Mashairi: Sigara, Shisha, Kiko, Tumbaku
Sigara, Shisha, Kiko, Tumbaku
‘Abdallah Bin Eifan
(Jeddah, Saudi Arabia)
Salamu zenye harara, zifike pwani na bara,
Sikiliza muhadhara, naomba fanya subira,
Kwa wengi itawakera, basi acheni hasira,
Sigara ina madhara, na tena ina hasara.
Na tena ina hasara, sigara ina madhara,
Hii ndio “tabdhira,” na pesa inakupora,
Kwa mtu mwenye busara, kuiepuka ni bora,
Sigara ina madhara, na tena ina hasara.
Madhara kwa mazingira, na moshi ndio ishara,
Tusifanye maskhara, madhara yake kathira,
Wafanyao biashara, waache hii tijara,
Sigara ina madhara, na tena ina hasara.
Kiko, tumbaku na“shisha,” madhara kama sigara,
Ugoro nawakumbusha, zote hizo ni izara,
Zote zinatusumbusha, kila siku kila mara,
Sigara husababisha, madhara pia hasara.
Dini inatukataza, soma uone mwangaza,
Kila kinachoumiza, Mungu Amekikataza,
Moshi unapopuliza, pesa unazisambaza,
Sigara mbele ni giza , mwisho hutuangamiza.
Dini inatuhimiza, wazi imetueleza,
Shetani hakunyamaza, yupo anatuongoza,
Sana hutuelekeza, kule kwenye kuunguza,
Sigara inaumiza, madaktari uliza.
Sigara inachukiza, harufu kama kuoza,
Mtu ukimuuliza, uso anaugeuza,
Hataki kusikiliza, pale unapomweleza,
Sigara inapoteza, kuiacha tunaweza.
Na nguvu inapunguza, mapafu inakwaruza,
Cancer ikikuanza, mwisho wake ni jeneza,
Watoto utawaliza, yatima utabakiza,
Sigara huteketeza, kabisa hukumaliza.
Faida yake ni nini, hebu nipeni maoni?
Inaumiza moyoni, huziba mifelejini, (coronary thrombosis),
Hata njaa huioni, ina madhara tumboni,
Sigara ni mtihani, tujionee imani.
Mwenye mimba anakanywa, asivute huambiwa,
Mengi huharibikiwa, mwana anapozaliwa,
Nicotine inauwa, kama bado hujajuwa,
Sigara kama kulewa, inagonga kwenye kichwa.
Kina dada sikuhizi, kwa kuvuta huwawezi,
Wanavuta kwa mapozi, wanajifanya wajuzi,
Na kumbe ndio wapuuzi, na tena hawapendezi,
Sigara mwisho majonzi, mwisho wake ni machozi.
Kiumbe mwenye akili, akikanywa hukubali,
Akiambiwa ukweli, upesi anabadili,
Ninamuomba Jalali, mwisho nimeshawasili,
Sigara ni ukatili, zinaonyesha dalili.