Jimai: Akiota Ndoto Ya Jimai Mchana Wa Ramadhaan Afanye Ghuslu? Je Aendelee Na Swawm?

SWALI:
 
Assalamu aleikum warahmatullahi wabarakatuh.  Swali langu ni kuwa nimelala mchana wa ramadhan nikaota ndoto ya utu uzima, nikaamka na kuona majimaji kwa nguo yangu.  Je nitaoga josho la janaba ama nitaendelea na saum yangu.

Jazakallahu kheir.

 


JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Asli katika mas-ala ni kuwa swawm ya mtu mume au mke haibatiliki kama ataamka wakati wa alfajiri na janaba iwe janaba kwa sababu ya kulala na ahli yake au kwa kutoa kama ilivyothibiti katika hadithi kutoka kwa Mama wa Waumini ‘Aaishah na Mama wa Waumini Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘anhumaa) wamesema:

“Kwa hakika Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa ’ala aalihi wa sallam) alikuwa inamdiriki Alfajr hali ya kuwa na janaba kutokana ahli zake, kisha hukoga na kufunga” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, Kitaab cha Swawm, mlango mwenye kufunga na kuamka na janaba].

 

Hivyo basi hukumu ni kuwa Swawm haibatilika bali ipo na inaendelea kwa kila atakayelala mchana na kuota ndoto ya utu uzima, awe mwanamume au mwanamke.

 

Kitacho kulazimu ni kukoga josho na kuendelea na Swawm yako na huna kulipa wala fidia kwani huna kosa lo lote.

 

FAIDA: Kuyatoa manii –maji ya uzazi- kwa makusudi iwe kwa mkono au kwa kuchezewa na Mkeo au kwa kutazama kwa matamanio mpaka yakatoka au njia yoyote ile itayokuwa na shahwah, funga inabatilika na itamlazimu mhusika kuilipa siku hiyo. Ama yakiwa yametoka kwa kutazama -bila kukusudia- basi haiharibu Swawm yake.  

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share