Malaika Hawaingii Nyumba Iliyotundikwa Picha Za Familia?
Malaika Hawaingii Nyumba Iliyotundikwa Picha Za Familia?
Swali:
Asalam Aleikum,
Kwanza namshukuru Allaah kunipa uwezo wa kufungua huu mtandao pamoja na kuuliza suala lifuatalo. Allaah akupeni kila yalo mema kwa kuanzisha mtandao huu.
Mimi nyumbani kwangu nimeweka picha ukutani ya kwangu pamoja na ya mume wangu ya harusi na nimeweka ukutani picha za watoto wangu. Hizo hazikuchorwa ila ni camera jee ni vibaya malaika hawatopita. au hazina neno zilokatazwa ni zile za kuchora tu.
Jibu:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
In shaa Allaah tuzitazame baadhi ya Hadiyth kuhusu hilo kwanza kabla ya kuhitimisha.
Sa‘iyd bin Abul Hasan amesema nilipokuwa na Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) alikuja mtu akasema, “Ee Ibn ‘Abbaas! Riziki yangu inatokana na kazi yangu ya kutengeneza picha hizi”. Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) alisema: “Nitakuambia yale tu niliyoyasikia kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam). Nilimsikia akisema, ‘Yeyote mwenye kutengeneza picha ataadhibiwa na Allaah mpaka aitie uhai na hataweza kufanya hivyo’”. Aliposikia hayo yule mtu alivuta pumzi na uso wake ukaiva. Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) alimuambia: “Sikitiko lilioje! Ikiwa huna budi mpaka ufanye picha basi nakunasihi uchore picha za miti na kitu chengine chochote ambacho hakina uhai” [Al-Bukhaariy]
Napia Ametueleza Rasuli wa Allaah (Swalla Alaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika hadiyth ifuatayo:
Imepokewa kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kuwa niliupamba mto wa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) na picha (michoro) za wanyama ambacho kilionekana kama Namruqa (mto mdogo). Alikuja akasimama kati ya watu akiwa na taharuki iliyoonekana usoni mwake. Nikasema, “Ee Rasuli wa Allaah! Kuna nini?” Akasema: “Huu mto ni wa nini?” Nilisema: “Nimeutayarisha kwa ajili yako ili upate kuuegemea”. Alisema: “Kwani wewe hujui kuwa Malaika hawaingii katika nyumba ambazo kuna picha ndani yake; na yeyote mwenye kutengeneza picha ataadhibiwa Siku ya Qiyaamah na ataambiwa kukipatia uhai (kwa alichokiumba)” [Al-Bukhaariy]
Na zipo Hadithi nyengine nyingi kuhusu mas-ala haya tafadhali ingia katika viungo vifuatavyo ambavyo vina majibu ya maswali kama lako takriban ili kupata maelezo zaidi:
Hukmu Ya Kuchora Au Kupiga Picha Za Viumbe Vyenye Roho
Michezo Ya Watoto Masanamu Na Vinyago Vinafaa?
Masanamu Ya Michezo Ya Watoto Yanafaa Kuwekwa Nyumbani?
Hukmu Ya Kupiga Picha - Shaykh Ibn 'Uthaymiyn
Nguo Za Kuswalia Zenye Picha Zinfaaa Kuswaliwa?
Na ubaya mwengine mkubwa zaidi ni kuweka picha yako ukutani ambayo bila shaka itakuwa bila ya hijaab na hali ukiwa umejipamba, na katika nyumba huingia watu ambao sio mahram (maana ya mahram ni, wanaume wasioweza kukuoa kama baba, kaka zako n.k). Hivyo utakuwa umeasi kwa kuonyesha mapambo yako ambayo yamekatazwa na (Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa). Jambo hili ndugu zetu wengi hudhani kuwa ni maendeleo au kwenda na wakati, hali ni mambo ya kuiga makafiri bila ya kujua madhara yake.
Hivyo, hairuhusiwi kutundika picha aina yoyote isipokuwa ya mimea, miti, majabali na vitu ambavyo havina uhai. Lakini za binaadamu, wanyama na hayawani wengine hairuhusiwi. Mwenye kufanya hivyo basi inamkosesha wema na mambo mengi mazuri, mojawapo ni Malaika kuingia katika nyumba hiyo na kuadhibiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa)
Na Allaah Anajua zaidi