Maana Ya Hadiyth Dhaifu

SWALI: 

asalam alaikum w w ndugu zangu katika imani baada ya kumshukuru allah na kmtakia sala ana amani mbora wa viumbe mtume m sw a was na ali zake, kwa kweli nakuta kieni kila la kheiri nabaraka zake mola, na akuzidishieni nguvu na imani katika juhidi hiyi ambayo sio rahisi kila mtum kujtuma, pia akupeni maisha marefu katika uwanja huyu wa dawa ili mzidi kututowa katia kiza. cha huyu ujahilia mpia ok ndugu zangu kwanza nakuombeni samahani kwa swali hili naomba mnielewe mimi kwa jina la mungu sija soma dini hata kidogo ila nafuatilia tu ka hivi mnavyo tuelimisha, biiman mimi sina haja ya kukujadili masheikh zangu isipokuwa mimi ni mdadisi tu hasa katika mambo ya dini, pia nimeshukuru kupata jibu mlilotowa kuhusu mapenzi ya mke na mume.ok sasa mimi nimeona katika maelekezo au muelezo mlio utumia kunijibu kwa kweli mimi kama kipenzi cha mtume nime kekarika kidogo kuona lipo neno lililo tumika kwa kuandikwa yakuwa kuna Hadiyth dhwaif je vipi maneno ya mtume ambaye alikuwa hasemi kwa matamnio ya nafsi yake ka jinsi mna tueleza yawe na udhaifu kwakweli naomba mniweke sawa hapo ili nielewe nini mana ya Hadiyth dhwaif, haitosho kutokana na uelewa wangu mimi ninavyo fahamu hadith ni matendo ya mtume au ni kauli yake, naomba ufafanuzi kwa kina wa billahi tawfiq, tana ndugu naomba mtusaidie kama mimi hapa nilipo naishi nchi ambayo imekithiri kwa maasi yani niko hapa holand

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Maulamaa wanasema kuwa:  Hadiyth dhaifu ni ile isiyokuwa na sifa zinazokubalika. Na wengine wakasema kuwa  Hadiyth dhaifu ni ile isiyostahiki kuitwa Sahihi wala Hasan (njema).

Zipo aina nyingi ya Hadiyth dhaifu zikiwemo:

Mursal:

Nazo ni zile zilizonyanyuliwa moja kwa moja kutoka kwa Taabi'iy  mpaka kwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم   

Taabi'iy ni Muislamu aliyeishi wakati wa Maswahaba رضي الله عنهم   akawaona lakini hajamuona Mtume صلى الله عليه وآله وسلم     

Kwa mfano Taabi'iy  aseme:

“Mtume wa Allaah  صلى الله عليه وآله وسلم    amesema…...”

Wakati yeye hajawahi kuonana na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم    

Maulamaa wamekhitalifiana juu ya kuzitumia Hadiyth za aina hii mafungu manne:

     1- Imaam Abu Haniyfah na Imaam Malik na baadhi ya wanavyuoni wanasema kuwa Hadiyth hizi zinafaa kutumika.

     2- Imaam An-Nawawi akieleza juu ya Jamhur kubwa ya Maulamaa na pia akimnukuu Imaam Shaafi'iy anasema kuwa Hadiyth za aina hii zinaweza kutumika kama ni hoja lakini si hoja ya moja kwa moja (ya kutegemewa).

     3- Imaam Muslim anasema; “Hadiyth Mursal kwetu sisi na kwa wengi kati ya wanavyuoni si hoja hata kidogo.

     4- Wengine wakasema kuwa inaweza kuwa hoja pale tu ikiwa imepokelewa kutoka kwa Tabi'iy mkubwa, kisha Hadiyth hiyo iwe imefanyiwa kazi na Swahaba yeyote au na wanavyuoni wengi.

Munqati'i:

Hizi ni zile Hadiyth zilizokatika Isnadi zake, yote sawa kukatika huko kuwe mwanzo au mwisho wa majina ya wapokezi.

Al Mudallas:

Nazo ni zile Hadiyth ambazo muelezaji aeleze kuwa amehadithiwa  na mtu aliyeishi katika zama moja kisha ikathibiti kuwa hawajapata kuonana. Au ahadithie kama kwamba amehadithiwa  na mtu huyo wakati ukweli ni kuwa hakuhadithiwa na mtu huyo, kwa mfano aseme:

“Amenihadithia  fulani.” Au: “Nilimsikia fulani.” Wakati ingekuwa sahihi kama angesema:

“Amesema fulani.” Au: “Kutoka kwa fulani.”

Maulamaa wanasema kuwa Mudallis (muelezaji wa Hadiyth hizi) hazikubaliwi riwaya zake hata kama aliwahi mara moja tu katika maisha yake kusema uongo katika hadiyth.

