Mashairi: Muziki, Ngoma, Haramu
Muziki, Ngoma Haramu
‘Abdallah Bin Eifan
(Jeddah, Saudi Arabia)
Salaam kwa ikhwani, Bismillaahi naanza,
Nitowe yangu maoni, nalifungua baraza,
Liende kila makani, tupate kulisambaza,
Dini imetukataza, ngoma, muziki haramu.
Ipo kwenye Qur-ani, vizuri ukichunguza,
Aya ipo tazameni, Mola Ameshatangaza, [Luqmaan: 6]
Nyimbo upuuzi yakini, Aya inatueleza,
Dini imetukataza, ngoma, muziki haramu.
Muziki ya mashetani, dini imetukataza,
Wengine yao maoni, eti inatupumbaza,
Ukweli umebaini, kumbe inatupoteza,
Dini imetukataza, ngoma, muziki haramu.
Kasema na iblisi, Mola Alipozungumza, [Al-Israa: 64]
Wachochee wafuasi, kwa sauti (ya kupendeza),
Kawafuate kwa farasi, na kwa miguu ukiweza,
Dini imetukataza, ngoma, muziki haramu.
Malaika hutoroka, muziki huwakimbiza,
Shetani hufurahika, tena hukuelekeza,
Nia yake kwa hakika, yeye kukuangamiza,
Dini imetukataza, ngoma, muziki haramu.
Anaimba kwa vizuri, tarumbeta hupuliza,
Wengine na mizumari, ona wamejitandaza,
Na ngoma zipo tayari, zinapigwa kwenye meza,
Dini imetukataza, ngoma, muziki haramu.
Na maneno ya mapenzi, vizuri hutengeneza,
Huyaimba kwa mapozi, huku akijigeuza,
Analia kwa machozi, chongo huita kengeza,
Dini imetukataza, ngoma, muziki haramu.
Disco inapovuma, ona vipi wanacheza,
Anakumbatiwa mama, dansi kutekeleza,
Nenda mbele rudi nyuma, huku akijilegeza,
Dini imetukataza, ngoma, muziki haramu.
Wengine kwenye taarabu, wapo wanasikiliza,
Eti ndio ustaarabu, “wajibu” ametimiza,
Kajipara “kiadabu,” mapambo hakupunguza,
Dini imetukataza, ngoma, muziki haramu.
Ngoma nyingi za kijadi, hakika zina matusi,
"Msondo" ni ufisadi, "sindimba" ni unajisi,
Ujahili umezidi, ni mambo ya iblisi,
Dini imetukataza, ngoma, muziki haramu.
Na ngoma za "lelemama", kutembea mitaani,
Zilishamiri Dodoma, zama zetu za shuleni,
Nadhani wameshakoma, Wasamehe Muhisani,
Dini imetukataza, ngoma, muziki haramu.
Mwanamwali akinema, anabebwa mgongoni,
Na huku akina mama, "chereko" wanaighani,
Wote wanamtazama, yupo wazi kifuani!!!
Dini imetukataza, ngoma, muziki haramu.
Chakacha kule Mombasa, ni mchezo wa zamani,
Sijuwi kwa hivi sasa, kama ipo majumbani,
Mirungi kwao "anasa," na vibiri midomoni,
Dini imetukataza, ngoma, muziki haramu.
Tumemsahau Mola, na dini tumeipuza,
Ameshatutia pingu, shetani ametuweza,
Watu wenye vichwa ngumu, hawataki kunyamaza,
Dini imetukataza, ngoma, muziki haramu.
Maghfira kwa Mkwasi, sote tunabembeleza,
Tunamuomba halisi, dua tumeziongeza,
Tuepushwe na maasi, Mola Atatuongoza,
Dini imetukataza, ngoma, muziki haramu.
Kamba ya Mola shikeni, tunazidi kutangaza,
Kila mara tuombeni, na dua kufululiza,
Nawaaga kwaherini, mengi sitaki ongeza,
Dini imetukataza, ngoma, muziki haramu.