Katlesi Za Mviringo Za Samaki
Katlesi Za Mviringo Za Samaki
Vipimo
Viazi - 7-8 kiasi
*Samaki wa Tuna wa kopo - 3 vibati
Kitunguu - 1
Chumvi - kiasi
Pilipili manga ya unga - 1 kijiko cha chai
Pilipili mbichi - 1
Ndimu - 1 kijiko cha supu
Kotmiri (Corriander leaves) - ½ kikombe
Unga wa ngano - ½ kikombe
Chembe za mkate (Bread crumbs) - 1 kikombe
Mayai - 2
Mafuta ya kukaangia - kiasi
Namna Ya Kutayarisha Na Kupika
- Chemsha viazi hadi viwive, menya na uviponde uweke kando.
- Katakata kitunguu, pilipili mbichi, kotmiri ndigo ndogo (chopped) weka kando.
- Tia tuna katika kikaangao (frying pan), mchanganye na chumvi, pilipili manga, pilipili mbichi, kitunguu na ndimu kisha weka motoni mkaushe akolee viungo hivyo.
- Epua tia kotmiri uchanganye vizuri.
- Chukua kiasi cha viazi viliyopondwa ufanye kiduara mkononi na utie mjazo wa tuna.
- Kisha chukua tena viazi kiasi kidogo ufunike huku unatandaza viazi na kufanya duara kama ya picha. Endelea hadi umalize viazi na mjazo weka kando.
- Weka unga wa ngano katika sahani pekee. Weka chembe za mkate (Bread crumbs) katika sahani nyingine na piga yai katika sahani nyingine.
- Chukua donge la viazi ulojaza, chomva katika unga, kisha katika yai, kisha katika chembe za mkate, kisha uchome katika karai au kikaango.
- Zitakapobadilika rangi, epua weka kando zikiwa tayari.
Kidokezo:
Unaweza kutumia samaki wa nguru badala ya tuna ila itabidi umtie maji kidogo apikike vizuri hadi akauke.