Shari'ah Ya Kiislam Na Hoja Ya Kwenda Na Wakati
Sharia’ah Ya Kiislam Na Hoja Ya Kwenda Na Wakati
Naaswir Haamid
Uislamu Na Wakati Wa Sasa
Neno 'mila' ndani ya karne ya 21 ni neno ambalo linatumika mno, sambamba na maadili au utamaduni wa jamii husika. Imani tofauti zimechunguzwa na wataalamu ndani ya nyanja tofauti na kugundulika kwamba mila inatumika kuathiri sheria za dini husika.
Hata hivyo, hii haina maana kwamba msingi wa dini wenyewe ubadilike. Kwa dini ya uteremsho kama Uislamu, kanuni hizi ni butu. Lakini itambulike kwamba hakuna dini inayoweza kukimbia hamasa za kijamii[i].
Qur-aan imetilia mkazo kwenye kufikiri na kuhoji. Nayo inatumia maneno kama 'aql, tadabbur na tafakkur zenye maana ya hoja, kupima mambo na hisia za chini. Hakuna sehemu yoyote ndani ya Uislamu inayotoa amri au mifano kwa njia ya upofu.
Ifuatayo ni baadhi ya mifano kutoka kwenye Qur-aan inayotaka wanaadamu kutumia akili zao wanapofuata amri za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
'Aql
وَتِلْكَ الْأَمْثَالُ نَضْرِبُهَا لِلنَّاسِ ۖ وَمَا يَعْقِلُهَا إِلَّا الْعَالِمُونَ ﴿٤٣﴾
Na hiyo ni mifano Tunawapigia watu. Lakini hawaifahamu isipokuwa wenye elimu. [Al-Ankabuwt: 43]
وَإِذَا نَادَيْتُمْ إِلَى الصَّلَاةِ اتَّخَذُوهَا هُزُوًا وَلَعِبًا ۚ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَوْمٌ لَّا يَعْقِلُونَ ﴿٥٨﴾
Na mnapoita kuadhini Swalaah; huifanyia mzaha na mchezo. Hivyo ni kwa kuwa wao ni watu
wasiotia akilini. [Al-Maaidah: 58]
وَسَخَّرَ لَكُمُ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ ۖ وَالنُّجُومُ مُسَخَّرَاتٌ بِأَمْرِهِ ۗ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَعْقِلُونَ﴿١٢﴾
Na Amekutiishieni usiku na mchana, na jua na mwezi, na nyota zinazotiishwa kwa amri Yake. Hakika katika hayo, bila shaka ni Aayaat (ishara, dalili) kwa watu wanaotia akilini. [An-Nahl: 12]
ضَرَبَ لَكُم مَّثَلًا مِّنْ أَنفُسِكُمْ ۖ هَل لَّكُم مِّن مَّا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُم مِّن شُرَكَاءَ فِي مَا رَزَقْنَاكُمْ فَأَنتُمْ فِيهِ سَوَاءٌ تَخَافُونَهُمْ كَخِيفَتِكُمْ أَنفُسَكُمْ ۚ كَذَٰلِكَ نُفَصِّلُ الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَعْقِلُونَ ﴿٢٨﴾
(Allaah) Amekupigieni mfano kwa hali ya nafsi zenu. Je, katika hao iliyowamiliki mikono yenu ya kuume mnao washirika wowote katika vile Tulivyokuruzukuni; kisha mkawa nyinyi katika hivyo sawasawa, mnawaogopa kama mnavyoogopeana wenyewe kwa wenyewe. Hivyo ndivyo Tunavyofasili waziwazi Aayaat kwa watu wenye akili. [Ar-Ruwm: 28]
Tadabbur
كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ إِلَيْكَ مُبَارَكٌ لِّيَدَّبَّرُوا آيَاتِهِ وَلِيَتَذَكَّرَ أُولُو الْأَلْبَابِ ﴿٢٩﴾
Kitabu Tumekiteremsha kwako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) chenye Baraka, ili wapate kuzingatia kwa makini Aayaat zake, na ili wapate kukumbuka wenye akili. [Swaad: 29]
قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أَمَّن يَمْلِكُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَمَن يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ۚ فَسَيَقُولُونَ اللَّـهُ ۚ فَقُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ﴿٣١﴾
