Amechukua Faida Katika Kumpatia Mteja Huduma, Je, Ni Ribaa?

SWALI:

 

Hakika kila Sifa njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Assalaamu Aleykum.


Swali langu ni kama ifuatayo. Je mimi nikiwa Mwajiriwa na ninafanya kazi ya mwajiri wangu na katika hiyo kazi ninayo fanya Akatokea Mteja wangu akahitaji huduma na ile huduma anayo hitaji huyo mteja sina itanibidi nimtafutie kwa watu wengine kisha nikamwuzia. Baada ya kumwuzia na nikapokea pesa kisha nimpelekee pesa yake kwa yule mtu niliye chukua ile huduma ambaye mimi nilikuwa sina na nikachukua faida kidogo nileyepata kutokana na ile huduma. Bila kujua Mwajiri wangu. Je nitakuwa mwenye kula Haram au Riba?


Jazakumullaahu kheyran.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu biashara na riba. Awali ya yote inatakiwa tufahamu kuwa biashara na riba ni vitu viwili tofauti kabisa. Biashara ni halali na riba ni haramu japokuwa wenye kutaka kuhalalisha riba huwa wanasema riba pia ni biashara.

Allaah Aliyetukuka Anafuhamisha:

 

"Haya ni kwa sababu wanasema: 'Biashara ni kama riba', hali Allaah Amehalalisha biashara na kuharamisha riba" (2: 275).

 

Tofauti ya hizo mbili ni wazi kwani riba ni unyanyasi wa hasa walio wanyonge kwa kuwakopesha kwa maslahi yao lakini wakawatoza ziada ambayo inazidi kuwafanya wabaki katika umaskini. Tufahamu kuwa Allaah Aliyetukuka Akihalalisha kitu au Akiharamisha huwa ni kwa ajili ya maslahi yetu sisi wenyewe.

 

Hayo uliyoyaeleza hapo juu hayana shida na hiyo ni katika biashara kwa njia ya kuwa unanunua kutoka sehemu nyingine na kuuza kwa faida. Kufanya hivyo ni halali kabisa wala hakuna mushkila wowote katika sheria. Mushkila unakuja kuwa wewe ni muajiriwa wa mtu ambaye anakulipa ajira na kukutaka ufanye kazi za biashara yake. Ni katika adabu za uajiriwa kutompunja mwajiri wako kwa njia yoyote ile. Hivyo, ikiwa huna kweli bidhaa hiyo katika duka unalouza itabidi umtafute huyo mteja bidhaa anayotaka katika wakati usio wa kazi katika duka unalofanya. Ima uende katika wakati wa kula au baada ya kazi.

 

Ushauri wetu ni kuwa ikitokea hali ya kuwa hakuna bidhaa katika duka unalouza mwambie mwenye duka (mwajiri wako) kuwa kuna mteja hapa anataka bidhaa lakini hakuna. Kisha umwambie inapopatikana hiyo bidhaa na bei yake na bei ambayo mnaweza kumuuzia huyo mteja. Kwa kufanya hivyo utaonyesha uaminifu wako kwa mwajiri wako na hilo laweza kukufanya wewe uwe ni mwenye kuaminiwa na hata kupandishwa cheo katika kazi hapo kwake. Hata ikiwa hutapata hilo utapata makubwa kwa Allaah Aliyetukuka.

 

Kwa muhtasari ni kuwa zipo njia mbili ambazo unaweza kufanya na katika zote hizo utakuwa uko bado katika biashara na hutaingia kabisa katika riba ya aina yoyote ile.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share