Hadiyth: “Tengezeni Swafu” Katika Swalaah Ya Jamaa: Ufafanuzi Wake
SWALI:
Kuhusu Hadhithi “Tengezeni swafu zenu kwani katika kutengeza swafu ni katika kusimamisha Swalah” Naomba kufahamishwa kama kuna maelezo zaidi, kwa sababu ni wazi kabisa hadithi inaumaanisha
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani kwa swali lako kuhusu maelezo ya Hadiyth uliyoitaja hapo juu.
Hadiyth hiyo inatufahamisha kuwa kutengeneza swafu ndio kukamilika kwa Swalaah, kwa maana kuwa ikiwa swafu ni kombo au si sawa basi Swalaah hiyo huwa na kasoro kubwa na kupungua daraja yake kwa wale wanaosababisha
Na katika kutengeneza Swafu ni kuinyoosha sawa sawa kabisa bila kupinda wengine kuwa mbele kidogo na wengine kuwa nyuma. Kadhalika unyooshaji wa Swafu hunyooshwa kwa kulingana visigino vya wenye kuswali na si kulingana vidole vya miguu
Vilevile, kutengeza Swafu na kuinyoosha ni watu kugusana mabega kama alivyoeleza Swahaba Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa walikuwa wakikamatanisha mabega
Tutazame Hadiyth zifuatazo tuone umuhimu wa Swafu na kuinyoosha na kuitengeneza:
Imepokewa na mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakika Allaah na Malaika Wake wanawaombea wenye kuswali katika swafu, na mwenye kuziba upenyo (nafasi) Allaah anamnyanyua daraja yake” (Ahmad, Ibn Maajah, Ibn Khuzaymah na Ibn Hibbaan).
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliusia: “… Wala msiache upenyo kwa Shaytwaan, na mwenye kuunganisha swafu, Allaah Humuunganisha na mwenye kuikata, naye Hukatwa na Allaah” (Ahmad na Abu Daawuud, na kusahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy).
Imepokewa na Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyesema: Kulikimiwa Swalah, naye Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatukabili kwa uso wake, akasema: “Tengezeni swafu zenu, kwani mimi nawaona nyuma ya mgongo wangu” (al-Bukhaariy na Muslim).
Imepokewa na Jaabir bin Samurah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa alitutokea Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Je, hamupangi swafu
Imepokewa na Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Tengezeni swafu zenu kwani katika kutengeza swafu ni katika kusimamisha Swalah” (al-Bukhaariy na Muslim).
Na imepokewa na an-Nu‘man bin Bashiyr (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mtaendelea kuweka swafu sawa au Allaah Atazibadilisha nyuso zenu” (al-Bukhaariy na Muslim). Na katika riwaya ya Ahmad na Ibn Hibbaan: “… au Allaah Atazibadilisha nyoyo zenu”.
Kinyume na leo tunavyoona kwenye Misikiti mingi hususan ya ndugu zetu wa Ki-Hanafi ambao hawataki kugusana na wenzao miguu wala mabega na hivyo kuachwa nafasi katika Swafu, nafasi ambazo wanaweza kuingia watu wengi katika Swafu moja kama nafasi hizo zingezibwa na kama wangelifuata mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) vizuri kama yalivyopokelewa na kuacha kasumba za kimadhehebu ambazo zimeiletea madhara makubwa Diyn hii.
Na Allaah Anajua zaidi