Sema: Nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini. Au nani anayemiliki kusikia na kuona; na nani anayemtoa aliye hai kutoka mfu, na anayemtoa mfu kutoka aliye uhai; na nani anayeendesha mambo (yote)? Watasema: Ni Allaah; basi sema: Je, basi hamuwi na taqwa? [Yuwnus: 31]
يُدَبِّرُ الْأَمْرَ مِنَ السَّمَاءِ إِلَى الْأَرْضِ ثُمَّ يَعْرُجُ إِلَيْهِ فِي يَوْمٍ كَانَ مِقْدَارُهُ أَلْفَ سَنَةٍ مِّمَّا تَعُدُّونَ ﴿٥﴾
Anadabiri mambo kutoka mbinguni mpaka ardhini, kisha inapanda Kwake katika siku ambayo kipimo chake ni miaka elfu katika yale mnayoihesabu nyinyi. [As-Sajdah: 5]
Tafakkur
وَلَوْ شِئْنَا لَرَفَعْنَاهُ بِهَا وَلَـٰكِنَّهُ أَخْلَدَ إِلَى الْأَرْضِ وَاتَّبَعَ هَوَاهُ ۚ فَمَثَلُهُ كَمَثَلِ الْكَلْبِ إِن تَحْمِلْ عَلَيْهِ يَلْهَثْ أَوْ تَتْرُكْهُ يَلْهَث ۚ ذَّٰلِكَ مَثَلُ الْقَوْمِ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا ۚ فَاقْصُصِ الْقَصَصَ لَعَلَّهُمْ يَتَفَكَّرُونَ ﴿١٧٦﴾
Na lau Tungelitaka Tungelimnyanyua kwazo (hizo Aayaat), lakini aligandamana na dunia na akafuata hawaa zake. Basi mfano wake ni kama mfano wa mbwa, ukimhujumu ananing’iniza ulimi nje na kuhema, na ukimwacha pia ananing’iniza ulimi nje na kuhema. Hivyo ndiyo mfano wa watu waliokadhibisha Aayaat Zetu. Basi simulia visa huenda wakatafakari. [Al-A’raaf: 176]
يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ ۖ قُلْ فِيهِمَا إِثْمٌ كَبِيرٌ وَمَنَافِعُ لِلنَّاسِ وَإِثْمُهُمَا أَكْبَرُ مِن نَّفْعِهِمَا ۗ وَيَسْأَلُونَكَ مَاذَا يُنفِقُونَ قُلِ الْعَفْوَ ۗ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمُ الْآيَاتِ لَعَلَّكُمْ تَتَفَكَّرُونَ ﴿٢١٩﴾
Wanakuuliza kuhusu pombe na kamari. Sema: Katika viwili hivyo mna dhambi kubwa na (baadhi ya) manufaa kwa watu. Na dhambi yake viwili hivyo ni kubwa kuliko manufaa yake. Na wanakuuliza nini watoe. Sema: Yaliyokuzidieni. Hivyo ndivyo Allaah Anavyokubainishieni Aayaat (na shariy’ah) ili mpate kutafakari. [Al-Baqarah: 219]
وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِّتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُم مَّوَدَّةً وَرَحْمَةً ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ ﴿٢١﴾
Na katika Aayaat (ishara, dalili) Zake ni kwamba Amekuumbieni katika jinsi yenu wake ili mpate utulivu kwao; na Amekujaalieni baina yenu mapenzi na rahmah. Hakika pana katika hayo, bila shaka Aayah (ishara, zingatio nk) kwa watu wanaotafakari. [Ar-Ruwm: 21]
Lengo la Shari'ah za Kiislamu sio kuweka vikwazo, lakini kuwa ni fundisho kwa jamii bora. Ndani ya jamii inayobadilika kila mara, Ibn Khalduun aliwahi kusema:
Masharti, manufaa, mila na makundi ya dunia na mataifa hayaendelei kutokana na kitu maalum au utaratibu usiobadilika. Daima kuna mabadiliko, muda hadi muda, na kutokana na sharti moja kwenda jengine. Kwa vile hili linatumika kwa watu, wakati na mipaka, linatumika pia kwenye nchi, umri na mataifa. Ukweli huu wa kijamii bila ya shaka yoyote unapelekea mabadiliko ndani ya mapenzi ya watu. Kwa kuangalia ukweli kwamba, mapenzi ya watu ni msingi wa Shari'ah, ni mahitaji na hoja za msingi kwamba Shari'ah na kanuni ziendane na mabadiliko ili kukidhi masharti na hoja zinazobadilika.
