Uzushi Wa Kitabu Cha Aayatul-Kifaayaah
Uzushi Wa Kitabu Cha Aayatul-Kifaayaah
SWALI:
Nimenunua kijitabu kina dua Za ayatul kifaayat, na kuna taratibu za kuisoma ukitaka kumuomba mtume usome mara 3, kama kuna shida ya kuondoa nuksi unasoma mara 99, kumuomba Allah akusaidie kupata kazi ni mara 111 kwa siku 41na mengineyo, hichi kijitabu ni cha kweli, na kama sio, dua zipi zitanisaidia kama nna shida mbalimbali kuomba kwa Allah kupitia hizo dua
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Kitabu hicho ulichokitaja cha “Ayatul-Kifaaayat” hatukitambui. Juu ya hivyo, kwa jinsi ulivyoelezea kinavyodai kusomwa kwake hizo adhkaar na du’aa, ni dhahiri kabisa kwamba hayo ni mambo ya uzushi yasiyokuwa na dalili yoyote katika Shariy’ah.
Ni muhimu Waislamu watambue kwamba ‘ibaadah yoyote ile lazima ipatikane dalili zake kutoka katika Qur-aan na Sunnah. Ikiwa hakuna dalili basi haijuzu kabisa kutekeleza, bali huwa ni dhambi kwa sababu bid’ah (uzushi) ni dhambi miongoni mwa dhambi kubwa. Hadiyth zifuatayo za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni dalili miongoni mwa dalili tele nyinginezo:
عَنْ جَابِرِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ قَالَ: كَانَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ فِي خُطْبَتِهِ يَحْمَدُ اللَّهَ، وَيُثْنِي عَلَيْهِ بِمَا هُوَ أَهْلُهُ، ثُمَّ يَقُولُ: مَنْ يَهْدِهِ اللَّهُ فَلَا مُضِلَّ لَهُ وَمَنْ يُضْلِلْهُ فَلَا هَادِيَ لَهُ إِنَّ أَصْدَقَ الْحَدِيثِ كِتَابُ اللَّهِ وَأَحْسَنَ الْهَدْيِ هَدْيُ مُحَمَّدٍ وَشَرُّ الْأُمُورِ مُحْدَثَاتُهَا وَكُلُّ مُحْدَثَةٍ بِدْعَةٌ وَكُلُّ بِدْعَةٍ ضَلَالَةٌ وَكُلُّ ضَلَالَةٍ فِي النَّارِ...)) مسلم، أبو داود، النسائي، ابن ماجه، أحمد، الدارمي
Kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisema katika khutbah zake: ((Yule ambaye Allaah Amemhidi, hakuna wa kumpotoa, na yule ambaye Allaah Amempotoa hakuna wa kumhidi. Hakika maneno ya kweli kabisa ni Kitabu cha Allaah, na mwongozo mbora kabisa ni wa Muhammad, na jambo la shari kabisa ni uzushi, na kila jambo jipya (katika Dini) ni bid'ah (uzushi) na kila bid'ah ni upotofu, na kila upotofu ni motoni)) [Muslim, Abuu Daawuwd, An-Naasaaiy, Ibn Maajah, Ahmad, Ad-Daarimiy]
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ عَنِ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((مَنْ كَذَبَ عَلَيَّ مُتَعَمِّدًا فَلْيَتَبَوَّأْ مَقْعَدَهُ مِنَ النَّارِ)) متفق عليه
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayeniongopea makusudi basi ajitayarishie makazi yake motoni)) [Al-Bukhaariy Na Muslim]
Vile vile Muislamu mwenye kufuata na kutekeleza ‘ibaadah zisizokuwa na Ushahidi wowote ule huwa anapoteza muda wake bure kwani hizo ‘amali hazipokelewi kamwe kwa dalili Hadiyth ya ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa):
عن عائشةَ أنّ الرَّسولَ صلى الله عليه وسلم قال: ((مَنْ عَمِلَ عَمَلاً ليسَ عليه أمرُنا هذا فهو رَدٌّ)) البخاري
((Atakayetenda kitendo kisichokuwa chetu (katika dini yetu) basi kitarudishwa)) [Al-Bukhaariy]
Vitabu vinginevyo ambavyo ni vya uzushi ni vifuatavyo, na tunakuwekea pia viungo upate faida zaidi kutambua ubaya wake.
Du’aa Ya ‘Al-Jawshan Al-Kabiyr’ (Diraya Kubwa) الجوشن الكبير
Du'aa Za Kanzul-Arsh Na Du'aa Za Masiku Ya Wiki Zimethibiti?
Du’aa Ya Kanzul-'Arsh (Ganjul-'Arsh) Ni Uzushi Wa Mashia Na Masufi
Kitabu Cha Du'aa Kiitwacho 'Ad-Du'aa Al-Mustajaab' Kimejaa Uzushi Mkubwa
27-Tawassul Za Shirki Kufru Bid’ah: Kutawassal Kwa Du'aa Kanzul-'Arsh (Ganjul-Arsh)
28-Tawassul Za Shirki Kufru Na Bid’ah: Kutawassal Kwa Du'aa Ya Al-Fawz Wal-Qabuwl
Uzushi Wa Du’aa Ya Mara Moja Katika Umri (Maisha)
Na Allaah Anajua zaidi