Kwa Iliyemfikia Ramadhwaan - Nasaha Kwa Wanawake
Kwa Iliyemfikia Ramadhwaan - Nasaha Kwa Wanawake
Imekusanywa na Ukht Haliymah ‘Abdullaah
Kusudio dada yangu ni vipi utaishi katika Ramadhwaan kama inavyotakikana kutumia kila hatua kwa kufuata yaliyoamrishwa kujikurubisha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kufahamu maana ya mwezi huu mtukufu na kufaidika nao kwa kusafisha nafsi na kuitakasa katika miezi iliyobaki sio kama baadhi ya watu wanaoabudia Ramadhwaan tu na kucheza katika miezi mingine nawe unajua Mola wa Ramadhwaan ndiye wa miezi mingine pia.
Ukiingia mwezi nawe una afya njema ujue ni neema kubwa inahitaji Kumshukuru Allaah na Kumsifu, Swawm ina ujira mkubwa hakuna ajuaye ila Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na ndani yake kuna usiku wa Laylatul Qadr ambao ni bora kuliko miezi elfu, takriban miaka themanini na nne hebu fikiri ukijaaliwa kupata usiku huu unaandikiwa umefanya kheri miaka yote hii! Shime tujipinde mwezi mzima tuweze kuupata usiku wenye heshima na fadhila nyingi. Katika mwezi huu unasamehewa madhambi na kuwekwa mbali na moto pia kumeandaliwa Jannah mlango maalum kwa wafungao unaoitwa Ar-Rayyaan.
Baada ya kugusia hayo tunarudi kuuliza je tumepanga nini cha kufanya katika huu mwezi mtukufu au tunaenda bila ratiba na kukaa na njaa na kiu bure?
Yahitaji tuweke nia ya kweli katika kupanga ratiba zetu Kwani tunaelewa majukumu ya kinamama katika malezi na kusimamia nyumba. Kila mtu apange kuendana na nafasi yake mfano:
Al-Fajr
Baada ya kuswali Alfajiri na Sunnah kabla yake unasoma du’aa na Qur-aan na kumtaja Allaah sana unaweza kupumzika baada ya hapo kidogo kwa kulala baada ya kutoka jua kisha unaswali Dhuhaa Rakaa mbili mpaka nane kadri ya utakavyoweza muhimu uanze na Rakaa kidogo ili udumu nayo hata baada ya Ramadhwaan jitahidi usilale mpaka Adhuhuri ikakufikia Kwani utakuwa mchovu na mvivu. Ujitahidi kuhudhuria mihadhara na darsa mbalimbali za dini na huu wakati wa asubuhi ni mzuri ili uweze kukamilisha siku vizuri.
Adh-Dhuhr
Unaswali Adh-Dhuhr na Sunnah zake. Jitahidi kusoma walau juzuu moja baada yake na unaweza kupumzika baada yake na kufanya shughuli za nyumbani.
Al-‘Asr
Swalah ya Al-‘Asr kisha du’aa za jioni baada ya hapo unaandaa futari na kama katika nyumba mpo wengi pangeni zamu ili kila mmoja apate muda mwingi wa kufanya ‘Ibaadah wakati wa kuaandaa futari sikiliza mawaidha au Qur-aan au unaweza kumtaja Allaah kwa moyo.
Al-Maghrib
Unafungua Swawm na tende au maji usisahau du’aa kwani ni yenye kujibiwa. Usizidishe katika kula kwani mara nyingi tunataka kulipiza milo mitatu ya siku. Tule katika wakati mmoja na hili ni tatizo katika huu mwezi na yanajitokeza matatizo ya kuvimbiwa hata kunyanyuka huwezi na kuwa mvivu na Swalah ya taraawiyh, chakula hakisagiki! Inachotakiwa ule kiasi na baadaye unaweza kula tena. Wamama wengi wanapitwa na Swalah kwa kujishughulisha kwao na kuaandaa futari ni kosa kubwa tuliepuke.
Baada ya kufuturu pale tulipokusanyika tujiepushe na kutazama vipindi, picha, tamthilia zisizofaa au kuongea maneno ya upuuzi na kwenda matembezi na ziara badala ya kujiandaa na Swalah ya taraawiyh.
Al-Ishaa
Ujitahidi kuswali kwa wakati na taraawiyh unaweza kuswali msikitini au nyumbani, muhimu wakati wa kutoka usipake mafuta mazuri wala kuvaa nguo za mapambo.
