Du’aa Ya ‘Al-Jawshan Al-Kabiyr’ (Diraya Kubwa) الجوشن الكبير

 

Du’aa Ya Uzushi: ‘Al-Jawshan Al-Kabiyr’ (Diraya Kubwa)  

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalam Alaikum w.w.

Baada ya salam nilikua nataka nijuwe uhakika wa dua ya jausha kabir au (gaushan kabir). nimesikia kua ni dua kutoka kwa Allah akimpa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) kama hidaya kwake na kwa umma wake.

wasalam.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kutokufupisha maamkizi ya Kiislamu. Tafadhali bonyeza kiungo kifuatacho upate maelezo zaidi yatakayokusaidia kufahamu mas-alah hayo vema:

 

Hukmu Ya Kufupisha Kumtukuza Allaah Na Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) Na Maamkizi Ya Kiislam

 

Tukirejea kwenye swali lako, du’aa uliyoulizia ni du’aa ya uzushi inayoitwa  

الْجَوْشن الكبير

 

Duaa hiyo imejaa uongo, inatoka katika vitabu vya Mashia.  Imesimuliwa katika vitabu vyao kwa isnadi iliyotungwa ya kubuniwa ya uongo. Miongoni mwa hivyo vitabu vya Mashia vyenye du’aa hiyo ni kile kiitwacho ‘Mafaatiyhul Jinaan.

 

Tunawanasihi Waislam wajiepushe sana na kitabu kama hicho kilichojaa du'aa za uzushi na ushirikina.

 

Na katika mambo Mashia wanayoyafanya wanaposoma du’aa hiyo ni kuweka Misahafu vichwani mwao wanapofika maeneo fulani kwenye du’aa hiyo! Huo ni wazimu na ujinga uliovuka mipaka mwengine wa Mashia ambao hakika dini yao imejaa vituko utakaposoma vitabu vyao na itikadi zao.

 

Anasema Shaykh al-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah):

 

“Huwezi kukuta mongoni mwa makundi yanayodai ni katika watu wa Qiblah (Waislam) walio na ujahili mkubwa kuliko Mashia (Raafidhwah), na hakuna waipendao dunia kama wao, na nimewatafiti na kuona kuwa aibu na kasoro zote wanazowasingizia nazo Maswahaba, basi wao ndio waliojawa nazo kuliko kiumbe chochote, na Maswahaba wametakasika kabisa na hayo. Hakuna shaka yoyote ile kuwa hakuna watu waongo kupita kiasi kama wao (Mashia). Ni kama yule Musaylamah al-Kadh-dhaab ambaye alidai: “Mimi ni Rasuli  mkweli, na Muhammad ni muongo!” Ndio ni kama Mashia wanaojisifu na kujitukuza kwa imani na wakiwatuhumu Maswahaba kuwa ni wanafiki, bali wao Mashia ndio katika kundi lenye unafiki mkubwa kuliko makundi yote. Na hakika Maswahaba ndio viumbe vyenye Iymaan kubwa kabisa.” [Minhaajus Sunnah An-Nabawiyyah, mj. 2, uk. 87]

 

Wanadai Mashia ndani ya du’aa hiyo kwamba:

 

“Jibriyl alimshukia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa katika moja ya ghazwa (vita vya Dini) akiwa na Jawshan (diraaya - vazi la kiaskari kama kizibao cha ngozi ngumu au chuma) akasema: “Ee Muhammad, Rabb wako Anakupa salaam, ana Anakwambia vua hilo al-Jawshan, na soma du’aa hii, kwani hiyo ni amani kwako na umma wako.”

 

Na wanadai pia:

 

“Atakayeiandika katika kafani yake, Allaah Atastahi kumuadhibu na moto.”  

 

Na “Atakayeiomba kwa niyah safi mwanzo wa mwezi wa Ramadhwaan, Allaah Atamruzuku usiku wa Laylatul-Qadr, na Atamuumbia Malaika elfu sabiini wanamsabihi Allaah, na wanamtukuza, na Atajaalia thawabu zao kwake. Na atakayeomba katika mwezi wa Ramadhwaan mara tatu, Allaah Ataharamisha mwili wake kutokana na moto, na atawajibikiwa Jannah, na Allaah Atamwakilishia Malaika wawili wamhifadhi na maasi, na atakuwa katika amani ya Allaah uhai wake wote.”