Ibnul Qayyim pia ameeleza
Ufafanuzi wa kisheria ni lazima uendane pamoja na mabadiliko ya wakati, sehemu, masharti, madhumuni na mila. Ujinga wa ukweli huu umepelekea kutotenda haki ambako ni kubaya mno kwa Shari'ah, na umesababisha vikwazo vingi, ugumu wa kupelekwa (sehemu) kusikowezekana. Ingawa inatambulika kwamba Shari'ah tukufu, ambayo inawatumikia wanaadamu kwa mapenzi ya hali ya juu haitoweka vikwazo kwa matokeo kama hayo.
Mila Zinasababisha Kuwepo Urahisi
Kanuni za kukubali mabadiliko na dhana ya kupima (mizani) ndani ya Maarifa ya Shari'ah ya Kiislamu (Fiqhi) ni lazima zipewe kipaumbele pale vinapotafsiriwa na kutolewa fafanuzi vipengele vya Shari'ah.
Hatua hii inayokubalika na wanazuoni wengi wa Fiqhi, imepelekea kufanyiwa kazi kwenye juhudi zetu za kufafanua Shari'ah ndani ya mfumo tulio nao sasa wa sheria za nchi (zisizofuata Shari'ah).
Ingawa fikra za kurudisha utawala wa Shari'ah bado zipo na hamu ya Waislamu walio wengi ni kuona kanuni za Shari'ah zinafanya kazi. Lakini utaratibu wa kutoa fataawa unatumika kutoa fafanuzi kwa kutilia mkazo mila za sasa, ni utaratibu ambao utapelekea mpango mzuri kwa wenye hamasa ya kupanua Shari'ah bila ya njia za kimabavu. Kila mmoja wetu, atapendelea kuona zimepanuka kwa njia nzuri ya uadilifu na ya salama[ii].
Juu ya hivyo, bado ukweli utabaki kupewa kipaumbele na utazungumzwa kwa kutoa fataawa sahihi kabisa ambazo zimepingwa na baadhi ya wanazuoni pamoja na ulimwengu wa Magharibi. Kwa hivyo; masuala nyeti kama vile jihaad, hijaab, miyraath na mengineyo bado yatabaki kufuatwa kwa mujibu wa kanuni kuu za Uislamu.
Tunapozungumzia kuhusu kanuni za kubadilika na dhana ya kupima mizani, hatutoi msamaha kwamba Shari'ah ikubali upanuzi bila ya msingi. Ila tunahisi kwamba sio muafaka kama Shari'ah zitatumika katika hali ya kubaguliwa, kuachwa nyuma kutokana na upanuzi wa nyanja nyenginezo kama za kijamii, kiutamaduni, kiuchumi na kisiasa. Zote hizi ni lazima zihusishwe kwamba Shari'ah inawezekana kufanyiwa kazi kwa uzuri na kwa mafanikio.
Ada Za Watu Ndani Ya Uislamu
'Azm inatumika kwa jambo lililozoeleka na lililo kawaida baina ya watu, na jambo ambalo wamelizoea kulitenda, vyovyote itakavyokuwa, ikiwa ni neno au kitendo ambacho hakiendani kinyume na Qur-aan wala Sunnah.
