Zingatio: Babu Wa Loliondo Hatufai
Zingatio: Bado Mali Haijaisha….Endelea Kuitafuta!
Naaswir Haamid
Shirki ni dhambi kubwa na hii ni dhambi iliyopo orodha ya juu miongoni mwa madhambi makubwa katika Uislamu. Asili ya Vitabu vyote vya Rabb na ambavyo vyote vimekuja kuhubiri Uislamu, vinakataza dhambi ya shirki. Hivyo, yeyote atakayekuja na amali ya ushirikina hata kama ni Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au ni Malaika Jibriyl (‘Alayhi swalaatu was-salaam) basi atahesabika ni Mshirikina na hukumu yake ataikuta mbele ya Muumba.
Katika ushirikina uliotia fora hapa Afrika Mashariki ni wa yule Babu Ambilikile Masapila wa Loliondo. Huyu ni Mchungaji Mstaafu kutoka kanisa la Kiinjili anayedai kuwa na sifa sawa na za Nabiy. Miongoni mwa hizo ni kusema kwamba ameoteshwa mambo ya ghaibu kama vile kuoteshwa ndoto na Allaah, kudai kupewa uwezo wa kutibu maradhi sugu kama vile kisukari, shinikizo la damu, saratani na UKIMWI. Ni kusema kwamba wahyi bado haujakatika na unaendelea kwa Babu Loliondo.
Sio hayo tu, Babu huyu anatoza dola moja ya Kimarekani kwa mgeni wakati mwenyeji anatozwa sh. 500 tu kwa kila kikombe cha dawa yake. Mgawanyo wa fedha hizi ni kwamba sh. 200 zinapelekwa Kanisani, sh. 200 ni za watumishi wanaomsaidia kazi na sh. 100 inayobaki ni ya kwake yeye Babu. Haya ni mapato yaliyofikia takriban sh. milioni 50 hadi tarehe 4/04/2011 na fedha hizi zinasimamiwa na kukusanywa chini ya uangalizi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT). Kama kweli yeye anatibu kwa mujibu wa huyo Yesu anayemfuata, basi hakupatapo Yesu kutoza hata shilingi moja kwa matibabu yake.
Cha maajabu zaidi, ni kwa idadi ya watu waliovutiwa na waliorogwa akili kwenda kupata matibabu kwa Babu huyu. Bila ya kujali dini wala imani zao, umbali wa masafa, gharama, ushirikina, misukosuko na taabu ya safari; makundi kwa makundi ya watu wanaendelea kumiminika kwenda kupata hicho kikombe. Kutokana na msongamano huo na maradhi kuwazidi wagonjwa; kuanzia tarehe 11/03/2011 hadi kufikia tarehe 29/03/2011 jumla ya watu wapatao 74 wameripotiwa kupoteza maisha. Ni vyema kuelewa kwamba maiti hawa ni mjumuiko wa kinamama, kinababa, watoto, wasio Waislamu na halikadhalika Waislamu. Wengine wamekufia hapo hapo na kuzikwa huko huko. Je, hivi ndivyo Yesu alivyokuwa akitoa dawa zake na kuwatibu waumini wake?
Kuhusiana na dhambi ya ushirikina, Allaah Anasema ndani ya Qur-aan:
إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدِ افْتَرَىٰ إِثْمًا عَظِيمًا ﴿٤٨﴾
Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amezua dhambi kuu. [An-Nisaa: 48]
Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ
Mwenye kumshirikisha Allaah bila shaka Allaah Atamharamishia Jannah, na makazi yake yatakuwa ni motoni. [Al-Maaidah: 72]
Halikadhalika, kuna makemeo makali juu ya Muislamu kwenda kwa mganga kama huyu Babu wa Loliondo, na ambaye ataenda kwa mganga basi huyo amekufuru. Hii inathibitishwa ndani ya Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inayosema: “Atakayemwendea mchawi na kuamini aliyoambiwa, basi amekufuru yale aliyoteremshiwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)”. [Imepokewa na Abu Daawud]
Kwa lengo la kuzilinda imani zetu na hadhi ya Uislamu wetu, tunawanasihi wale ndugu zetu Waislamu kuacha mara moja kushiriki kwenda kwa huyu Mshirikina Babu wa Loliondo.
Rabb Atuongoze njia iliyonyooka na Atuepushe kutumbukia kwenye dhambi kubwa haswa ya shirki pamoja na kutuepusha kuwa miongoni mwa wasajiliwa wa Moto wa Jahannam Siku ya Qiyaamah