Amezaa Na Asiye Muislamu Nini Hukmu Yake

SWALI:

 

ASALLAM ALLAIKUM,

Swali langu ni, JE INAKUWAJE MTU AMBAYE ALIZAA MTOTO NA MTU AMBAYE SI MUISLAMU YAANI MFANO MZUNGU, JE HUYU MTOTO UTAISHI NAE VP? INSHAALLAAH NATARAJI JIBU.

ASALLAM ALLAIKUM.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kumlea mtoto uliyezaa na Mzungu ambaye si Muislam au asiye Muislamu mwengine yeyote. Hakika isiyopingika ni kuwa ikiwa asiyekuwa Muislamu ni katika Wayahudi au Manasara, mkafunga ndoa, bila ya kufanya uzinzi wala kuwaweka kinyumba nao ni wema basi mtoto huyo atakuwa ni halali kisheria

.

Hata hivyo, ikiwa msichana Muislamu ameolewa na Myahudi au Mnasara au asiyekuwa Muislamu yeyote yule hakutakuwa na ndoa, bali hao wawili watakuwa wanazini na hivyo atakayezaliwa hatakuwa wa halali. Lakini ikiwa mwanamke ni Mzungu asiyekuwa na Dini au asiyekuwa Muislamu mwengine kama Baniyani, Budha n.k. mbali na waliopewa Kitabu basi hakutakuwa na ndoa bali hiyo itakuwa ni zinaa baina ya watu hao wawili.

 

Na ikiwa wamezaa tu kwa kukaa kinyumba, huyo mtoto hatakuwa wa huyo mwanamme kisheria. Japokuwa kibinadamu ni damu yake na anaweza kumfanyia ihsani kwa kumtazama kihali na mali. Baba huyo hatarithiwa na huyo mtoto, wala mtoto kurithiwa na baba huyo.

 

Ni juu ya Waislamu wanaume na wanawake wachunge sana mipaka ya Dini na wasiingie katika zinaa kwa hali yoyote ile. Ikiwa tumeshindwa kujizuia na kutozini basi tufanye bidii tuoe au tuolewe ili kujikinga na maafa ya zinaa. Na ikiwa hatujapata kuoa au kuolewa basi tufunge Swawm ili tujizuie kuingia katika mtego huo mbaya katika maisha yetu.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share