Mzazi Wangu Aliyenilea Kausia Nisiolewe Na Yeyote Ila Kabila Fulani Nami Nimeposwa Na Mtu Mwengine

SWALI:

 

 

Asalam Alaikum Warahamatullahi Wabarakat mie ni binti wa kiislam, niliyefiwa na baba yangu tokea umri wa miaka 6, nikachukuliwa na jama akanilea kwa lillahi mpaka nilipofika umri wa miaka 30 yule mlezi wangu akafariki. Ila aliwahi kuniachia usia kuwa nisiolewe na mtu wa kabila lolote ila anayotaka yeye.

Na mie nimebahatika kupata mtu wa kabila tofauti sio lile analotaka yeye aliyefariki mlezi wangu, na ndugu zangu wote hawati kunioza kwa huyo mtu kisa sio kabila moja. Na huyo mtu anayetaka kunio ni muislam wa kweli na mwenyezmungu ndio anajua zaidi, namie nilichopenda kwake ni dini yake. Nifanye nini kwenye hilo kwa kweli umenikumbuka mtihani naweza kujioza mwenyewe?

 

 

Wahadha salam Alaikum.

 


JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu wasiya ulioachiwa na aliyefariki mlezi wako. Mwanzo tunapenda kumkumbusha kila mmoja kuwa huu ulimwengu ni sehemu ya mitihani. Kila mmoja anapata mtihani wa aina yake. Kwa hiyo, inatakiwa tufanye juhudi katika kuipita hii mitihani na huku tunaendelea kumuomba Allaah Atupe istiqaamah na misimamo katika Dini Yake.

 

 

Tufahamu kuwa wazazi wana haki juu yetu nasi tunafaa tuwatii katika wema na mambo ya sawa. Hatufai kabisa kuwatii katika maelekezo na nyasiya ambayo zinakwenda kinyume na Dini. Hii ni hali ambayo hufai kuwatii kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"Hakuna utiifu kwa kiumbe katika kumuasi Muumba".

 

 

Katika wasiya alioacha mzazi wako kuna matatizo na unakwenda kinyume na mafundisho ya Uislamu. Kwa kuwa unakwenda kinyume utakuwa hufai kuwafuata katika hilo. Allaah Aliyetukuka Anatuambia:

 

 

"Enyi watu! Kwa hakika Tumekuumbeni nyote kwa mwanamme mmoja na mwanamke mmoja. Na Tumekufanyeni mataifa na makabila mbali mbali ili mjuane. Hakika ahishimiwaye sana miongoni mwenu mbele ya Allaah ni yule amchaye Mungu zaidi katika nyinyi" (49: 13).

 

 

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuusia sana katika ndoa tutafute mwenye Dini (al-Bukhaariy na Muslim) na mwenye maadili na tabia nzuri za Kiislamu (at-Tirmidhiy). Hakuna kabisa katika machimbuko ya Kiislamu kufanya uchaguzi kwa ajili ya kabila lako au jengine.

 

 

Hivyo, ikiwa kweli umejua kwa kuuliza uliza kuwa huyo mwanamme ameshika Dini na mwenye maadili mazuri kitu ambacho unafaa ufanye ni kujaribu kuzungumza na nduguzo kwa njia nzuri na hekima uwaelezee msimamo wa Uislamu. Ikiwa hawakukusikiliza basi jaribu kutumia jamaa zako ambao wamekuelewa au mashaykh ili kuzungumza nao na kuwakinaisha katika hilo. Pia swali Swalah ya Istikhaarah umtake shauri Allaah Aliyetukuka kuhusu ndoa yenu kama ni kheri au kuna shari ndani yake.

 

 

Ikiwa ndugu zako hawakuweza kukusikiliza kitu ambacho unaweza kufanya ni kupeleka kesi yako kwa Qaadhi na ikiwa hayupo basi kwa Shaykh mwenye kuozesha. Qaadhi au Shaykh huyo baada ya kupeleka kesi yako atawaita nduguzo na kuwasikiliza pamoja nawe. Ikiwa ni mas-ala ya ukabila tu, Qaadhi au Shaykh atachukuwa ile daraja ya uwalii wa mke na kuwaozesha.

 

 

Tunakuonya na tunakunasihi sana usichukue kabisa hatua mikononi mwako kwa kutoroka na huyo mwanamme ili mwende kuzini ili mupate baada ya hapo kuozwa na nduguzo. Baki na muruwa wako na maadili yako ya Kiislamu na tuna yakini kuwa Allaah Aliyetukuka Atakufungulia kila la kheri na kukuepushia kila la shari na kukupatia mume wa kheri.

 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share