Jimai: Kuzini Ramadhwaan (Usiku) Na Kutofunga Mchana Wake Nini Hukmu Yake?
SWALI:
Assalam aleykum
ndungu waislam wa nakala hii shukrani za ngu kwa mungu natoa kwa kuwapa nafasi na uzima kutufundisha sisi kwa kutumia teknologia hii ya kisasa mungu awape yanayo wastahali. "Amin"
Swali langu ni kwa muislam aleye zinii katika mwezi mtukufu wa ramadhani na kuamka siku ya pili yake akiwa haja funga naomba uniambie hukumu ya mtu huyu na anatakiwa afanye nini kama anataka apate msaama wa mola wake,
Jazzaka Allahau kheri, Assalam aleykum
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Hakika hayo ni maasi makubwa kufanya zinaa khaswa katika mwezi mtukufu huu wa Ramadhaan. Inapasa kutambua kwamba vitendo vya mja ikiwa ni vyema au viovu katika miezi mitukufu, au siku tukufu, au saa tukufu huzidi thawabu zake au dhambi zake. Hivyo mwenye kufanya maasi ya zinaa dhambi zake zitakuwa ni zaidi ya mwenye kufanya nje ya mwezi mtukufu.
Tunafahamu kwamba maasi ya zinaa hukmu yake katika sheria ya Kiislamu inafikia kupigwa mawe hadi kuuliwa ikiwa ni mwanamume aliyeoa na mwanamke aliyeolewa. Hivyo ni dhahiri kuwa ni maasi makuu ambayo hapasi Muislamu hata kuyakaribia kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
"Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya." Al-Israa: 32.
Hivyo basi Muislam amehadharishwa kwa kushauriwa kuwa asiukaribie uzinzi, kwa kuziingilia sababu zinazopelekea uzinzi. Jambo hilo ni jambo la aibu na uovu usiofichikana, na hapana njia mbovu kama hiyo. Hivyo basi kuikaribia zinaa tu ni jambo lisilotakiwa, sasa kama umeiingia na kuifikia zinaa ni jambo ovu kabisa kwani amehadharishwa kuikaribia kwa kufanya chochote kitachopelekea kufikiria kulikaribia tendo la zinaa; kama kukaa peke yao mwanamume na mwanamke wasio kuwa maharimu, kuangalia magazeti au filamu zenye wanawake waliojiweka uchi, kutazama wanawake, na kadhalika.
Vipi Muislamu ashindwe kujizuia kufanya maasi katika mwezi mtukufu kama huu ambao ni siku chache tu? Vipi Muislamu ashindwe kuuheshimu mwezi mtuku kama huu ambao ni mwezi mmoja tu na ambao tunategemea kughufuriwa madhambi yetu na kuepushwa na moto?
Muislamu asiyezingatia hayo ni dhahiri kuwa ni mtu aliyejiweka mbali na ridha ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) bali ni mtu asiyemkhofu Mola wake.
Na imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa amesema kumwambia Ibn Mas'uud alipomuuliza ni dhambi gani kubwa mbele ya Allaah? Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamjibu kwa kusema:
"Kumuwekea Allaah mshirika hali ya kuwa Yeye ndie Aliyekuumba; Ibn Mas'uud akauliza tena kisha dhambi gani baada ya hilo? Akamjibu kwa kusema: "Kumuua mtoto wako kwa kuchelea kulishwa pamoja nawe" Ibn Mas'uud akauliza tena kasha dhambi gani baada ya hilo? Akamjibu kwa kusema: "Kuzini na mke wa jirani yako" Imepokelewa na Al-Bukhaariy na Muslim.
Ndio Allaah Akashusha:
"Na wale wasiomwomba mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu, wala hawaui nafsi Aliyoiharimisha Mwenyezi Mungu isipokuwa kwa haki, wala hawazini - na atakayefanya hayo atapata madhara," Al-Furqaan: 68.
Pia ni vyema tuelewe kuwa kila Muislamu anapozini wakati wa hili tendo Allaah Humvua iymaan kama mtu anavyovua nguo yake kama ilivyothibiti katika Hadiythi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Mzinifu aliyezini iwe katika Ramadhaan au mwezi mwengine hukumu yake ni kama ilivyothibiti katika Qur-aan kama hakuwahi kuoa au kuolewa; Qur-aan inasema:
"Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mtandikeni kila mmoja katika wao bakora mia. Wala isikushikeni huruma kwa ajili yao katika hukumu ya Allaah, ikiwa nyinyi mnamuamini Allaah na Siku ya Mwisho. Na lishuhudie adhabu yao kundi la Waumini" An-Nuur: 2.
Ama akiwa mmoja wao au wote wawili wamewahi kuwa wanandoa japo mara moja katika umri wao basi hukumu yao ni kupigwa mawe mpaka kufa kama ilivyothibiti katika Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Muislamu amezini katika mwezi wa Ramadhaan
Amezini usiku wakati anapotarajiwa kama ni Muislamu kujishughulisha na Qiyaam kwa kutafuta na kutarajia radhi na rehma za Mola wa Ramadhaan, lakini yeye amefadhilisha kutafuta ghadhabu za Jabbaar kwa kumuasi wakati kila mmoja anatokwa na machozi kwa kuomba atolewe katika Moto; hivyo amejichagulia amali aliyopendekezewa na kumpambia na Shaytwaan ndio katika walionunua upotofu kwa uongofu, Qiyaam cha Ramadhaan hakikuwa muhimu.
