Mke Kazini Kisiri Kisha Mume Kamsamehe, Ni Makosa?

SWALI:

Halafu ninaswali: tumeambiwa binadamu asokuwa na wivu ni kama nguruwe na ataingiya motoni. Mkee alikuwa akiishi Afrika na mume ulaya wameishi mbalimbali kwa miaka mitatu ikatokea mke amezini halafu kaja kwa mume wake akamuambiya kwamba kipindi kile hawakuwa pamoja ilimtokea kuzini mume akaamuwa amemsamehe (tume ambiwa binadamu asokuwa na wivu nikama nguruwe na ataingiya motoni sasa vipi hapo)? Mtu mke wake kaziniwa kisiri halafu kaomba msamaha kwa mumewe kuapa kuto kurudia akasamehewa sasa vipi kuna makosa? Je, inajuzu?


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kusamehe makosa ya mwenzio. Mwanzo tunataka kurekebisha msemo ulioutaja kuwa asiokuwa na wivu ni kama nguruwe na ataingia motoni si Hadiyth bali huenda ukawa ni msemo wa Kiswahili unaotumiwa na Waswahili. Hata hivyo, tufahamu kuwa hayaa ni katika Imani na hayaa inaelezwa katika machimbuko ya kisheria.

Hakika alilolifanya huyo mwanamke ni jambo chafu na ovu na khiyana ya hali ya juu kabisa. Na si rahisi kwa mtu mwenye ghera kuweza kuendelea kuishi na mtu wa namna hiyo. Lakini pia tufahamu kuwa Uislamu umeweka milango ya toba wazi na kila dhambi linaweza kutubiwa maadam haijafika ile hali ambayo toba haikubaliki tena.

Wanazuoni wanatuambia kuwa toba inatakiwa kwa kila dhambi ambalo mwanaadamu atafanya. Na ili kutubia kwa Allaah Aliyetukuka ni lazima utimize masharti yaliyowekwa, na kwa kuwa swali lako linaingia haki ya binaadamu ndani yake kukubaliwa toba yako ina masharti manne:

i)                   Kujivua na maasiya (kujiondoa katika madhambi).

ii)                  Kujuta kwa kufanya dhambi.

iii)                Kuazimia kutorudia tena dhambi hilo.

iv)               Kutaka msamaha kutoka kwa aliyemdhulumu (Imaam Abi Zakariya

Yahyaa bin Sharaf an-Nawawiy, Riyaadh asw-Swaalihiyn, uk. 41 – 42).

Kulingana na swali lako ni kuwa mke huyo ametekeleza yote hata lile sharti gumu la kuonana na mumewe ana kwa ana na kumueleza alilofanya na kuwa hatafanya tena. Kwa kuwa mume mwenyewe amemridhia na kumuamini huwa makosa yake (mke) yamesamehewa. Hiyo ni kuwa aliyefanyiwa ameridhia na kinyongo kishamtoka.

Kukosa ni ubinaadamu na mbora wa anayekosa ni yule mwenye kutubia na kujirekebisha. Tazama jinsi gani Ma’iz na yule mwanamke wa al-Ghaamidiyah walivyojileta kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili kutakaswa kwa kosa lao la kuzini kwa sababu ya kuoa na kuolewa walipigwa mawe hadi kufa. Kwa hukumu hiyo kutekelezwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema kuwa wametubu kiasi ambacho lau toba yao itagawiwa watu wa Madiynah ingewafunika wote

Tunawaombea kheri baada ya mume kumsamehe mkewe kwa kosa kubwa alilolifanya. Na ni juu ya mke akachukulia ihsani hiyo kwa kutorudia tena daima kosa hilo. Zinaa hasa ikiwa mwanamke ameolewa au mume ameoa ni dhambi kubwa lenye kustahiki adhabu iliyowekwa na sheria. Pia ni juu ya mume isiwe ndio adhaa kutoka kwake kwa sababu ya kumsamehe huko. Awe kweli amesamehe na asiwe ni mwenye kumkumbusha ihsani hiyo mkewe wakati wamegombana.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share