Bibilia Imetaja Kuhusu Ribaa?
SWALI:
Assalaamu alaykum warahmatullah
Tafadhali nakuombeni munipatie aya ndani ya Bibilia zinazozungumzia mikopo na riba, kama inawezekana Inshaallah.
Jazaakallahul khair
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kupatiwa mistari katika Biblia inayozungumzia kuhusu mikopo na Ribaa.
Mwanzo tuanze na Qur-aan inavyosema kuhusu kukatazwa kwa Mayahudi kuchukua RibaA. Allaah Aliyetukuka Anasema:
“Na kuchukua kwao Ribaa, nao wamekatazwa, na kula kwao mali ya watu kwa dhulma. Basi Tumewaandalia makafiri katika wao adhabu yenye uchungu” (an-Nisaa’ 4: 161).
Ama katika Biblia zipo aya mbili katika vitabu tofauti, moja ikikataza kuchukua Ribaa kwa maskini na nyingine ikitoa ruhusa kuchukua Ribaa kwa asiyekuwa Muisraili. Hizi ni baadhi ya hizo aya:
1. “Ukimkopesha fedha mtu yeyote miongoni ma watu wangu walio maskini, usiwe kwake kama mdai, wala usimtoze riba. Ukilichukua vazi la mwenzako kuliweka rehani, lazima umrudishie kabla ya jua kutua, kwa kuwa hiyo ndiyo nguo yake ya pekee; ndiyo atakayojifunika nayo. Au wadhani atalalia nini? Akinililia nitamsikiliza, maana mimi ni mwenye huruma” (Kutoka 22: 25 – 27).
2. “Unaweza kutoza riba unapomkopesha mgeni, lakini ndugu yako Mwisraeli usimtoze riba, naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, atakubariki katika shughuli zako zote utakazofanya katika nchi ambayo unakwenda kuimiliki” (Kumbukumbu la Sheria 23: 20).
Na Allaah Anajua zaidi