Njia Kumi Za Kuhifadhi Qur-aan - 1
Njia Kumi za Kuhifadhi Qur-aani – 1
Kutoka
“كيف تحفظ القرآن في عشر خطوات – حسن أحمد بن أحمد همام”
Imekusanywa na Ukht Haliymah ‘Abdullaah
Haifichiki kwa kila Muislam ubora wa kuhifadhi Qur-aan Tukufu na fadhla za aliyeihifadhi.
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
الَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَتْلُونَهُ حَقَّ تِلَاوَتِهِ أُولَـٰئِكَ يُؤْمِنُونَ بِهِ ۗ وَمَن يَكْفُرْ بِهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ ﴿١٢١﴾
Wale Tuliowapa Kitabu wanakisoma kwa haki ipasavyo ya kusomwa kwake; hao ndio wanaokiamini, na atakayekikanusha basi hao ndio waliokhasirika. [Al-Baqarah: 121.]
Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
ثُمَّ أَوْرَثْنَا الْكِتَابَ الَّذِينَ اصْطَفَيْنَا مِنْ عِبَادِنَا ۖ فَمِنْهُمْ ظَالِمٌ لِّنَفْسِهِ وَمِنْهُم مُّقْتَصِدٌ وَمِنْهُمْ سَابِقٌ بِالْخَيْرَاتِ بِإِذْنِ اللَّـهِ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَضْلُ الْكَبِيرُ ﴿٣٢﴾
Kisha Tukawarithisha Kitabu wale Tuliowakhitari miongoni mwa waja Wetu. Basi miongoni mwao ni mwenye kudhulumu nafsi yake na miongoni mwao aliyekuwa wastani na miongoni mwao aliyesabiki kwa mambo mengi ya kheri kwa idhini ya Allaah. Hiyo ndio fadhila kubwa. [ Faatwir: 32.]
Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
إِنَّ الَّذِينَ يَتْلُونَ كِتَابَ اللَّـهِ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَأَنفَقُوا مِمَّا رَزَقْنَاهُمْ سِرًّا وَعَلَانِيَةً يَرْجُونَ تِجَارَةً لَّن تَبُورَ ﴿٢٩﴾
Hakika wale wanaosoma Kitabu cha Allaah na wakasimamisha Swalaah, na wakatoa kutokana na yale Tuliyowaruzuku kwa siri na dhahiri wanataraji tijara isiyoteketea. [Faatwir: 29.]
Katika hizi Aayah ni dalili ya ubora ya watu wa Qur-aan na kufaulu biashara yao na Allaah.
Ama Hadiyth za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallamni nyingi tunachukua zifuatazo:
Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakuna hasadi ila katika vitu viwili; mtu ambaye Allaah Amempa hekima (elimu) anaisimamia usiku na mchana, na mtu ambaye Allaah Amempa mali naye anatoa sadaka usiku na mchana.” [Muslim]
Kutoka kwa ‘Uthmaan bin ‘Afaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu): Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mbora wenu ni aliyejifunza Qur-aan na akaifundisha.” [Al-Bukhaariy]
Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amru bin Al-‘Aasw (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ataambiwa Swaahib al-Qur-aan: Soma kama ulivyokuwa ukisoma duniani hakika daraja yako peponi ni mwisho wa Aayah utakayosoma.” [At-Tirmidhiy]
Kutoka kwa Sahl bin Mu’aadh kutoka kwa baba yake kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mwenye kusoma Qur-aan na akaifanyia kazi yaliyomo atavalishwa mzazi wake taji siku ya kiyama mng’aro wake ni bora kuliko mwangaza wa jua katika nyumba za dunia lau ingekuwa kwenu mnadhani vipi kwa aliyeifanyia kazi.” [Abu Daawuwd]
Imepokewa katika Al-Bukhaariy kwamba walikuwa wanatangulizwa watu wa Qur-aan (Ahlul Qur-aan) kuliko wengine katika Swalaah na katika kuwazika mashahidi. Pia kuna mtu alimuoa mwanamke kwa Qur-aan aliyokuwa nayo kama mahari.
Kuhifadhi Qur-aan Ni Khaswa Kwa Ummah Huu
Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amejaalia Ummah huu kuwa bora kuliko Ummah zingine na Akajaalia wepesi kuhifadhi Kitabu hiki kimaandishi na kifuani.
