Miswaak (Mswaki) Utumiaji Wake
SWALI:
Assalaam 'alaykum samahanini
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu upigaji wa mswaki wa kijiti.
Mswaki ni miongoni mwa Sunnah nzuri ambazo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuachia na kusema:
“Lau si ugumu ambao Ummah wangu ungepata ningeweka ulazima wa kupiga mswaki kabla ya kila wudhuu” (Maalik, Abu Daawuud, ash-Shaafi’iy, al-Bayhaqiy na al-Haakim).
Msuwaki unaweza piga katika sehemu nyingi kwa mfano chooni, Msikitini wakati unatawadha, unapoingia nyumbani, pia chumbani. Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) amesema:
“Kitu cha kwanza ambacho Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifanya anapoingia nyumbani ilikuwa ni kupiga mswaki” (Muslim).
Utumiaji huwa ni kwa kutumia kijiti au kitu chengine chochote kusafisha meno yake. Kitu bora cha kusafishia meno ya mmoja wetu ni kijiti cha mti wa arak ambao unapatikana Hijaaz.
“Mswaki unasafisha mdomo na unampendeza Mola” (Ahmad, at-Tirmidhiy na an-Nasaa’iy).
Utumiaji wa mswaki unapendeza kila wakati, lakini zipo nyakati nyingine ambazo inapendeza zaidi haswa nyakati zifuatazo:
1. Wudhuu,
2. Swalaah,
3. Usomaji wa Qur-aan,
4. Unapoamka, na
5. Pindi ladha ya mdomo inapobadilika. Wasiofunga au waliofunga wanaweza kutumia bila ya tatizo lolote. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anatumia mswaki na huku amefunga (Ahmad, Abu Daawuud na at-Tirmidhiy).
Ni Sunnah kuuosha mswaki baada ya kupiga, amesema
“Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Alipomaliza kutumia mswaki, alikuwa ananipatia mimi. Nilikuwa nauosha, nautumia, nauosha tena, kisha namrudishia” (Abu Daawuud na al-Bayhaqiy).
Na pia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kutuonyesha umuhimu wa mswaki amesema:
“Mambo kumi ni katika fitrah: … kupiga msuwaki, …” (Muslim na Abu Daawuud).
Tunaona hata katika Siyrah ya Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa hata wakati alipokuwa katika sakaraatul Mawt kitandani kwa Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) alimuona nduguye mama ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) aitwaye ‘Abdur-Rahmaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) akiwa na mswaki wa mti akautamani na Mama wa Waumini akauchukua na kuutafuna kuulainisha kisha akampatia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kusugua nayo meno yake; hiyo ni kuonyesha jinsi gani Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyokuwa akilipendekeza jambo hilo.
Ni muhimu kwetu sisi kuifufua Sunnah hii na kuwafundisha watoto wetu kutumia mswaki wa kijiti kwa kusafisha meno
Na Allaah Anajua zaidi