Tunaomba Du’aa Pamoja Kwa Ajili Ya Mitihani Inafaa?

 

Tunaomba Du’aa Pamoja Kwa Ajili Ya Mitihani Inafaa?

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Asalamu Aleykum Warahmatullahy Wabarakatuh

 

Mimi ni mwanachuo, huwa tuna kawaida ya kuomba dua ya pamoja inapokaribia kipindi cha mitihani (Dua ya kuanza na kumaliza mitihani) katika jumuiya yetu ya waislamu hapa chuoni. Naomba munifafanulie ili niweze kuijua haki kwani kuna wale wanaona haifai kwani haikuthibiti na wengine wanasema inafaa kwa kusema mbona Mtume s.a.w aliomba mvua?

 

Namuomba Allaah S.w. Awafanyie Wepesi Katika Kazi Zenu Ili Muweze Kunijibu Mapema Inshaallah.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta’ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja NAbiy. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea.  

 

 

Mas-ala ya du’aa ni suala muhimu katika Uislamu kwani yamehimizwa sana kwa Aayah na Hadiyth tofauti. Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ ۖ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ ﴿١٨٦﴾

Na watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi ni Niko karibu (kwa ujuzi); Naitikia du’aa ya muombaji anaponiomba. Basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi, wapate kuongoka. [Al-Baqarah: 186].

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

Duaa ni ‘Ibaadah, kisha akasoma: (Ghaafir: 60)[at-Tirmidhiy].

وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ ۚ

Na Rabb wenu Amesema: Niombeni, Nitakuitikieni. [Ghaafir:60]

 

Duaa iliyo bora ni mtu mwenyewe kumuomba Allaah Aliyetukuka hasa katika nyakati ambazo du’aa hujibiwa. Mfano ni kuinuka usiku na kuswali Tahajjud kisha ukaomba, baina ya Adhana na (Iqaamah) Swalah, wakati unapofunga Swawm, na kadhalika. Na kwa sababu unafanya mtihani maombi yako kwa Allaah Aliyetukuka yatakuwa:

 

“Ee, Allaah Nijaalie nipite mtihani wangu, Ee Allaah nizidishie elimu”.

 

Vile vile du’aa zifuatazo  za Qur-aan na Sunnah anaweza kuomba kila mmoja wenu:  

 

 

Katika Qur-aan: 

 

قَالَ رَبِّ اشْرَحْ لِي صَدْرِي ﴿٢٥﴾وَيَسِّرْ لِي أَمْرِي ﴿٢٦﴾ وَاحْلُلْ عُقْدَةً مِّن لِّسَانِي ﴿٢٧﴾ يَفْقَهُوا قَوْلِي ﴿٢٨﴾

(Muwsaa) Akasema: Rabb wangu, Nikunjulie kifua changu. Na niwepesishie shughuli yangu. Na fungua fundo (la kigugumizi) katika ulimi wangu. Ili wafahamu kauli yangu. [Twaahaa 25 – 28]

 رَّبِّ زِدْنِي عِلْمًا 

Rabb wangu! Nizidishie elimu. [Twaaha: 114]

 

Katika Sunnah ni du’aa ambayo mtu anapokabiliwa na jambo gumu: 

 

اللّهُـمَّ لا سَـهْلَ إِلاّ ما جَعَلـتَهُ سَهـلاً، وَأَنْتَ تَجْـعَلُ الْحَـزَنَ إِذا شِـئْتَ سَهـْلاً

Allaahumma laa sahla illa maa Ja’latahu sahlan, wa Anta Taj’alul-hazna idhaa shi-ita sahla.

"Ee Allah hakuna jepesi ila Ulilolifanya jepesi, Nawe Unalifanya gumu jepesi ukitaka".

 

 

Hilo ndio lililo bora na mtu kufanya bidii kwanza ya kusoma na kisha aombe du’aa na vizuri na bora ni kujiombea mtu mwenyewe na pahali pazuri pa kuomba ni wakati wa kusujudu kwenye Swalaah na kabla ya kutoa Salaam. Pia hali hiyo ya kukusanyana kwa ajili ya du’aa, mbali na kuwa haikuthibiti, vilevile inawea kujenga nadharia ya kwamba mimi nitafanya mchezo kisha najua kuwa tutakutana na kuomba du’aa na Allaah Atanijaalia nipite. Ni nadharia ya wengi wafanyao hayo kabla ya mitihani na wengine hawaonekani wakati mwengine wote wa mwaka katika shughuli za Kiislamu za jumuiya lakini wanaonekana siku hiyo kwa sababu wana shida.

 

 

Kwa hiyo inatakiwa Waislamu wema wafanye juhudi ya kuwaelimisha wenziwao kuwa Allaah Aliyetukuka humsaidia mwenye kujisaidia. Hivyo, pamoja na du’aa ni muhimu kwa kila mmoja asome kwa bidii pamoja na kufanya ‘Ibaadah itakiwavyo.

 

 

Ama kufananisha jumuiko la kuomba kupita mitihani na du’aa ya mvua si sawa na hayo mawili hayalingani kabisa. Hayafanani kivipi? Hebu tutazame:

 

  1. Kuhusu mvua Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliiomba du’aa juu ya Minbar wakati wa khutbah siku ya Ijumaa (hapa si wakati wa Swaalah ya mvua, kwani Swaalah ya mvua inafanyika nje. Hii ilikuwa ziada ya maombi). Nanyi sijui kama mnamuambia Khatibu siku ya Ijumaa kabla ya mitihani awaombee watoto wa Kiislamu wanaofanya mithani?

  2. Du’aa ya mvua huwa inafuata baada ya Swaalah maalumu ya kuomba hilo. Wakati wa kuomba du’aa kupasi mitihani huwa hatuswali wala hakuna Swaalah ya kuomba kupita mitihani.

  3. Swaalah na du’aa yake ya mvua hufanyika nje ya mji sio Msikitini ilhali hilo hatufanyi tunapoomba kupita mitihani.

  4. Katika siku ya kuomba pamoja na Swaalah ya mvua wale waliohudhuria wanatakiwa wavae nguo zao ndani nje. Sijui hilo linafanywa wakati wa kuomba kupita mitihani.  

 

Kwa hiyo kulinganisha mambo hayo mawili si sawa kabisa.

 

Ingia katika viungo vifutavyo upate maelezo zaidi kuhusu makatazo ya jambo hilo:

 

Kualika Watu Kusoma Qur-aan Kuomba Haja

 

Kumuombea Du'aa Mgonjwa Kwa Mkusanyiko Inafaa?

 

Kusoma Du’aa Pamoja Baada Ya Swalah na Kuomba Du’aa Baada ya Mihadhara

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share