Kuamkiana Kila Ijumaa Kwa Kutumiana Mashairi, Du'aa, Kupitia Barua Pepe, Text Messages .n.k.

 

Kuamkiana Kila Ijumaa Kwa Kutumiana Mashairi,

Du'aa, Kupitia Barua Pepe, Text Messages .n.k.

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Asalam aleikum

 

Tunashukuru kupata mahali pa kuuliza maswali yetu yenye utata.

 

Swali langu ni kwamba kuna mtindo siku hizi watu kusalimiana kila Ijumaa kwa kupelekeana ima text message au e-mail na kuamkiana 'Ijumaa ya Baraka' wengine hutumiana mashairi, kuombeana dua etc. wanasema inadumisha mapenzi baina ya Waislamu na pia wanaadhimisha siku ya Ijumaa. Je ni hukmu yake?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Ndugu katika Uislamu, kusalimiana ni jambo ambalo lipo katika kila jamii tena lilikuwepo kabla ya hata kuja Uislamu. Ulipokuja Uislamu haukuliondoa bali ulileta matamshi yake maalumu kwa Waislamu kusalimiana, matamshi ambayo kama yalivyothibiti katika Hadiyth ni yale yale waliyosalimiana baba yetu Aadam (‘Alayhis Salaam)  na Malaika wa Ar-Rahmaan kama yalivyothibiti katika Hadiyth:

 

 

"Allaah Amemuumba Aadam kwa sura yake urefu wake alikuwa dhiraa sitini, Alipomuumba Alimwambia: Nenda ukawasalimie kikundi kile pale miongoni mwa Malaika waliokaa na usikilize watachokuitikia nacho; kwani hayo maamkizi watayokuitikia nayo ndio maamkizi yako na ya vizazi vyako; Aadam akawaamkia kwa kusema: Assalaamu ‘Alaykum; Malaika wakamuitikia: Assalaamu ‘Alaykum wa RahmatuLlaahi, Malaika waliongeza wa-Rahmatu Llaahi…" [Imepokewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha Istiidhaan, mlango wa kuanza Salaam].

 

 

Ni vyema tuelewe kuwa dini yetu Anayoiridhia Allaah ilikamilika toka wakati wa uhai wa Mjumbe Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama inavyothibitisha Aayah iliyo wazi katika Suwrah Al-Maaidah; hivyo basi mitindo yote kama ulivyonukuu kauli yako; 'kuna mtindo siku hizi' iliyokuwa haipo wakati ule haitegemewi kuwa na faida kwa Waislamu hata wakitumia ndani yake Hadiyth au jambo lililokuwepo katika dini na lililokuwa likitekelezwa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) kama hili la 'watu kusalimiana kila Ijumaa kwa kupelekeana ima text message au e-mail na kuamkiana 'Ijumaa ya Baraka (Barakatul Jumu’ah)' au 'Jumaa Mubarak' wengine hutumiana mashairi, kuombeana dua'.

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu ‘anhum) na Salafus Swaalih na Waislamu wenye kumpenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuomba Mola Awawafikishe kushikamana na Sunnah za Mjumbe Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) huwa wanasalimia kila wakati na kila siku na si kila Ijumaa; tena husalimia kwa kila mmoja kumsikia mwenzake huku akitabasamu au akiwa na uso mkunjufu.

 

 

Waislamu wenye kumpenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) humuomba Rabb Awawafikishe kushikamana na Sunnah za Mjumbe Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na katika kujaribu kwao kutekeleza na kushikamana na maaamrisho ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) huwa wanasalimiana kama alivyokuwa alikisalimiana Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu ‘anhum) kwa kusema 'Assalaamu 'Alaykum' na hakuna katika yaliyothibiti kuwa siku ya Ijumaa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu ‘anhum) ambao kwa kweli walikuwa wakiilewa vyema siku ya Ijumaa au hata Salafus Swaalih kwamba walikuwa wakisalimiana na kuamkiana kwa kusema: 'Ijumaa Kariym' au 'Ijumaa ya Baraka' (Jumu'ah Mubaarakah). Kwa hiyo haya mambo ambayo hivi sasa yanaenea kwa kasi kwenye barua pepe, text msgs za simu za mkononi n.k. ni mambo yanayopelekea kwenye uzushi na kupotosha mafundisho sahihi ya Uislam na siku za mbele vizazi vinavyokuja watakuja kuona haya ni sehemu katika Dini na mwisho itakuwa ni jambo litakaloonekana kama ni faradhi. Na tukiangalia historia ya mambo ya uzushi, tutaona yalianza kama hivi.

