Zingatio: Ndio Asili Yetu

 

Zingatio:  Ndio Asili Yetu

 

Naaswir Haamid 

 

Alhidaaya.com

 

 

Ndani ya tumbo la mama ndimo tuliishi kwa muda wa miezi tisa. Hatukuelewa namna ya kupiga tonge wala anachoelewa mama kinachomfikia mwanawe tumboni. Jicho lilifumbwa kuiangalia dunia na katu hatukushuhudia polisi kutulinda wala satellite kutumurika. Mama akamtoa mwanawe tumboni kwa shida, tabu na uchungu wa hali ya juu. Humuelewi kama analia au anacheka pale anapokabidhiwa mwanawe kwa mara ya kwanza.

 

Bila ya kufunguliwa darasa wala juhudi ya ujuzi wa mama; mtoto anafyonza maziwa, siku zinapita anaanza kukaa, baadaye anatambaa. Mtoto anakuwa kwa kusimamia kiambaza kimoja kimoja huku akiinua hatua zake za mwanzo.

 

Basi ni nani mlinzi wa mtoto awapo tumboni? Na ni nani mwalimu anayemfundisha mtoto kwenda hata kupiga mbio? Sote tulipitia huko na ndio asili yetu.

 

Nashuhudia ya kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ndie Mlinzi wa kila mmoja wetu alipokuwa tumboni mwa mama yake na ndiye Mwalimu wetu Aliyetufunza kuketi, kutambaa hadi kwenda.

 

Wala hakuna penginepo tunapoweza kupata maelezo ya asili yetu kwa lengo la kupata mwongozo na maw’idhah isipokuwa Qur-aan na Sunnah ya Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Nayo Qur-aan inatuambia ya kwamba asili yetu ni udongo ulio nadhifu: 

وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن سُلَالَةٍ مِّن طِينٍ ﴿١٢﴾

Kwa yakini Tumemuumba insani kutokana na mchujo safi wa udongo. [Al-Muuminuwn: 12]

 

Ndani ya sehemu iliyohifadhiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akatuweka humo kwa kutumia tone la manii. Muujiza mkubwa ni kwamba Qur-aan inatueleza asili yetu hatua kwa hatua kana kwamba kulikuwa na vifaa vya kisasa enzi za Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Allaah Mkuu wa wakuu anatueleza asili yetu kama ifuatavyo:

 

ثُمَّ خَلَقْنَا النُّطْفَةَ عَلَقَةً فَخَلَقْنَا الْعَلَقَةَ مُضْغَةً فَخَلَقْنَا الْمُضْغَةَ عِظَامًا فَكَسَوْنَا الْعِظَامَ لَحْمًا ثُمَّ أَنشَأْنَاهُ خَلْقًا آخَرَ ۚ فَتَبَارَكَ اللَّـهُ أَحْسَنُ الْخَالِقِينَ ﴿١٤﴾ 

Kisha Tukaumba tone la manii kuwa pande la damu linaloning’inia, Tukaumba pande la damu hilo linaloning’inia kuwa kinofu cha nyama, Tukaumba kinofu hicho cha nyama kuwa mifupa, Tukavisha mifupa hiyo nyama, kisha Tukamuanzisha kiumbe kingine. Basi Tabaaraka-Allaah, Amebarikika Allaah Mbora wa wenye kuumba. [Al-Muuminuwn: 14]

 

AlhamduliLlaah hivi sasa twapumua pumzi Alizoturuzukia Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), lakini tuelewe kuwa wakati wowote mauti yatatufika na Siku ya Qiyaamah tutafufuliwa.

 

Tamba mashriq wal-maghrib, mwishowe tambua kwamba asili yetu ni hali iliyo dhaifu na tutamalizia kwa kifo kisichojulikana muda wake. Na iweje kwa udhaifu wa asili hii, tukawa ni wenye kusahau hadi tukazidhulumu nafsi zetu.

 

Lililo salama kwa upande wetu ni kunyenyekea kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa kuutambua Ukubwa Wake Ambao Hauna mfano wa kitu chochote.

 

 

Share