Inafaa Kuibia Serikali Mita Za Taa?

 

Je Inafaa Kuibia Serikali Mita Za Taa?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI

 

assalaam alaikum nashkuru sanaa kwa kunijibu maswali yangu mengi alla akulipenl ila nna tatizo jengine mimi kama mnavojua huku kwetu zanzibar matumizi ya umeme ni madogo kwenye nyumba zetu lakini hubambikiziwa bili kubwaa pengine kwa mwezi utalipa hata sh 30000 sasakuna fundi ataibana mita nitalipa sh 7000tu kwa mwezi jee mashekh wetu kisheria inafaa?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Tunashukuru kuona kwamba ndugu zetu wako katika khofu ya kujiepusha na maovu na kuchuma dhambi na hivyo ndivyo anavyotakiwa Muislamu awe kila anapokosa ajirudi.

 

Lakini kuna dhambi ambazo hugeuka kuwa ni dhulma nazo ni baina ya mja na Rabb wake kama kumshirikisha Allaah (‘Azza wa Jalla).    Na zilizo baina ya bin Aadam na bin Aadam mwenzake. Na  Zilizo baina ya mja na Rabb wake, huenda Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa)   Akamsamehe pindi akiomba maghfirah na tawbah kabla ya kufariki huyo mtu au kabla ya jua kuchomoza upande wa Magharibi.

 

Ama dhambi zilizo baina yake na baina ya mwenzake hizi huwa ni haki za huyo mwenzake, na haifai kabisa kuchukua haki ya mtu kwa aina yoyot  kama kumuonea au kumvunjia heshima yake au kumchukulia mali yake na kadhalika, kama tunavyopata mafundisho katika Hadiyth hizi ifuatayo:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ أَتَدْرُونَ مَا الْمُفْلِسُ قَالُوا الْمُفْلِسُ فِينَا مَنْ لَا دِرْهَمَ لَهُ وَلَا مَتَاعَ فَقَالَ إِنَّ الْمُفْلِسَ مِنْ أُمَّتِي يَأْتِي يَوْمَ الْقِيَامَةِ بِصَلَاةٍ وَصِيَامٍ وَزَكَاةٍ وَيَأْتِي قَدْ شَتَمَ هَذَا وَقَذَفَ هَذَا وَأَكَلَ مَالَ هَذَا وَسَفَكَ دَمَ هَذَا وَضَرَبَ هَذَا فَيُعْطَى هَذَا مِنْ حَسَنَاتِهِ وَهَذَا مِنْ حَسَنَاتِهِ فَإِنْ فَنِيَتْ حَسَنَاتُهُ قَبْلَ أَنْ يُقْضَى مَا عَلَيْهِ أُخِذَ مِنْ خَطَايَاهُمْ فَطُرِحَتْ عَلَيْهِ ثُمَّ طُرِحَ فِي النَّارِ

 Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli   wa Allaah  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Je, mnamjua muflis?)) Wakasema [watu]: “Muflis kwetu sisi ni yule miongoni mwetu asiyekuwa na dirhamu [pesa] wala vyenye kumnufaisha yeye hapa duniani.” Akasema  Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam: ((Hakika muflis katika Ummah wangu ni yule atakayekuja Siku ya Qiyaamah na Swalaah, Swawm na Zakaah, lakini amemtusi huyu, amemsingizia huyu mwingine kuwa amezini, amekula mali ya huyu, amemwaga damu ya mwingine na kumpiga mwengine. Thawabu zake zitapatiwa huyu na yule mpaka zimalizike. Na zinapokwisha basi madhambi ya hao [aliowadhulumu] atabandikwa nayo, kisha aingizwe Motoni)) (Muslim)

 

Kitendo hicho cha kubana mita za umeme wa serikali ili itembee polepole na uweze kulipa gharama ndogo, ni kitendo cha wizi na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amelikataza jambo hili kwa makatazo makali kabisa hata Ametoa hukmu yake kuwa ni kukatwa mkono kama Anavyosema:

 

وَالسَّارِقُ وَالسَّارِقَةُ فَاقْطَعُوا أَيْدِيَهُمَا جَزَاءً بِمَا كَسَبَا نَكَالًا مِّنَ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ ﴿٣٨﴾

Mwizi mwanamume na mwizi mwanamke ikateni (kitanga cha) mikono yao; ni malipo kwa yale waliyoyachuma, ndio adhabu ya kupigiwa mfano kutoka kwa Allaah. Na Allaah ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote.    [Al Maaidah: 38]

 

Nayo pia huwa ni dhulma pindi hatorudisha mtu haki hiyo aliyochukua. Na inabidi arudishe haki hiyo kabla ya mauti kumfika bin Aadamu au sivyo itabidi ahesabiwe Akhera kama tulivyoona katika Hadiyth hiyo ya juu.

 

Ikiwa hakuna uwezekano wa kumrudishia mtu haki yake, kama kuwa na khofu kuwa labda itamletea madhara zaidi, basi anatakiwa Muislamu aombe  maghfira na Tawbah, kisha baada ya kuacha kitendo hicho kabisa, azidishe mema yake na amfanyie wema yule mwenzake aliyemdhulumu na kumuombea maghfira na du'aa.  

 

Vile vile mnasihi na huyo fundi maana naye anashiriki kwenye wizi huo, na ni wangapi anaowasaidia kwenye wizi huo?? Mfikishie nasaha na mwambie amche Allaah.

Na Allaah Anajua Zaidi

 

 

Share