Jambo lililo muhimu hapa ni hili mtu ye ote anayezini iwe katika Ramadhaan au mwezi mwengine huwa na hali mbili:
1. Anazini kwa imaan kuwa zinaa sio haramu, kwani hakuna tofauti yoyote katika tendo zaidi ya kuwa moja linaitwa tendo la ndoa na jengine linaitwa zinaa, na yeye anazini kwa kuwa haoni tofauti bali ni katika haki yake ya kuishibisha jinsia yake na hakuna mwenye haki ya kumuingia katika hilo, huyu huwa amehalalisha Alichoharamisha Allaah, na mwenye kuhalalisha Alichokiharamisha Allaah huwa amejiweka nafsi yake kuwa ni mshirika wa Allaah katika yenye kumhusu Allaah pekee, nako ni kuhalalisha na kuharamisha na huyo huwa ametoka nje ya duara la Uislam na huwa mshirikina na kila ataekubaliana nae huwa anamuabudu, tunajilinda kwake al-Waahidul al-Ahad na kumshirikisha na tunamuomba Atufishe hali ya kuwa ni Waislam.
2. Anazini huku akiwa na iymaan kuwa analolifanya ni haramu na yeye ni mkosa na aasi; huyu ndiye katika wenye kuvuliwa iymaan wakati wa tendo la zinaa na adabu yake ndio kama ilivyothibiti na itamlazimu toba kwani imethibiti katika Hadiyth ya 'Ubadah bin Asw-Swaamit (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kuahidiwa na Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) hawatafanya mambo sita likiwemo zinaa; alisema:
"… Basi yeyote miongoni mwenu atakayeshikamana na kutekeleza ahadi hizo basi ujira wake uko kwa Allaah; na atakayefanya lolote katika hayo na akapewa adhabu inayostahiki – kupigwa mawe au mijeledi mia kwa mzinifu - basi hiyo itakuwa ndio kafara yake, na atakayefanya lolote katika hayo na Allaah Akamsitiri basi itakuwa juu ya Allaah Akipenda Atamsamehe au Akipenda Atampa adhabu huko Akhera" Imepokelewa na Al-Bukhaariy.
Kwa vyovyote, Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) ni Mwenye Rahma na Mwenye Kumsamehe mja Wake. Na madamu mja anataka kutubia kikweli basi Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Hupokea tawbah yake. Hivyo linalopasa ni haraka kabisa kurudi kutubu kwa Mola wake na kuazimia kutokurudia tena, kuendelea na Swawm yake, khaswa siku hizi chache zilizobakia na kuomba sana Maghfirah. Pia kutimiza Swalah zake zote na fardhi nyinginezo akiwa ni mwenye uwezo, na kuzidisha vitendo vyema.
Tafadhali ingia katika kiungo kifuatacho upate maelezo zaidi yanayohusu kutubu.
Kuamka siku ya pili yake akiwa hajafunga
Jambo lililo muhimu hapa ni kama lililotangulia kwa mzinifu; hivyo yeyote asiyefunga Ramadhaan na pia asiyeswali huwa na hali mbili:
1. Hakufunga kwa iymaan kuwa funga sio wajibu sio lazima, bali ni kujitesa tu, na yeye hajafunga kwani haamini kuwa Allaah Amefaradhisha Swawm kwa waja Wake, huyu huwa ametoka nje ya duara la Uislam, amekufuru kwa alichoteremshiwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam); hivyo basi atatakiwe atubie; akitubia na kukubali na kukiri kuwa Swawm ni wajibu na ni faradhi Aliyoifaradhisha Allaah kwake vyenginevyo akifariki na hali yake hii hatokoshwa wala hatoswaliwa kama waswaliwavyo Waislamu kwani yeye si Muislam, na kama iymaan yake kuwa kula mchana wa Ramadhaan bila ya udhuru wowote ule ni halali jambo Aliloliharamisha Allaah basi huwa amejiweka nafsi yake kuwa ni mshirika wa Allaah katika yenye kumhusu Allaah pekee nako ni kuhalalisha na kuharamisha na huyo huwa ametoka nje ya duara la Uislam na huwa mshirikina na kila ataekubaliana nae huwa anamuabudu.
2. Hakufunga tu huku akiwa na iymaan kuwa analolifanya ni haramu na yeye ni mkosa na aasi; huyu aelewe kuwa hata akija kutaka kuilipa siku aliyokula bila ya udhuru wenye kukubaliwa kisharia kulipa kwake huwa haikubaliwi – kulingana na kauli iliyo sahihi zaidi katika kauli za Ahlul 'Ilmi - kwani kila ibaadah iliyowekewa wakati wake maalum na mtu akakusudia kuitoa nje ya wakati wake uliopangiwa bila ya udhuru basi haitokubaliwa ibaadah hiyo; hivyo itamlazimu kujuta kuleta istighfaar, kukithirisha amali njema, kukithirisha Sunnah mithilli ya hiyo amali aliyoiacha; kwani ibaadah yoyote iliyopangiwa wakati wake huwa haikubaliwi kama itafanywa kabla ya wakati iliyopangiwa, basi hivyo hivyo huwa haikubaliwi kama itafanywa baada ya wakati wake bila ya kuwepo udhuru wenye kukubalika kisharia.
Ama kuhusu kutokufunga siku ya pili yake ni kwamba ikiwa ni maasi hayo tu bila ya kuzini mchana wa Ramadhaan, basi itabidi alipe siku hiyo. Ama ikiwa amezini mchana wa Ramadhaan basi itabidi afanye kafara yake ambayo ni kuachia huru mtumwa, na kama haiwezekani (jambo ambalo halipo sasa) basi itabidi afunge miezi miwili mululizo (bila ya kukatiza), na ikiwa hawezi kufunga kutokana na sababu za kiafya, basi alishe masikini 60 au watu wanaohitaji.
Na Allaah Anajua zaidi