Mume Hataki Kuswali Anasema Hana Muda Yuko Kazini

SWALI

 

Asalam alekum. Naomba munijulishe nifanye nini mume wangu hataki kuswali asema hana time yuko kazini ni sawa kwa uwislamu na mimi ni mke wake nifanye nini?


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mumeo asiyetaka kuswali. Ni ajabu kwa Muislamu kuwa na tabia kama hiyo ingawa inatokea kwa wengi. Hii ni hatima na matokeo ya malezi mabaya majumbani mwetu.

 

Dada yetu ulifanya makosa ulipokuja kuposwa ukawa ni mwenye kukubali bila ya kutaka kujua hali ya yule anayetaka kukuoa. Kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuusia:

 

Akikujieni yule ambaye mnaridhika Dini na maadili yake muozesheni” (at-Tirmidhiy).

 

Lakini huyu haridhishi Dini wala maadili yake. Haya pia kwetu ni matokeo ya kupuuza nasiha na maelekezo ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa sababu moja au nyingine. Hili ni tatizo sugu katika jamii yetu ulimwenguni. Katika kila sehemu jamii ya Kiislamu inakuwa na tatizo hili hili.

 

Hata hivyo, tatizo hili lishatokea kwako sasa ni wewe kukabiliana nah ali uliyonayo hivi sasa. Muislamu mwanamme hafai kukaa katika ndoa na mwanamke ambaye haswali na kinyume chake pia ni sawa.

 

Tufahamu kuwa katika sababu zinazokubalika kisheria mtu akose Swalah, hiyo sababu ya kazi si moja wapo. Ni ajabu kwa Muislamu akawa ni mwenye kusema hivyo kwani Swalah anaweza kuiswali mahali popote pale, akiwa kazini, safarini, uwanjani na sehemu nyingine nyingi. Kuwa kazini si udhuru wa mtu kuacha Swalah.

 

Swalah ndiyo yenye kumtofautisha Muislamu na kafiri, Muislamu huwa haachi Swalah ilhali kafiri hajui Swalah. Mbali na kuwa kuna tofauti baina ya wanazuoni kuhusu ukafiri huo, wengine wakasema kwa kuacha Swalah tu, ikiwa kwa kupuuza au kuona si lazima basi amekuwa kafiri. Wengine wakasema ukiwa unaona si faradhi basi umekuwa kafiri. Kwa hali zote kuacha Swalah ni dhambi kubwa na kunamueka mtu pabaya.

 

Jambo ambalo unatakiwa ufanye ni kujaribu kuzungumza naye, tuma watu hasa Mashaykh kuzungumza naye na uitishe kikao kuangazia suala hilo baina yako, yeye, jamaa zake na jamaa zako. Ikiwa kumepatikana ufumbuzi sawa kama hakukupatikana basi itabidi uende kwa Qaadhi uelezee kesi yako hiyo. Hakuna uwezekano katika Dini hii kwa mwanamke kuishi katika ndoa na mwanamme asiyeswali. Na kwa sababu hiyo Qaadhi ataweza kuamua kuwaachisha ikiwa mume hayuko tayari kuswali, na ikiwa ataamua kujirkebisha kabla ya hatua hiyo na kuswali, basi mnaweza kuenedela kuishi pamoja inshaAllaah.

 

Pia, mpatie makala katika kiungo kifuatacho apate kutambua umuhimu, fadhila na madhara ya kuacha Swalah:

 

Swalah

 

Twakutakia kila la kheri na twamuomba Allaah Aliyetukuka Akupe tawfiki ya kuweza kumrekebisha mumeo ili aingie tena katika Dini hii kikamilifu.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share