Kusoma Majina Ya Allaah Kwa Idadi Maalum
Kusoma Majina Ya Allaah Kwa Idadi Maalum
SWALI:
Nimeona kitabu kimeandikwa majina ya Allaah na maana yake kwa kiswahili, na baadhi ya majina yameelezwa kwamba kama ukiyataja mara kadhaa 70 au 100-nk, basi unaweza kupata jambo fulani, jee nikweli mambo haya?
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Vitabu kama hivyo vipo vingi vinavyoelezea mambo haya ya kutaja majina ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa idadi maalumu nawe utapata thawabu kadhaa. Kwa hakika ukiangalia vitabu hivyo hutapata kukuta maelezo hayo ni Hadiyth na ikiwa imesemekana kuwa ni Hadiyth basi aghalu za ni Hadiyth zisizotegemewa. Kumkumbuka Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kutumia Majina Yake au aina yoyote ya Tasbiyh kwa kutaja idadi ma'aluum bila kuweko dalili katika Qur-aa au Sunnah ni jambo la uzushi (Bid'ah) na linapaswa kuachwa kwani mtu atahangaika bure na kitendo hakitokubaliwa kutokana na dalili za Hadiyth nyingine kuhusu mambo ya Bid'ah, mojawapo wapo ni hii:
((من عمل عملا ليس عليه أمرنا فهو رد ((خرجه مسلم في صحيحه
"Atakayefanya kitendo kisichokuwa katika amri yetu basi kitarudishwa (hakitokubaliwa)" [Imesimuliwa na Muslim]
Jambo ambalo lipo wazi kuhusu majina ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni kama inavyotueleza Qur-aan kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ana majina mazuri hivyo tumuombe kupitia majina hayo yake. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا ۖ
Na Allaah Ana Majina Mazuri kabisa, basi muombeni kwayo. [Al-A'araaf: 180]
Na Amesema tena:
قُلِ ادْعُوا اللَّـهَ أَوِ ادْعُوا الرَّحْمَـٰنَ ۖ أَيًّا مَّا تَدْعُوا فَلَهُ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ ۚ
Sema; Muiteni Allaah au muiteni Ar-Rahmaan, vyovyote mtakavyomwita basi Yeye Ana Majina Mazuri kabisa. [Israa: 110]
Kwa hiyo unaweza kuomba mfano unataka Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akughufurie dhambi zako, ukamwita kwa Jina Lake Tukufu 'Yaa Ghaffaaru' au 'Ya 'Afuwwu' kama mfano unataka Akuruzuku kitu ukamwita 'Ya Razzaaq' au mfano unamuomba kitu na unataka Akutakabalie dua yako, ukamwita 'Ya Sami'u', 'Ya Qariybu', 'Ya Mujiybu' na kadhalika. Hivi unaweza kumwita kwa mara unazotaka bila ya kuweka idadi ma'aluum.
Katika vitu vyenye idadi maalumu ni dhikri (kumtaja Allah) kwa kusema: Subhanallah, Alhamdullillah, Allahu Akbar na adhkari nyingine za baada ya Swalaah, au za mchana na usiku. Tazama Kitabu cha
Hiswnul-Muslim: Du’aa Na Adhkaar Kusoma Na Kwa Kusikiliza (Toleo Lilohaririwa)
kilichokuweko Alhidaaya humo utapata dalili ya Tasbiyh na Adhkaara ambazo zimetajwa idadi ma'aluum kuzisoma.
Kiungo kifuatacho kumetajwa idadi maaulumu zilizothibiti.
Fadhila za Tasbiih, Tahmiid, Tahliil, na Takbii
Na Allaah Anajua zaidi