Nurse Amekataa Kumhudumia Mgonjwa Asiye Muislam Nguruwe, Kashtakiwa, Je, Atii Taratibu Za Kazi Au Afanyeje?

SWALI:

Assalam Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh, Swali langu ni hivi mimi ni mwanafunzi ninaesomea kazi ya uuguzi (nurse) sasa kuna wakati inabidi umpe mgonjwa chakula na umlishe na hapa hospital wanapika nguruwe jee mimi ninaweza kumhudumia mgonjwa kwa kumpa au kumlisha nguruwe kama ndio chakula alichokitaka? Naomba mnijibu kwa haraka maana ndio nipo kwenye kesi kwa kukataa kumpa mgonjwa chakula. Waalaykum ssalam.


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kumpa mgonjwa nguruwe kama chakula chake. Japokuwa hukutuambia uko mji au nchi gani tutajaribu kukusaidia na kukusaidia katika hilo na tunatumai kuwa utapata tawfiki katika hilo.

 

Awali ya yote tunaona ajabu sana kusikia hayo baada ya kuwa ulimwengu umekuwa mdogo (mfano wa kijiji) na kila mwanadamu ana haki za msingi hapa duniani. Kila wakati tunafahamishwa haki za kila mmoja wetu. Miongoni mwazo ni uhuru wa Dini, wa kujieleza na kadhalika. Kwa hivyo, kila mmoja ana haki ya kufuata Dini yake bila kushurutishwa kufuata mambo ambayo yanakwenda kinyume na maagizo ya Dini yake.

 

Kwa Muislamu haifai kabisa kumsaidia mtu mwengine yeyote yule katika dhambi. Msingi mkubwa kwetu ni Aayah ifuatayo:

"Na saidianeni katika wema na uchamngu, wala msisaidiane katika dhambi na uadui" (5: 2).

 

Hivyo, kinachohitajika ni kwenda kuwaeleza wasimamizi wa hospitali unayojifunza kuhusu jinsi Dini yako inavyosema na kukutaka wewe uwe. Na itakuwa ni vyema upate taasisi au chama cha Kiislamu au Imaam ili aje awafahamishe hilo. Pia uwaeleze kinaganaga kuwa uko tayari kuwalisha wagonjwa chakula chengine chochote.

 

Inatakiwa utumie njia zote katika uwezo wako kuitetea haki yako hiyo ya msingi.

 

Tunakuombea upate tawfiki katika kupata haki zako za kimsingi.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share