Kununua Visanduku Vya Cable Za Internet Vilivyofunguliwa Kumwezesha Mtu Kutazama Vipindi Bure

SWALI:

 

assalam alaikum,kuna cable za ntl ambazo zauzwa kimpango pauni 100/= alafu hulipi tena, ambapo unaweza kuangalia mpira, vipindi vya kihindi na vitu vengine. Ambapo watu wengine wanalipia. Sasa ningependa kujua kama haifai mimi kuwanacho hicho cable au yafaa, na kama haifai je naweza kukiuza nikapata pesa zangu au nifanye nini? Assalam alaikum;


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kununua cable za internet. Tufahamu kuwa Uislamu ni mfumo kamili wa maisha na hakuna chochote isipokuwa tumeelezewa kinaganaga.

 

Hakika huo ni wizi wa dhahiri na udanganyifu ambao Uislamu umeukemea kwa hali za juu kabisa. Madhara yake ni makubwa sana hapa hapa duniani lau utakuja gunduliwa na vyombo husika na kufedheheka, na kesho Akhera utapata adhabu kubwa zaidi kwa dhuluma hiyo. Tufahamu kuwa adhabu ya wizi hapa duniani katika sheria ni kukatwa mkono kama alivyosema Allaah Aliyetukuka:

 

"Na mwizi mwanamme na mwizi mwanamke, ikateni mikono yao; malipo ya yale waliyoyachuma. Ndiyo adhabu, itokayo kwa Allaah" (5: 38).

Muislamu wa kweli hafai kufanya hivyo na inatakiwa uachane na jambo hilo na hiyo cable usiwe ni mwenye kumuuzia mtu kwani kufanya hivyo ni kusaidia uhalifu na wizi. Hivyo, kubali hasara kama uliinunua kwa wizi, na iharibu au itupe asiipate mwengine.

 

Jingine ni kuwa kama ulivyotaja kuwa cable hizo watu wazinunua kwa sababu wanaona mipira au filamu za kihindi n.k., tunataka kukutanabahisha na kukujulisha kuwa Muislam hakuletwa hapa duniani kutumia wakati wake kuupoteza kwa kutazama mipira na sinema za kihindi au za zozote zile zenye malengo ya kuliwaza, kufurahisha, kuburudisha, kupumbaza n.k. Sinema nyingi hazikosi vipande visivyo vya maadili, kama mchanganyiko wa wanawake na wanaume, ngono, mapenzi, kushikana, visa vya mapenzi, muziki na balaa na uchafu  mbalimbali. Mbali na ushirikina wa kutazama miungu ya kibaniani kwenye hizo sinema za kihindi, kutukuzwa miungu hiyo, nyimbo na miziki ambayo ni haramu yote hayo katika Dini yetu. Mipira pia ni masuala yenye utata haswa yanapochukua wakati wa Muislam na kumcheleweshea Ibaadah zake na hata kumkosesha kabisa. Pia kwa wanawake kutazama wanaume walio nusu uchi wenye kucheza mipira ni jambo lisilofaa kisheria.

 

Tunakunasihi, epukana na dhuluma hizo za kununua cable za wizi ambao tunasikia umenea sana Uingereza na nchi kama hizo za Magharibi, hasa katika jamii ya Waswahili, hakuna tofauti ya kumdhulumu au kumuibia Muislam au kafiri katia Dini yetu; yote ni wizi na hukumu ni moja. Pia jiepushe na kutazama sinema za kihindi na zinginezo zenye uchafu wa maadili na upotezaji muda na kukupelekea kuishi katika ulimwengu wa ndoto.

 

Tuna imani kuwa wewe ni mtu mwenye nia njema na ndio umeamua kutuuliza swali hili, kwani wapo wengi wanaofanya haraam na kuendelea bila kushtuka wala kuwa na wasiwasi. Hivyo, tuna imani kuwa uko tayari kuepukana na madhambi hayo na kuwa karibu zaidi na Allaah Aliyetukuka. Na inshaAllaah utakuwa ni katika wale wenye kupendwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share