Kufanya Adhkaar Kwa Pamoja Inajuzu?
Kufanya Adhkaar Kwa Pamoja Inajuzu?
SWALI:
Assalam aleykum.. kwanza napenda to pongezi kwa kuanzisha website hii, inatusaidia sana hasa kwa sie tulio ughaibuni, Allaah (Subhanahu wa Ta'aalaa) awajaze majazo mema.
Swali langu ni hili... nilipokua nyumbani (tanzania) chuo chetu kilikua cha dhikri nadhani nikisema hivo utakua umenielewa... Nachotaka Kujua Sasa Je Dhikri Ni Halal Au La? Na Je Kama Ni Halal Au Haram Kuna Ushahidi Wowote? A.aleykum warahma tullah wabarakat..
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Hakika dhikr (utajo wa Allaah) ni jambo ambalo limehimizwa sana na Allaah Aliyetukuka na Nabiy wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Hata hivyo, njia ya kuifanya ndio inafanya iwe halali au haramu. Allaah Aliyetukuka Anasema kuhusu kumdhukuru:
لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّـهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ وَذَكَرَ اللَّـهَ كَثِيرًا ﴿٢١﴾
Kwa yakini mna kigezo kizuri kwa Rasuli wa Allaah kwa mwenye kumtaraji Allaah na Siku ya Mwisho na akamdhukuru Allaah kwa wingi. [Al-Ahzaab: 21].
Na Anasema pia:
...وَالذَّاكِرِينَ اللَّـهَ كَثِيرًا وَالذَّاكِرَاتِ أَعَدَّ اللَّـهُ لَهُم مَّغْفِرَةً وَأَجْرًا عَظِيمًا ﴿٣٥﴾
Na wanaomdhukuru Allaah kwa wingi wanaume na wanawake; Allaah Amewaandalia maghfirah na ujira adhimu. [Al-Ahzaab: 35].
Sasa jinsi yakutekeleza dhikr ndio muhimu na kuhusu hilo tumepata maelekezo kutoka kwa Qur-aan yanayosema:
وَاذْكُر رَّبَّكَ فِي نَفْسِكَ تَضَرُّعًا وَخِيفَةً وَدُونَ الْجَهْرِ مِنَ الْقَوْلِ بِالْغُدُوِّ وَالْآصَالِ وَلَا تَكُن مِّنَ الْغَافِلِينَ ﴿٢٠٥﴾
Na mdhukuru Rabb wako katika nafsi yako kwa unyenyekevu na kwa khofu na si kwa jahara katika kauli asubuhi na jioni; na wala usiwe miongoni mwa walioghafilika. [Al-A’raaf: 205].
Kwa minajili hiyo, dhikr za watu kukusanyikana na kukohoa hazipo katika shari’ah yetu na hiyo inakuwa haramu.
Ama mtu kukaa Msikitini au nyumbani kwake au sehemu yoyote ile na kuanza kumtaja Allaah Aliyetukuka kama alivyotufundisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni jambo zuri linalopendekezwa sana.
Na watu kupoteza wakati kwa kuwaingiza watoto wao au vijana wao kwenye vyuo kama hivyo vya kudhikiri kwa kupiga kelele na kukohoa na maneno ya ‘Huw’ ‘Huw’ au kufundishwa kupiga twari (dufu) ni mambo yasiyo na manufaa kwa Dini yao wala kuwaongezea Iymaan, isitoshe ni mambo yenye kuwapotezea wakati wao na miaka ambayo wangejifunza mambo muhimu kama Tawhiyd, ‘Aqiydah, Qur-aan, Hadiyth, Fiqh ambayo ndio mambo ya msingi Muislamu kuyafahamu na yenye kuweza kumsaidia kuongeza Iymaan yake na kumpeleka Peponi.
Kwa hiyo, ni muhimu sana wazazi na watu kuchagua vyuo vya kuaminika vya watu wa Ahlus Sunnah wal Jama’ah wenye kufundisha Uislamu kama ulivyokuwa ukifahamika na Salafus Swaalih (Wema waliotangulia; Swahaba, Tabiina na waliowafuata Tabiina).
Kwa maelezo na manufaa zaidi, bonyeza viungo vifuatavyo:
Kusoma Uradi Kwa Pamoja Kila Mwezi Kwa Kukusanyika Inafaa?
Kumuombea Du'aa Mgonjwa Kwa Mkusanyiko Inafaa?
Na Allaah Anajua zaidi