Wengine akiwemo Imaam Shaafi'iy wakasema kuwa; ni zile Hadiyth alizodallis tu hazikubaliki, lakini zile alizozielezea kwa njia sahihi zinakubalika.

Mudh twarib:

Nazo ni zile Hadiyth nyingi zinazogongana (Contradiction). Hadiyth aina hii zimedhoofishwa kwa sababu ya kugongana kwake na kutokuwa thabit.

Munkar:

Nazo ni zile zilizohadithiwa na ‘Dhaifu’ (asiyeaminika) kisha zikakhitilafiana na Hadiyth zilizohadithiwa na Thiqah (mwenye  kuaminika).

 

Al Mudha'af:

Nazo ni zile zilizodhoofishwa na baadhi ya Maulamaa kutokana na udhaifu wa wapokezi wake, wakati baadhi nyingine ya Maulamaa wakasema kuwa ni sahihi.

Al Matruk:

Nazo ni zile zilizohadithiwa na mtu anayetuhumiwa kwa uongo katika Hadiyth au hata katika mazungumzo yake. Au anayetuhumiwa kuwa ni faasiq wa maneno au vitendo. Matruk pia ni yule mwenye kusahau sana au mwenye kukosea sana.

Wakati gani Hadiyth dhaifu inakuwa na nguvu?

Hadiyth dhaifu inapata nguvu pale tu ikiwa rawi wake (mwenye kuhadithia) anatuhumiwa kuwa ameanza kusahau sahau sharti awe thiqah hatuhumiwi kwa uongo wala kwa ufaasiq wala kwa kusahau sana. Kisha Hadiyth alozungumza juu yake ziwe zimepokelewa kwa njia nyingi sana, na hapo inapanda darja na kuwa ‘Hadiyth Hasan.’

Na hii ni kwa sababu imepokelewa kwa njia zinazokubalika tena kwa njia ya rawi asiyetuhumiwa kwa uongo au kwa sababu ovu za kumdhoofisha.

Kuzifanyia kazi Hadiyth dhaifu:

Maulamaa wamekhitalifiana katika hukumu za kuzifanyia kazi Hadiyth za aina hii katika makundi matatu:

     1- Wapo wanaosema kuwa Hadiyth hizi hazifai kuzifanyia kazi kabisa, yote sawa iwe katika kuamrisha mambo ya fadhila au katika hukmu. Na hii ni kauli ya Yahya bin Ma'iyn na Abubakar bin Al-'Arabiy na pia Al-Bukhaariy na Muslim.

     2- Wengine wakasema kuwa Hadiyth hizi zinaweza kufanyiwa kazi.

     3- Na wengine wakasema kuwa Hadiyth hizi zinaweza kufanyiwa kazi katika mambo ya fadhila na katika kuwaidh watu tu. Na kwamba zisitumike katika kutoa hukmu au katika ibada, tena ziwe zimekamilisha baadhi ya masharti kama vile asituhumiwe mmojawapo wa wapokezi wake kwa uongo au ufuska nk. Na pia udhaifu wa Hadiyth usiwe mkubwa sana, na pia mtu anapoelezea Hadiyth ya aina hii awajulishe watu kuwa ina udhaifu ndani yake.

 

Anasema Dr. Muhammad Ajjaj Al Khatwiyb katika kitabu chake ‘Al-Mukhtaswar Al-Wajiyz fiy 'Uluum al Hadiyth:

“Mimi naunga mkono rai ya mwanzo inayosema kuwa Hadiyth dhaifu zisifanyiwe kazi kabisa. Zipo Hadiyth za kutosha zilizo sahihi katika mambo ya fadhail na mawaidha kiasi ambapo haina haja ya kuingiza Hadiyth zenye shaka zinazoweza kuwa ni maneno ya uongo aliyozuliwa Mtume wa Allaah صلى الله عليه وآله وسلم         

Pia fadhail na tabia njema ni katika mambo muhimu sana katika dini kwa hivyo haina haja kuzitumia Hadiyth dhaifu kwa ajili yake.”

 

Rai ya Dr. Muhammad Al Ajjaj ni bora zaidi kwa sababu mtu atawezaje kuiamini Hadiyth iliyosimuliwa na Mudallis, mtu mwenye kubadilisha majina ya mashekhe au ya miji akijua kuwa anawadanganya wasikilizaji wake, au muongo ‘Kadhaab’ anayependa kuwadanganya watu katika mambo ya kidunia ambaye hatoshindwa kuwadanganya katika mambo ya dini.  

Na vipi mtu ataweza kuifanyia kazi Hadiyth Mudhtwarib inayogongana na Hadiyth sahih au Hadiyth Matruk iliyodhoofishwa kwa ajili ya tabia ovu za msimulizi kwa ajili ya uongo na ufuska n.k.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share