 

 

Waarabu walikuwa wakisifika sana kuwa ni mabingwa katika fani ya mashairi na Qur-aan katika baadhi ya Surah zake imekuja kama shairi kwa kumalizika kila Aayah kwa namna moja kama yanavyomalizika mashairi na ilikuwa katika kawaida yao kushindana kwa kuleta shairi na yalieleweka yale yaliyokuwa mazuri na bora katika hayo kwa jina la Mu’alaaqaat kumi ambayo ilitundikwa katika A-Kaabah. Ulipokuja Uislamu pia Swahaba  (Radhwiya Allaahu ‘anhum) walitumia njia hiyo hiyo ya mashairi kuwalingania watu lakini hakuna katika yote yaliyopokewa kuwa yalikuwa yakitumiwa makhsusi kwa siku ya Ijumaa kama hivi ‘wengine hutumiana mashairi’ wala haikupokewa kuwa mshairi wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Hassaan bin Thaabit (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akitunga mashairi na kumsalimia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) siku ya Ijumaa; bali alikuwa alitunga mashairi kushajiisha watu kupigania dini ya Allaah na kuinusuru sio kusalimiana.

 

 

Du'aa ni katika ‘Ibaadah kubwa ambayo alishikamana nayo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu ‘anhum) na Salafus Swaalih na mpaka leo Waislamu wenye kumpenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) huwa du'aa ndio silaha yao kubwa kila siku na kila wakati na huwa wanajitahidi kuomba katika nyakati ambazo kumethibiti uzuri wa kuomba du’aa katika nyakati hizo ambazo zimethibiti katika Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama siku ya Ijumaa na kadhalika.

 

 

Kuhusu 'kuombeana dua n.k.' ni kwamba du'aa nzuri kumuombea Muislamu mwenzako kama ilivyothibiti katika Sunnah ni kumuombea bila ya yeye kuelewa kama unamuombea; kumuombea katika hali ya siri; hivyo kumpelekea du'aa kama hivi huwa mtu kisha kwenda kinyume na ushauri wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na pia huenda ikawa kuna aina fulani ya kujionyesha; kuwa unamuombea du'aa, hivvo kuna hatari fulani, hivyo basi la kufanya ni kuombeana du'aa kwa siri bila ya muombaji kumueleza au kumpa ishara yoyote kwa yule anayemuombea ishara itayompelekea kuelewa kuwa kuna anayemuombea du'aa; kinachotakiwa ni ikhlaasw; na ikhlaasw haihitaji hilo la kupelekea text wala shairi kwani mapenzi baina ya Waislamu hayahitaji mashairi wala tenzi.

 

 

Watu wana haki ya kusema wakitakacho na wote wanachokisema kinaweza kurejeshewa wenyewe lakini katika Uislamu, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema huwa akisemacho ni amri, hivyo Waislamu hutakiwa washikamane nacho na hawana khiari wakipenda wasipende; vinginevyo huwa imani zao hazijakamilika. Sasa basi kama kuna miongoni mwa wenye kudai kuwa wanampenda Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumfuata kwa kuwa wanasema hizo ‘Ijumaa ya Baraka ‘barakatul Jum’ah’ zao 'wanasema inadumisha mapenzi baina ya Waislamu' waelewe kuwa alichosema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye hasemi kwa matamanio yake kuwa kinadumisha mapenzi baina yetu ni hiki na si chengine:

 

"Naapa kwa Yule ambae nafsi yangu iko Mikononi Mwake, hamtoingia peponi mpaka muamini na hamtoamini mpaka mpendane, Je nikuelezeni kuhusu jambo mkilifanya mtapendana?!: Toleaneni Salaam baina yenu" [Imepokewa na At-Tirmidhiy, kitabu cha Istiidhaan kutoka kwa Mjumbe wa Allaah, mlango "Yaliyokuja kuhusiana na kutoa Salaam"  At-Tirmidhiy amesema :Hadiyth hii ni Hasan Swahiyh].

 

 

Siku ya Ijumaa ni siku tukufu kama ilivyothibiti katika Hadiyth nyingi na utukufu wake umeipata kutoka kwa Mola si kwa mwengine; na kusema kwako kuwa 'pia wanaadhimisha siku ya Ijumaa'. Tufahamu kuadhimisha jambo lolote lile katika Uislamu lazima liwe na asili kama Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au Makhalifa wake waongofu au Swahaba zake waliadhimisha jambo hilo; na katika yaliyopokewa kuhusiana na siku hii kama tutayapa jina kuwa ni maadhimisho ya siku ya Ijumaa ni kama haya:

 

  1. Kukoga siku ya Ijumaa ni wajibu kwa kila aliye baleghe

 

  1. Kujitia manukato (mwanaume)

 

  1. Kwenda Msikitini mapema; mwenye kwenda saa za mwanzo huwa kama aliyetoa Sadaqah ya ngamia na mwenye kwenda saa za mwisho ni kama aliyetoa yai na kadhalika.

 

Bonyeza kiungo kifuatacho upate maelezo zaidi:

 

 

Mambo Ya Kufanya Siku Ya Ijumaa

 

Kwa hiyo kama tunataka kuadhimisha Ijumaa basi hayo ndio baadhi ya maadhimisho ya kuadhimishwa na si vyenginevyo.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share