Mashairi: Ugonjwa Wenye Huzuni, Ukimwi Ni Mtihani

Ugonjwa Wenye Huzuni, UKIMWI Ni Mtihani

                     Abdallah Bin Eifan (Rahimahu-Allaah)

www.alhidaaya.com

Salaam kwa watu wote, wa bara hadi wa pwani,

Dini ya Mungu (Allaah) tufuate, tusitishwe asilani,

Ridha za Mungu (Allaah) tupate, tuwe katika amani,

Ugonjwa wenye huzuni, UKIMWI ni Mtihani.

Afya, ubora, uzima, ni matunda ya mwilini,

Hii ni kubwa neema, kutoka kwa Rahmani,

Na mtu mwenye hekima, hujua yake thamani,

Ugonjwa wenye huzuni, UKIMWI ni Mtihani.

Ukimwi wenye lawama, ugonjwa wenye huzuni,

Watoto huwa yatima, madhambi yao ni nini ?

Wakose baba na mama, waleleke masikini,

Ugonjwa wenye huzuni, UKIMWI ni Mtihani.

Tuwaonee huruma, wamekosa kitu gani ?

Huu kweli ni dhuluma, na adhabu maishani,

Matendo haya si mema, kinyume na yetu dini,

Ugonjwa wenye huzuni, UKIMWI ni Mtihani.

Lini jamaa tutakoma, na shetani kumlaani,

Mpaka lini tutasema, mbona hivi ikhwani ?

Tazama tena tazama, usiingie shimoni,

Ugonjwa wenye huzuni, UKIMWI ni Mtihani.

SABABU yake uzinzi, na kupotea imani,

Pia kukosa malezi, watoto kule nyumbani,

Ni wajibu kwa wazazi, kuwaongoza kidini,

Ugonjwa wenye huzuni, UKIMWI ni Mtihani.

SABABU pia ni damu, sindano hospitalini,

Hawachunguzi timamu, dharau tupu kazini,

Lazima tuwalaumu, tufike mahakamani,

Ugonjwa wenye huzuni, UKIMWI ni Mtihani.

Ukimwi tafuta dawa, tembea kila makani,

Kuitibu wameshindwa, hata huko Marekani,

Vipi bado hujajuwa, ni ghadhabu ya Manani,

Ugonjwa wenye huzuni, UKIMWI ni Mtihani.

Tumemsahau Mungu (Allaah), kufuata ya duniani,

Tunafuata ya Wazungu, tabia za hayawani,

Picha nyingi za Kizungu, uchafu tupu machoni,

Ugonjwa wenye huzuni, UKIMWI ni Mtihani.

Tunaigiza mavazi, na tabia za kihuni,

Msichana yupo wazi, mtazame kifuani,

Maneno hasikilizi, amejipamba usoni,

Ugonjwa wenye huzuni, UKIMWI ni Mtihani.

Yeye wa kujisitiri, anapotoka njiani,

Akae akifikiri, anafuatwa na shetani,

Asifanye ujeuri, akikanywa na jirani,

Ugonjwa wenye huzuni, UKIMWI ni Mtihani.

Na vijana kadhalika, na wao wamo kundini,

Tabia kubadilika, atuvalie hereni,

Halafu hukusanyika, pamoja na wanandani,

Ugonjwa wenye huzuni, UKIMWI ni Mtihani.

Waanze ulevi kunywa, hawajijui vichwani,

Halafu wajichukuwa, waende zao kuzini,

Hapo anaambukizwa, mhanga sasa ni nani ?

Ugonjwa wenye huzuni, UKIMWI ni Mtihani.

Waanze kuusambaza, utapakae nchini,

Watu kuwaangamiza, msiba kila makani,

Tunaona majeneza, yanavyobebwa begani,

Ugonjwa wenye huzuni, UKIMWI ni Mtihani.

Mungu Anatukumbusha, Anatupa mitihani,

Tupate kujirudisha, tukumbuke ya mwishoni,

Hivyo Anatutingisha, tuamke usingizini,

Ugonjwa wenye huzuni, UKIMWI ni Mtihani.

Maasi yanapozidi, na madhambi ardhini,

Hughadhibika Wadudi, huko Aliko mbinguni,

Dua zetu zinarudi, Hazijibu asilani,

Ugonjwa wenye huzuni, UKIMWI ni Mtihani.

Kinga yake si mpira, kuivaa huko chini,

Kinga kumbuka akhera, na adhabu ya motoni,

Kinga fanya maghfira, kwa Mungu sana ombeni,

Ugonjwa wenye huzuni, UKIMWI ni Mtihani.

Watu wapewe mawazo, wasikie redioni,

Waeneze matangazo, kila siku gazetini,

Wafanye na maelezo, kwenye matelevisheni,

Ugonjwa wenye huzuni, UKIMWI ni Mtihani.

Na Mashekhe wasichoke, kuhubiri mitaani,

kila pembe na wafike, waeleze hadharani,

Mabwana na wanawake, wote wamo hatarini,

Ugonjwa wenye huzuni, UKIMWI ni Mtihani.

Liwe somo la elimu, walifundishe shuleni,

Wazingatie walimu, wakiwa madarasani,

Jambo hili ni muhimu, kulitia akilini,

Ugonjwa wenye huzuni, UKIMWI ni Mtihani.

Fanya ndoa ya halali, ukatulie nyumbani,

Shika kamba ya Jalali, mauti yapo mbeleni,

Unapokanywa kubali, Mashekhe kuwathamini,

Ugonjwa wenye huzuni, UKIMWI ni Mtihani.

Hakika nasikitika, nina majonzi moyoni,

Machozi yananitoka, nifikapo kaburini,

Hivyo wanapukutika, watoto wetu jamani,

Ugonjwa wenye huzuni, UKIMWI ni Mtihani.

Kuwaaga sinabudi, nawaomba samahani,

Kwa Mungu wetu turudi, na tusome Qur-aani,

Na sana tujitahidi, kuswali misikitini,

Ugonjwa wenye huzuni, UKIMWI ni Mtihani.

Share