Kwa Nini Mashekhe Wengine Wanakubali Arubaini Na Wanashiriki Katika Kula Chakula Chake?

 

Kwa Nini Mashekhe Wengine Wanakubali Arubaini

Na Wanashiriki Katika Kula Chakula Chake

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI

 

Asalaam alaykum

 

Kwanza kabisa natanguliza shukran zangu za dhati nimejua mengi sana kupita hii site yenu pili naomba unikjibu kupitia email yangu moja kwa moja sababu nimeshauliza maswali mengi lakini sijui kama nimejibiwa au vipi? Maswali yangu kama ifiatavyo.

 

 

Nimesoma katika hii site yenu maswali na majibu na kuwa hakuna kitu kama arobaini katika uislam sasa mbona tunapofiwa baaada ya siku arobaini tunajumuika pamoja na mashekhe wakubwa kabisa tunakula mpunga na kusoma Qur-an na wao hawakemei swala hilo?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Pia tunakushukuru kufahamu kuwa umejifunza mengi kutoka ALHIDAAYA, In shaa Allaah Allaah Akuzidishie wewe elimu na sisi Atutaqabalie amali hii.

 

 

Kadhalika tunakujulisha wewe na wengine kuwa tunawajibu wengi maswali yao lakini baadhi ya anuani zao huwa hazipokei barua zetu nyinginezo hurudi kuwe zimefeli na hatujui sababu. Hivyo ni bora kama utaona swali lako halijajibiwa kwa muda mrefu, uulizie na utoe anauni nyingine ya akiba ili ujulishwe.

 

 

Tukirejea kwenye swali lako, tunataka kuweka wazi kuwa Uislamu hauendi kwa matamanio ya watu, wawe ni wakubwa au wadogo, Mashaykh au maamuma. Uislamu unakwenda kwa misingi yake ambayo ni thabiti kabisa.

 

 

Mtu akitoka katika misingi hii hata akiwa nani atakuwa amefanya makosa. Hili jambo la chakula liliwekwa kwa maslahi ya watu fulani ambao ni Mashaykh hao unaozungumzia. Kwa ukosefu wa mshahara au ajira watu wamekuwa wakitafuta njia tofauti za kuweza kujikimu kimaisha. Ama Sunnah hasa inavyotakiwa ni yale maneno aliyotuambia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuwataka majirani na wanaokwenda kwa wafiwa siku tatu za msiba ni kufanya kama alivyosema wakati wa kifo cha Swahaba Ja’afar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kutokana na maimulizi ya ‘Abdullaah bin Ja’afar: Ulipofika msiba wa Ja’afar wakati alipouawa vitani,

 

"Wafanyieni chakula watu wa Ja’afar kwani wamepata lenye kuwashughulisha". [Wamepokea

Imaam watano isipokuwa An-Nasaaiy pekee]

 

Hivyo, inatakiwa Waislamu wawe ni wenye kuwafanyia wafiwa chakula na kuwapelekea kuliko wafiwa kuwatengenezea wengine wawe ni wenye kuja kula hapo na kuzidi kuwatia dhiki.

 

 

Zaidi soma ndani hapa upate faida nyingi:

 

 

Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti

 

 

Kawaida mwenye kukemea ni yule ambaye atajua kuwa hilo ni kosa na yule ambaye haweki maslaha yake ya kidunia na tumbo mbele. Ama yule aliyezoea kulifanya na kulishiriki, basi si rahisi kulikemea, ingawa wengine pembeni huwa wanakiri na kusema: “Unajua twende na watu watakavyo, au jamii ilivyozoea, tukipinga yaliyozoeleka tutakosa uluwa na hatutakubalika wala kusikilizwa”!!

 

 

Kwa hiyo jambo hilo la kisomo cha  Arubaini na kufanyiwa chakula halimo katika sheria na halipasi kutendwa kwani ni bid’ah iliyokemewa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na akatuhidhirishia madhara yake kuwa ni upotovu na  adhabu zake ni kujitayarishia makazi motoni.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share