Jiepushe na kukesha, lala mapema uweze kuamka wakati wa daku (as-Suhuur) Kwani wengi tumezoea kula saa sita au kabla na huamki usiku! Jitahidi kunywa hata maji upate baraka zake ikiwa umeswali witri mapema. Na ujue usiku wa Laylatul Qadr unapatikana usiku na uwe unaomba du’aa hii ‘Allaahuma inaka ‘afuwu tuhibul ’afwa fa’af’aniy’ maana ‘Ee Allaah hakika wewe ni msamehevu unapenda kusamehe naomba unisamehe’ wakati huu wa usiku Anashuka Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na kuuliza “Nani aniombaye msamaha Nimsamehe? Nani mwenye shida nimpe? Nani anayeniomba nimuitikie? Isitupite fursa hii ipatikanayo katika kila usiku wengi wetu tumejawa na matatizo mbalimbali tutumie fursa hii.
Mengineyo
1. Usipoteze muda mwingi katika usingizi ukageuza usiku mchana na mchana usiku.
2. Jiepushe na kumuasi Allaah kwa kukesha mbele ya T.V.
3. Usizidishe ‘Ibaadah pasipostahili mfano Sunnah za qabliyah na ba’adiyah tumeambiwa jumla ni Rakaa kumi au kumi na mbili na ukiziswali vilivyo unajengewa nyumba peponi.
4. Jiepushe na maneno ya upuuzi; kusengenya, umbea, uchonganishi n.k. Utaharibu funga yako.
5. Jiepushe na kuitumia Ramadhwaan kwa kuzunguka madukani na haswa katika kumi la mwisho.
6. Toa sadaka hata kama huna mali unaweza kujitolea hata nguvu zako katika kazi au kunyesha maji na kufuturisha waliofunga.
7. Usifanye israfu katika chakula pika kiasi na usimwage utakuja ulizwa kesho neema hii.
8. Ramadhwaan ni fursa nzuri ya kuhama maasi kutubia jitahidi kuendelea na moyo huu. Usihudhurie hafla zenye miziki na michanganyiko ya wanawake na wanaume
9. Anayeswali msikitini asiende na watoto wachanga wanaolia au wanaoshawishi wanaoswali atakuwa mwenye kupata madhambi.
10. Msikitini ni fursa nzuri ya kuelimisha wasiojua hukmu za Swalah na mengineyo na hili ni jukumu letu sote.
11. Walio katika siku zao za ada au Nifaas (damu ya uzazi) wasiache kusoma vitabu vyenye manufaa, du’aa, adhkaar, kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), kusikiliza Qur-aan, kuleta istighfaar (kuomba msamaha), kujiunga na wanaofuturisha watu.
Usia Baada Ya Ramadhwaan
1. Jihadhari na usengenyaji, kutukana, kulaani, du’aa mbaya ujue hivi ni vitu vinavyowaingiza wanawake sana motoni.
2. Usivae Hijaab za mapambo na nakshi, nyepesi, zenye kubana kwani inapelekea kuwafitinisha wanaume.
3. Jiepushe na fitnah ya kuongea kwenye simu mambo yasiyofaa katika shariy'ah.
4. Jiepushe na kusoma magazeti yasiyokuwa na maadili (ya udaku) na yasiyojenga, yenye picha za wanawake walio uchi, ni haramu kuwepo katika nyumba yako ujue unakimbiza baraka.
5. Jiepushe kusikiliza miziki Kwani itakuweka mbali na mola wako na utakuja juta siku isiyofaa majuto.
6. Jiepushe na kujifananisha na wanaume kwa kuvaa suruali kukata nywele na kuiga mwendo wa kiume.
7. Usimuasi mumeo ukajidanganya kwa uzuri wako kuwa unaweza kupata mume mwengine wakati wowote ikakupelekea kumdharau! maisha ni subra inahitaji kurekebishana hakuna aliyekamilika.
8. Pupia kuswali kwa wakati, dumu katika kuomba msamaha, kisimamo cha usiku usiache kusoma Qur-aan kufunga Sunnah mbalimbali.
9. Watii wazazi wako wawili na uunge undugu na kukaa vizuri na majirani na kuwafanyia ihsani na kutowaudhi kuwatembelea wagonjwa na kuwasaidia madhaifu.
10. Uwe ni mwenye kuuliza yanayohusiana na dini yako pia usikilize mawaidha na Qur-aan na kuihifadhi isiwe kila mwaka huendi mbele.
11. Wape malezi ya Kiislamu watoto wako, wafundishe Qur-aan na tabia njema ili wawe wema na wakuombee du’aa baada ya kuondoka duniani.
Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atuwezeshe kuyatenda na kudumu katika mema.
Aamiyn.