 

Pia wanadai Mashia ndani ya du’aa hiyo:

 

“Al-Husayn amesema: ameniusia baba yangu ‘Aliy bin Abiy Twaalib kuhifadhi du’aa hii, na kuitukuza, na kuiandika katika kafani yake, na niwafunze ahli yangu, na niwahimize nayo, nayo ni majina elfu na humo mna jina tukufu kabisa.”

 

Pia wanadai:

 

“Yeyote atakayeisoma na kuibeba (kuifanyia hirizi) anapotoka nyumbani kwake wakati wa Swalzah ya Alfajiri au Swalaah ya ‘Ishaa, itakuwa kama amefanya vitendo vikubwa vyema na kama kwamba amesoma Tawraat na Injiyl na Zabusr na Qur-aan.”

 

Haya yamezidi uongo kwani hakuna kilicho sawa na vitabu vya Allaah! 

 

Wanadai pia:

 

“Allaah Atampa kwa kila herufi asomayo wake wawili wa Huwrul-‘ayn (wanawake wazuri Wa Jannah wenye macho mazuri) na Atamjengea qasri Peponi na Allaah Atampa thawabu kama hizo za Manabii wanne; Ibraahiym, Muwsa, ‘Iysaa na Muhammad.”.

Huu ni uongo wa dhahiri kwani thawabu za Manabii hazipati yeyote ila wenyewe! 

 

Wanadai pia:

 

“Allaah Atampa thawabu sawa na jini dume na jike miongoni mwa majini walioamini tokea siku Aliyowaumba hadi siku ya kufufuliwa na Allaah Atampa thawabu za mashuhadaa 900,000.”

 

Wanadai pia: 

 

 “Du’aa hii ina manufaa kupata mapenzi na kufaulu, na kuondosha fundo za ndimi, na kukabiliana na mahakimu, maamiri na wafalme na kuepushilia mbali silaha zote za vyuma na  risasi na kukidhia haja n.k.”

 

Dhahiri kwamba du’aa hiyo  imejaa kauli za uongo za kila aina, na fadhila za ajabu, na maelezo marefu! Na hili si jambo la kawaida katika du’aa za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwani aghlabu du’aa zake ni fupi zenye mkusanyiko wa maneno yaliyokamilika maana kama alivyosimulia Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa):

  "كَانَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وسلم) يَسْتَحِبُّ الْجَوَامِعَ مِنَ الدُّعَاءِ، وَيَدَعُ ما سِوَى ذَلِكَ"

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akistahabu du’aa za ujumla na akiacha zisizokuwa kama hizo.” [Abu Daawuwd na Ameipa daraja ya Swahiyh Shaykh Al-Albaaniy]

 

Kauli yake, “akistahabu du’aa za ujumla.”, ina maana ambazo zinajumuisha malengo mema na makusudio sahihi au zinajumuisha thanaa kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na adabu za mas-alah. Na kauli yake “akiacha zisizokuwa kama hizo”, amekusudia du’aa ndefu na ambazo hazijumuishi malengo sahihi” [Sharh Sunan Abi Daawuwd (5/397-398) na katika ‘Awnul-Ma’buwd (4/249)]

 

Za ujumla ina maana kheri za dunia na Aakhirah na hiyo kwa lafdhi ya uchache. Na maana yake kwa wingi, kama kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

رَبَّنَا آتِنَا فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الْآخِرَةِ حَسَنَةً وَقِنَا عَذَابَ النَّارِ

Rabb wetu Tupe katika dunia mazuri na katika Aakhirah mazuri na Tukinge na adhabu ya moto. [Al-Baqarah: 201]

 

Hivyo, Waislam wanapaswa wajiepushe kabisa na du’aa hii na zingine kama ile ndefu sana ya taklifa na usumbufu inayoitwa ‘Du’aa Kumayl’ kutoka kwa Maraafidhwah wanaotaka kutoa watu kutoka katika Kitabu na Sunnah na kuwaingiza Waislam kwenye ushirikina wao na dini yao ya kutungwa ya kulinda maslahi yao ya kidunia.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share