Mtoto Mchanga Anapenda Muziki, Je, Aendelee Kumsikilizisha?

SWALI:

 

A. ALEYKUM. kwanza kabisa nawashukuru sana kwa kutuongoza katika mambo mbalimbali ya ndini ya kiislam, MWENYEZI MUNGU, awajaliie na mtuvumilie maswali yetu.

swali la kwanza ni nina mtoto wangu ana miezi10, anpenda saana mziki. nafahamu mziki ni haram; saa nyengine kama analia nami nina kazi zangu namuekea mziki ananyamaza. sasa ninakuwa nafanya madhambi? Kwa sababu inanibidi kumwekea mziki nifanye shuhuli zangu. naomba jawabu swala hili linanitatiza saana.

 


JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika  Salaam hazifai kufupishwa kwa kuandikwa (A.A) au (A.A.W.W.) au kama ulivyoandika kwani haijafundishwa hivyo na pia ni kujikosesha fadhila za Salaam kama tulivyoelezwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo nayo tujizoeshe kuandika (Assalaamu ‘alaykum) au (Assalaamu ‘alaykum wa rahmatullaah) au (Assalaamu ‘alaykum wa Rahmatullaah wa Barakaatuh) kwa ukamilifu na tutakuwa tumeiga mafunzo ya Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na pia tutakuwa tumezoa thawabu zote za Salaam kama tulivyofundishwa. Na Mafunzo yote na fadhila zake zimo Alhidaaya katika kiungo kifuatacho: Maamkizi Ya Kiislamu.  

 

Shukran kwa swali lako kuhusu muziki. AlhamduliLlaah kuwa umefahamu kuwa muziki ni haramu kwa Muislamu. Kawaida mtoto ni kiumbe ambaye anashika haraka mambo tofauti. Hivyo, ukimzowesha mema atayazoea na vile vile ukimzoesha mabaya basi atayashika.

 

 Muziki una athari kubwa sana. Ili kutomfanya mtoto wako kutoingia katika dimbwi ambalo baadaye litamwia ugumu kutoka atakapokuwa mkubwa ni afadhali umzoeshe kitu kingine kama vile kusikiliza Qur-aan na ukiona bado hatulii, basi endelea kumwekea hadi atazoea, na ikishindikana basi mwekee Nashiyd, ambayo ni mashairi kwa maadili ya Kiislamu bila magoma, ala za muziki na vitu kama hivyo viliyokatazwa.

 

Muondolee tatizo hilo kuanzia umri huo wake ulio mdogo.

 

Pia soma mada ifuatayo ambayo inaelezea uharamu wa muziki ili uzidi kukinaika na madhara yake:

 

Hukmu Ya Muziki Katika Qur-aan Na Sunnah - Ewe Upendaye Nyimbo Na Muziki, Haujafika Wakati Wa Kuogopa Adhabu Kali Za Allaah?

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share