Kwa mfano, kama ambavyo inajulikana katika utamaduni wa Kiislamu, kwamba neno "nyumba" bayt - بيت linapotamkwa, lina maana ya nyumba ambamo watu wanaishi na sio msikiti, ingawa masjid – مسجد "msikiti" kimaana unaitwa nyumba ndani ya Qur-aan. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:
إِنَّ أَوَّلَ بَيْتٍ وُضِعَ لِلنَّاسِ لَلَّذِي بِبَكَّةَ مُبَارَكًا وَهُدًى لِّلْعَالَمِينَ ﴿٩٦﴾
Hakika nyumba ya awali iliyowekwa kwa ajili ya watu (kufanya ‘ibaadah) ni ile ambayo iko Bakkah (Makkah), yenye barakah na mwongozo kwa walimwengu. [Aal-Imraan: 96]
Ada za watu chini ya Uislamu ni miongoni mwa mambo yanayofanya kanuni kubadilika kwa mujibu wa wakati na sehemu. Ni lazima itambulike kwamba ni vyanzo vidogo vidogo tu vya Shari'ah vinakubali kubadilika na pia kuwe na haja ya kufanya hivyo; kwamba mahitaji yatapelekea kubadilika kwa kanuni; kwamba mabadiliko hayo yawe yanafanywa kwa lengo la kukutana na mahitaji ya watu na kuondosha ugumu kwa watu.
Kwa maneno mengine; chini ya Uislamu, mila inaweza kusemwa kuwa ni msuluhishi kwa nukuu ya 'Abdullaah bin Mas'uud (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) inayosema:
"Mila za watu ni msingi wa maamuzi"
Ambayo pia ameeleza kwamba kile ambacho Waislamu wataona kuwa ni kizuri basi ni kizuri mbele ya macho ya Allaah.
Hivyo, tunaweza kusema kwamba; Mahkama za Kiislamu bila ya kikwazo, zinaruhusiwa kuegemeza hukumu zake kwenye ada za watu ndani ya masuala ambayo hayajaelezwa katika maandiko. Ikiangaliwa kwamba, mila zinatofautiana kwa sehemu na wakati. Hivyo, ni lazima maamuzi yatolewe kama ni ya wakati wa sasa, na ambayo imezoeleka baina ya watu na kubwa zaidi ni kwamba isipingane na kanuni za Qur-aan na Sunnah.
Mila ni ada za jamii ambazo zinatekelezwa na mtu mwenye akili timamu zilizowekwa ndani ya jamii. Kwa mfano, malipo ya mahari hapo enzi za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yalikuwa na kawaida ya kulipwa kwa wakati mmoja. Lakini kwa wakati tulio nao sasa, yaruhusika kulipa kwa awamu au hata kama ilivyo enzi za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa mkumbo mmoja.
Hivyo, mila za watu zinabadilika muda baada ya muda au kizazi baada ya kizazi. Inafanya kuwa ni sehemu ya amri za Shari'ah, inapewa nafasi ya kutolea maamuzi.
Kuna simulizi nyengine ya lalamiko lililopelekwa kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka kwa mke wa Abuu Sufyaan, akilalamika kwamba mumewe hamtumikii yeye wala watoto. Alipoulizwa, Abuu Sufyaan alijibu kwamba hakuwa na uwezo. Ndipo tunaposoma ndani ya Qur-aan:
لِيُنفِقْ ذُو سَعَةٍ مِّن سَعَتِهِ ۖ وَمَن قُدِرَ عَلَيْهِ رِزْقُهُ فَلْيُنفِقْ مِمَّا آتَاهُ اللَّـهُ ۚ لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا مَا آتَاهَا ۚ سَيَجْعَلُ اللَّـهُ بَعْدَ عُسْرٍ يُسْرًا﴿٧﴾
Ili mwenye wasaa agharimu kwa wasaa wake, na aliyebaniwa riziki yake, basi agharimie katika kile Alichompa Allaah. Allaah Haikalifishi nafsi yeyote ile isipokuwa kwa kile Alichoipa. Allaah Atajaalia baada ya ugumu kuwa wepesi. [Atw-Twalaaq: 7]
Mabadiliko Ya Wakati Ndani Ya Shari'ah Ya Kiislamu
Ili mila zikubaliwe kwa kwenda pamoja na wakati ndani ya Shari'ah, ni lazima zikutane na masharti yafuatayo kabla ya kukubaliwa:
a. Iwe ni ada ya watu (kawaida yao).
b. Ada hiyo iwepo wakati inapofanyiwa kuwa ni sheria.
c. Isiendane kinyume na makubaliano ya awali.
d. Isikiuke vyanzo vya Shari'ah, yaani Qur-aan na Sunnah.
