Kuweka Mashine Ya ATM Katika Nyumba Inafaa? Ikizingatiwa Masuala Ya Riba

 

SWALI:

 

NINAFAHAMU KUWA HAIFAI KUTOA ENEO LAKO KUPANGISHA BANK INAYOJIHUSISHA NA RIBA, SASA JE KUWEKA MASHINE YA ATM AMBAYO ITAWASAIDIA WAPITA NJIA NA WASAFIRI KUTOA PESA ILI KUKIDHI HAJA ZAO HATA NYAKATI ZA USIKU, JE UISLAM UNANIRUHUSU?

JAZAKUM LLAAH KHER

 


 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 Shukrani zetu za dhati kwa swali lako. Tumefahamu kutoka swali lako kuwa umetambua uharamu wa Riba. Hakika ni jambo la kushukuriwa na kupongezwa kwani sio kila Muislamu yumo katika hima ya kujiepusha na madhambi kama haya. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akuzidishie hima hii na Akuzidishie Iymaan kwa ujumla ya dini yako, kisha Akulipe kwa Kukuzidishia kheri na baraka nyingi.  

Riba ni miongoni mwa madhambi makubwa yenye kuangamiza. Hivyo, kwa sababu hiyo Uislamu ukaupiga vita kabisa muamala wa Riba kwa njia yoyote ile. Mwenye kufanya hivyo huwa ametangaza vita na Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Allaah Aliyetukuka Anasema:

"Na kama hamtafanya (hivyo), basi fahamuni mtakuwa na vita na Allaah na Mtume Wake. Na mkiwa mmetubu, basi mtapata rasilmali zenu; msidhulumu wala msidhulumiwe" (2: 279).

Msingi wa Uislamu ni kuwa unapokataza dhambi basi hukataza na njia zote zinazompelekea katika dhambi hilo. Ndio Allaah Aliyetukuka Akatuambia: "Wala msikaribie zinaa. Hakika hiyo zinaa ni uchafu mkubwa na ni njia mbaya kabisa" (17: 32).

Allaah Aliyetukuka hapa Hakukataza tu zinaa bali na vinavyompelekea mja katika zinaa yenyewe. Sasa kitu chochote kinachompelekea katika dhambi nacho ni dhambi katika Sheria yetu tukufu. Hivyo, katika mas-ala ya zinaa Uislamu ukafanya ni kosa kwa mtu kumuangalia mtu wa jinsia nyingine kwa matamanio, kusalimiana kwa mikono, kukaa faragha, kutazama picha chafu na nyinginezo zote ni haramu. Uislamu unatatua tatizo la dhambi kwa kukata kuanzia mzizi na sio shina la mti pekee.

Na tufahamu kuwa Uislamu pia una msingi unaotokana na maneno ya Allaah: "Na saidianeni katika wema na ucha Mungu, wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na mcheni Allaah; hakika Allaah ni Mkali wa kuadhibu" (5: 2). Huko kuweka mashine ya ATM katika nyumba ni kusaidia katika kuendeleza dhambi la Riba na kuisaidia benki yenyewe, hivyo kufanya jambo hilo kuwa halifai.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share