Mashairi: Siku Ya Qiyaamah
Siku Ya Qiyaamah
‘Abdallaah Bin Eifan (Rahimahu-Allaah)
Hodi mlango nabisha, salaam zangu pokeeni,
Wajibu kukaribisha, akiwasili mgeni,
Sikuja kuwafundisha, bali natoa maoni,
QIYAAMA kipo njiani, siku hiyo inatisha.
Siku hiyo inatisha, Kiyama kipo njiani,
Ni nani ataebisha, wote kimya hadharani,
Siku ya kusikitisha, na siku yenye huzuni,
QIYAAMA kipo njiani, siku hiyo inatisha.
Ndio mwanzo wa maisha, ya pepo na ya motoni,
Yote Atarekebisha, Rabuka kwenye mizani,
Ukweli kubainisha, na haki itabaini,
QIYAAMA kipo njiani, siku hiyo inatisha.
Mitume Watasimama, na wao pia foleni,
Hakuna ataesema, mpaka Aje Rahmani,
Hapo watu hutetema, ataepasi ni nani?
QIYAAMA kipo njiani, ongezeni yenu mema.
Ikipigwa baragumu, sijuwi niseme nini,
Siku hiyo siku ngumu, kwa viumbe ardhini,
Siku ya kujilaumu, majuto tupu usoni,
QIYAAMA kipo njiani, tuwe tayari kaumu.
Majabali kuvunjika, kupeperuka angani,
Ardhi kutetemeka, kuja juu yalo chini,
Bahari moto kuwaka, Ya Ilahi Ya Manani,
QIYAAMA kipo njiani, tukae tukikumbuka.
Nyota zitapukutika, hazitabaki mbinguni,
Na jua litakunjika, imesema Qur-aani,
Na mimba kuharibika, mwana kutoka tumboni,
QIYAAMA kipo njiani, na tuzidishe sadaka.
Watoto huota mvi, nywele zote za kichwani,
Na watu kama walevi, hivyo wewe utadhani,
Na kumbe sio walevi, adhabu kali jamani,
QIYAAMA kipo njiani, fanya wema sasa hivi.
Allah Atakunja mbingu, kwa Mkono ni yakini,
Watafufuliwa wafu, watoke makaburini,
Tusimame kwenye safu, bila ya nguo mwilini,
QIYAAMA kipo njiani, tushike dini tukufu.
Kila mtu nafsi nafsi, na ndugu hawajuani,
Baba na mwana ni basi, umeshakwisha ubini,
Hakuna tena nafasi, mapenzi hufa moyoni,
QIYAAMA kipo njiani, tenda mazuri upesi.
Tuwe tayari kabisa, kwa ibada na imani,
Tuanze kutoka sasa, tuiizingatie dini,
Tuache zote anasa, na michezo ya kihuni,
QIYAAMA kipo njiani, tabia piga msasa.
Hapa nimefika mwisho, kuandika natamani,
Lakini natokwa jasho, nimechoka samahani,
Tufikirie ya kesho, Kiyama sio utani,
QIYAAMA kipo njiani, Siku Hiyo Ya Vitisho.