuzidi juu ya matarajio yako. Benki huwa hazitaki kusikia kuwa mimi sasa sina kazi, au mshahara umepunguzwa au nilitumia pesa kwa shida na matatizo mengine. Hayo na yako, wao wanataka pesa mlizosikilizana kwa kila mwezi. Pesa hizo utazitowa wapi ni shauri yako. Tatizo hilo likitokea basi ufakiri utazidi, pia huenda ukauza nyumba hiyo au benki ikaiuza na faida juu yake na pesa zote zinakuwa ni zao nawe unaruka patupu. Pesa zote zinakwenda benki au kwa ambayo ndio ilikukopesha au ilisimamia mkataba wako na mwenye nyumba.
Nchi kadhaa kama Phillipine, Mexico, Thailand na kadhalika uchumi wao uliharibika kwa sababu ya kuchukua mikopo ya ribaa kutoka kwa Benki ya Dunia au IMF, kisha wakashindwa kulipa. Na wangapi tumewaona waliochukua mikopo kwa ajili ya kuendesha biashara au kununua nyumba, biashara ikaharibika na kuondoka au nyumba kuikosa. Mfano hai ni hivi karibuni Muislam mwenye mabasi marufu Tanzania wadeni wake waliyashika mabasi yake mazuri kwa sababu ya kutolipa kwa muda ufaao, hivyo ikasababisha biashara yake kurudi nyuma sana.
Benki mara nyingi haitoi mkopo mpaka uwe na dhamana kwa sababu wao hawakubali kupata hasara kwa namna yoyote ile. Katika hilo unafaa uweke kwao hati ya nyumba nyengine, log book ya gari au kitu chochote chenye thamani ya mkopo unaochukua. Ukikosa tu kulipa kwa muda mlioandikiana ulichoweka kwao rehani kinauzwa ili warudishe deni lao. Hii ni dhulma ya hali ya juu kwani wewe huwa umelipa baadhi ya deni na kushindwa kwako kulipa basi kutapelekea kila kitu chako ulichowekesha kitoweke.
Kuhusu kipande cha mwisho kuwa tutafanya nini katika hali hiyo? Kitu cha kwanza ni kuwa ni lazima Waislam sehemu hiyo mushikamane na kuangalia tatizo hilo mnaweza kulitatua namna gani. Hilo ni kuwa nyinyi ndio mnayaelewa zaidi mazingira yenu ya huko. Hivyo suluhisho litatoka kwenu wenyewe na si lazima kuwe na benki ya Kiislam. Lakini baadhi ya sehemu huko Tanzania na Kenya watu wanafanya moja kati ya haya hapa chini:
1. Kuanzisha vikundi vya kusaidiana kukopeshana. Baada ya muda mmoja anaweza kukopesha pesa za kiwango ambacho yeye ataka kufanya jambo fulani. Akichukua mkopo atakuwa analipa polepole bila kuwa na haja ya kulipa ziada. Kwa njia hii kunawezwa kufanya mengi kwa uwezo wa Allaah Aliyetukuka.
2. Kuwakinaisha matajiri Waislamu na kuwaeleza umuhimu wa kujenga nyumba na kuweza kuwauzia Waislamu. Hili linafanyika huko Nairobi na Waislamu wanaweza kulipa polepole kwa kiwango ambacho wataridhiana.
Au njia nyengine yoyote ya halali.
Na Waislam wakiwa na moyo wa kuepuka haramu basi Allaah Aliyetukuka huwatolea njia ya kuweza kuondoka katika matatizo. Allaah Aliyetukuka Anasema:
وَمَن يَتَّقِ اللَّـهَ يَجْعَل لَّهُ مَخْرَجًا﴿٢﴾
Na yeyote anayemcha Allaah; Atamjaalia njia ya kutoka (shidani).
وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ لَا يَحْتَسِبُ ۚ
Na Atamruzuku kutoka njia ambayo hatizamii… [At-Twalaaq: 2-3]
Na Allaah Anajua zaidi