Zingatio: Dini Mseto
Zingatio: Dini Mseto
Naaswir Haamid
Rusuli ishirini na tano ambao wametajwa katika Qur-aan, Aliowaleta Rabb wetu Mtukufu, wote walikuwa na muongozo mmoja tu, nao ni kuusimamisha Uislamu kwa haki inayostahiki kusimamishwa. Nako ni kujikubalisha kwa amri za Rabb pamoja na kushuhudia kwamba hakuna Rabb Apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah na wala Hana mshirika.
Taariykh ya Uislamu haikupatapo hata siku moja kuandika kwamba Rusuli hawa walishirikiana na makafiri katika ibada. Wala hakuna uthibitisho wa kuonesha kuwepo muingiliano wa elimu baina ya misingi ya Uislamu na ukafiri. Hizo ni njia mbili tofauti, wala hazitakuwa na mfanano wowote hadi mwisho wa dunia hii.
Basi kwa wale wanaosema kwamba Uislamu upo sawa na dini nyengine, haswa zile zinazosemwa kuwa ni dini za Kitabu, kama vile Uyahudi na Unaswara, hao wamekwenda kombo na wala hawaelewi misingi ya Uislamu. Kwani hata huo Uyahudi na Unaswara unaofuatwa leo, hauna uhusiano sahihi na hivyo Vitabu Alivyovishusha Rabb wetu (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Sasa ni wapi tena tunataka kuwabebesha watoto wetu elimu ya Yesu aliyevumbuliwa na Ukiristo hali ya kuwa Uislamu unayo mafundisho yake sahihi ya Nabiy ‘Iysa bin Maryam (‘Alayhis-salaam)?
Rabb Wetu(Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amesema:
إِنَّ الدِّينَ عِندَ اللَّـهِ الْإِسْلَامُ ۗ وَمَا اخْتَلَفَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ إِلَّا مِن بَعْدِ مَا جَاءَهُمُ الْعِلْمُ
Hakika Dini mbele ya Allaah ni Uislamu. Na hawakukhitilafiana wale waliopewa Kitabu ila baada ya kuwajia elimu.. [Al-‘Imraan: 19]
Na Akasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) pia:
وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ ﴿٨٥﴾
Na yeyote anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu basi haitokubaliwa kwake; naye katika Aakhirah atakuwa miongoni mwa waliokhasirika. [Al-‘Imraan: 85]
Kwa hivyo, tuelewe Waislamu kwamba, iwapo tumeukubali Uislamu kuwa ni Diyn yetu, basi hayo hapo juu ndio mafunzo sahihi, wala Rabb wetu hajatutaka tuchanganye imani zetu zilizo safi dhidi ya imani za kikafiri. Na kwa hakika Uislamu wetu unatufunza kutochanganya ukafiri na Uislamu:
قُلْ يَا أَيُّهَا الْكَافِرُونَ ﴿١﴾ لَا أَعْبُدُ مَا تَعْبُدُونَ ﴿٢﴾ وَلَا أَنتُمْ عَابِدُونَ مَا أَعْبُدُ ﴿٣﴾ وَلَا أَنَا عَابِدٌ مَّا عَبَدتُّمْ ﴿٤﴾ وَلَا أَنتُمْ عَابِدُونَ مَا أَعْبُدُ ﴿٥﴾ لَكُمْ دِينُكُمْ وَلِيَ دِينِ ﴿٦﴾
Sema: “Enyi makafiri! Siabudu mnayoyaabudu. Na wala nyinyi si wenye kuabudu Ninayemuabudu. Na wala mimi si mwenye kuabudu yale mnayoabudu. Wala nyinyi hamutaabudu ninayemuabudu. Na wala mimi si mwenye kuabudu Yale Ninayemwabudu. Nyinyi mna dini yenu; nami nina Dini yangu. [Al-Kaafiruwn: 1-6]
Yapo mambo ambayo kweli tunaweza kushirikiana na makafiri, kama vile elimu sahihi za dunia kwa mfano utabibu na ufundi; lakini abadan sio ndani ya misingi ya Kiislamu hadi kufikia binti wa Kiislamu kutoona tofauti baina ya kuvaa ama kutovaa hijaab.
Tumche Rabb wetu (Subhaanahu wa Ta’aalaa), na tumuabudu Yeye kama Alivyotuamuru bila ya kumshirikisha. Tunamuomba Rabb wetu Atuongoze katika njia sahihi na Atukhitimishe kwa qawli ya haki iliyothibiti.