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
بَلْ هُوَ آيَاتٌ بَيِّنَاتٌ فِي صُدُورِ الَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ ۚ وَمَا يَجْحَدُ بِآيَاتِنَا إِلَّا الظَّالِمُونَ ﴿٤٩﴾
Bali hizo ni Aayaat bayana (zimehifadhika) katika vifua vya wale waliopewa elimu. Na hawazikanushi Aayaat Zetu isipokuwa madhalimu. [Al-‘Ankabuwt: 49]
Na imekuja katika Hadiyth al-Qudsiy; “Na imeteremshwa kwako Kitabu kisichooshwa na maji unasoma ukiwa umelala na ukiwa macho.” [Muslim]
Wepesi Wa Kuhifadhi Qur-aan
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
وَلَقَدْ يَسَّرْنَا الْقُرْآنَ لِلذِّكْرِ فَهَلْ مِن مُّدَّكِرٍ ﴿١٧﴾
Na kwa yakini Tumeiwepesisha Qur-aan kwa kuikumbuka, basi je, yuko yeyote mwenye kuwaidhika? [Al-Qamar: 17]
Yaani tumemfanyia wepesi katika kuhifadhi je yupo anayeelekea akatafuta kuhifadhi akasaidiwa. [Tafsiyr Al-Qurtwubiy]
Mtoto mdogo chini ya miaka kumi ameweza kuhifadhi Qur-aan yote pia asiyejua Lugha ya Kiarabu ameweza kuhifadhi na haya yashatokea.
Kuhifadhi Qur-aan Haina Umri Maalum
Wanadhani watu wengi kwamba kuhifadhi Qur-aan ina wakati maalum katika maisha ya mwana-Aadam nayo ni kipindi cha udogoni wanarudiarudia methali mashuhuri “Kuhifadhi udogoni ni kama nakshi katika jiwe” na wanatolea dalili pia kwamba kipindi cha ukubwa inashughulika akili kwa mambo ya kimaisha.
Maneno haya yanahitaji yatizamwe upya, ni kweli kuhifadhi udogoni ina faida zake lakini haiishii hapo, mwana-Aadam akiwezeshwa na Allaah akajitahidi na kufanya subra anaweza kwa uwezo wa Allaah kulifikia hilo hata katika umri mkubwa.
Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) ilikuwa Qur-aan inawashukia wakaihifadhi vifuani mwao na hawakuwa katika umri wa utoto mfano Khalifa wanne, Ubay bin Ka’ab, Zayd bin Thaabit, Ibn Mas’uwd na wengineo.
Imekuja kutoka kwa Ibn Mas’uwd kwamba amesema, “Alifariki Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) nami nina miaka kumi na nimeshasoma al-Muhkam na al-Mufaswal (yaani kuanzia Suwrah Al-Hujuraat mpaka An-Naas). [Al-Bukhaariy]
Maana yake alikamilisha kuhifadhi Qur-aan baada ya hapo kama Ubay bin Ka’ab na Zayd bin Thaabit.
‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alihifadhi Suwratul Baqarah kwa miaka kumi na alipomaliza alichinja ngamia kumshukuru Allaah na hii ni dalili kwamba kuhifadhi haina umri maalum wala wakati maalum.
Njia Kumi Za Kuhifadhi Qur-aan
1. Hatua Ya Kwanza: Ikhlaasw Na Niyya Ya Kweli
Qur-aan ni maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na kheri ya maneno, Naye hampi hii zawadi na fadhla (ya kuhifadhi) ila kwa aliyemjua ukweli wa nia yake na ikhlaasw kwake Yeye. Na mwana-Aadam bila ya nia ya kweli na ikhlaas inakuwa kazi yake ni bure.
Anasema Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Kila tendo ni kwa niyah na kila mtu atalipwa kwa niyah yake.” [Al-Bukhaariy]
Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) anasema: “Mwenye kujifundisha elimu inayotakiwa kwa ajili ya radhi ya Allaah akaitafuta ili apate cheo cha kidunia hatopata harufu ya Jannah.” [At-Tirmidhiy]
Tunamuomba Allaah Atutengenezee niyya zetu na matendo yetu na Ajaalie tufanye kwa ajili Yake.