Kukopeshwa Na Muajiri Lakini Serikali Kuchukua Kodi Ya Mkopo

SWALI:

 

Asaalaam alaykum,

Naomba kuuliza ikiwa muajiri wako atakukopesha pesa na kukutaka irejeshe kiwango kile kile. ila kuna sheria ya serikali inayosema kila mkopo mtumishi wa shirika la umma au serikali, akikopeshwa. Anatakiwa alipe kodi ya mkopo kwa mujibu wa sheria za nchi. Jee hii riba. Alokukopesha anachukua kiwango kile kile ila ile percent anaipeleka serikalini. Jee itakuwa riba hiyo?


 

JIBU: 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. 

Shukrani kwa swali lako kuhusu kukopeshwa na muajiri.

Hakika ni jambo la kushangaza ambalo hatujawahi kusikia kuwa mtu anakopesha kutoka kwa muajiri wake kisha serikali ikawa ni yenye kuingilia kati katika mapatano yenu na kuchukua kiwango cha ziada. Ni vigumu kuelewa serikali inawezaje kujiingiza hata katika masuala kama hayo. 

Hata hivyo, kwa kukujibu ni kuwa msingi wa kukopeshana katika Uislamu ni kusiwe na ziada wakati wa kulipa, kwani ziada hiyo ni Ribaa. Kwa hakika ziada hiyo serikali inayochukua ambayo wanaiita kodi ni Ribaa kwa sababu hakuna kodi kwa serikali kwa mapatano ya kukopeshana baina ya mwajiri na muajiriwa. Hivyo, kukiwa na njia nyingine itakuwa bora lakini ikiwa hakuna njia nyingine ya kuweza kukopeshana bila ya kulipa hiyo kodi basi tunakushauri utafute sehemu nyingine ambayo unaweza kukopa kwa ndugu au jamaa ambapo hutotozeshwa Ribaa.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share