Itikadi Ziziso Sahihi Kuhusu Nyama Ya ‘Aqiyqah Mifupa Yake Na Kupikwa Kwake.
Itikadi Ziziso Sahihi Kuhusu Nyama Ya ‘Aqiyqah Mifupa Yake Na Kupikwa Kwake.
SWALI:
Asalam aleycum,
Kwanza kabla ya yote napenda kumtakia Nabiy wetu Muhammad Swala Allaahu 'alayhi wa sallam daraja ya juu. Swali langu ni kwamba je ni lazima kufukia mifupa, ngozi,na kichwa mbuzi wa hakika?
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Tunashukuru kwa Swali lako ambalo limekuwa muhimu kujibiwa kwa sababu ya itikadi za watu wengi zisizo sahihi kuhusu nyama ya ‘Aqiyqah.
Mfano wa uchinjaji na ugawaji wa nyama ya ‘Aqiyqah ni sawa na uchinjaji wa nyama ya udhw-hiyah inayotekelezwa katika ‘Iydul-Adhw-haa (Iyd ya kuchinja). Kwa maana inaweza kupikwa yote na ikaliwa yote pamoja na jamaa, jirani na marafiki au kugaiwa yote au kuigawa sehemu yake kabla ya kuipika na wala haina wakati maalumu wa kuichinja au kuipika.
Ama kuhusu itikadi zifuatazo ambazo zimekuwa maarufu katika jamii kuhusu nyama ya ‘Aqiyaqah, ni kwamba si sahihi kwa sababu hakuna dalili zake katika Shariy’ah ya Dini. Kwa hivyo itikadi hizi zinabakia kuwa ni uzushi na ni wajib kuepukana nazo. Pia itikadi zenyewe zinahusiana na elimu ya ghayb kuhusu mambo yatakayomtokea binaadamu siku za mbele. Ujuzi huo wa ghayb hakuna ajuae isipokuwa Mwenyewe Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa); kwa hiyo kuzitekeleza inakuwa ni kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), na kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni dhambi kubwa ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) haisamehe mpaka mtu arudi kutubia Kwake na ni hatari kwa kuwa mwenye kumshirikisha Allaah ameahidiwa makazi ya Moto.
Baadhi ya Itikadi zenyewe za uzushi ni zifuatazo:
- Nyama ipikwe kwa kuchanganywa na sukari au vitu vitamu au kuliwa na asali kwa madai kwamba mtoto awe na tabia nzuri.
- Mifupa ya nyama haivunjwi kwa madai mifupa ya mtoto nayo ibakie salama yaani asipatwe na ajali ya kuvunjika mifupa n.k.
- Mifupa ya nyama ifukiwe baada ya kuliwa.
Hayo ni baadhi ya madai, na huenda yakaweko zaidi ya hayo lakini yote hayana dalili, bali lililothibiti ni kuipika nyama kama kawaida inavyopikwa nyama yoyote kwa kuitia chumvi na kuliwa pasipo na masharti yoyote yale. Mas-ala mengineyo yanayohusiana na ‘Aqiyqah yameshajibiwa Alhidaaya; utaweza kupata maelezo yake katika viungo vifuatavyo:
'Aqiyqah Afanyiwayo Mtoto Mchanga
Utaratibu Wa 'Aqiyqah Katika Sunnah
Kufanya Aqiyqah Ni Lazima Au Sunnah?
‘Aqiyqah; Je, Ni Lazima Wapatikane Mbuzi Weupe Tu?
Umri anaotakiwa mtoto mchanga kunyolewa nywele
Na Allaah Anajua zaidi