Wakati na pahala zinasababisha sheria kubadilika ikiegemezwa na ada za watu. Hivyo, zinatumika kwa mujibu wa mila hizo alimuradi ada za watu zimebadilika kwa mujibu wa wakati na pahala. Kwa mfano, kafiri aliyesilimu hawezi kukalifishwa kufunga kuanzia alfajiri hadi magharibi kwa kipindi chote cha Ramadhwaan nzima. Kwa kusherehesha hapa, mfano X amesilimu mwezi wa Sha’abaan, anaambiwa kuwa ni lazima atimize kanuni zifuatazo:
i) Atahiriwe
ii) Afunge mwezi mzima wa Ramadhwaan na
iii) Akirudi kwenye ukafiri atauawa.
Hayo mambo juu ni sahihi kabisa, lakini kuambiwa maelezo kama hayo kwa Muislamu mpya kutamrudisha nyuma imani yake. Ni lazima afunzwe kidogo kidogo bila ya kumkalifisha.
Halikadhalika, wakati wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakukuwa na mambo kama fatwa na fiqhi. Ila yamezuka leo kwa lengo la kuondoa ugumu wa mashaka ya kisasa ambayo yanahitaji kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
Mazingira Ambayo Yatasababisha Kubadilisha Kanuni
Mazingira ya mila ndani ya Uislamu yanaweza kufanya mabadiliko ya kanuni katika njia tatu kuu:
1-Kubadilika Tabia Za Waislamu:
Kubadilika kwa tabia za Waislamu kutasababisha baadhi ya kanuni kubadilika na kuzipa nguvu. Lakini jambo hili, ni lazima litofautishwe na ulimwengu wa Magharibi, ambapo watu wanaweza kubadilisha aina yoyote ya kanuni hata ziwe zimeganda ndani ya maandiko ya dini zao. Hii inaonekana wazi kwa kuruhusu biashara ya ukahaba baina ya jinsia tofauti au jinsia moja. Pia kuhalalisha kwa kinachoitwa 'ndoa' au ni vyema tuseme mahusiano ya watu wa jinsia moja.
Chini ya Uislamu, hili halipo na wala halitatokea; kwani ni kanuni ndogo ndogo tu ndizo zitakazobadilika. Kwa mfano, kutokana na kuondoka imani na uadilifu kwenye biashara, wanazuoni wameruhusu malipo ya kodi ya nyumba kufanywa mwanzo.
Pia wakati wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliruhusu wanawake kuswali jamaa msikitini. Nabiy pia aliwaomba Waislamu wanaume kutowazuia wanawake kuswali msikitini. Lakini hili lilikuja kuzuiliwa na baadhi kutokana na kukosekana uaminifu na usalama.
Hilo pia linaweza kuonekana wakati wa sasa, ambapo mabanati wanapewa ruhusa ya kwenda kuswali taaraawiyh au witri nyakati za usiku. Lakini ukweli ni kwamba tunawashuhudia binti hawa wakiwa na vijana wa kiume tena ajnabiyy (ambao si maharimu zao). Ni swalah gani inayoswaliwa hapo?
Utoaji wa talaka tatu kwa mkumbo haukuonekana wakati wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hii ni kutokana na kuwepo na masikilizano mazuri baina ya wana ndoa kwa wakati huo. Pia Waislamu walikuwa wakichunga mno mipaka ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwani halali inayochukiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ni talaka. Lakini kutokana na kubadilika tabia za wanawake na wanaume kufanya mzaha, Sayyidna 'Umar (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) alitoa amri kwamba talaka tatu zitasimama na kutambuliwa kuwa ni talaka tatu na sio talaka moja kama hapo ilivyokuwa mwanzo[iii].
Kukithiri kwa vitendo vya wizi hata ndani ya misikiti kumefanya misikiti kufungwa nje ya nyakati za Swalaah.
Ada za Waislamu katika kuwatumikia walimu wa Madrasah, maimamu, waadhini na wengineo zimeondoka. Hapo kale, walikuwa wakifuliwa nguo, wakipelekewa chakula na kadhalika. Hali hii imesababisha kuwepo mishahara maalum ya Waislam kama hawa ili kuwahamasisha na kuwawezesha kutekeleza harakati za dini hii tukufu ya Kiislamu.
2- Kubadilika Kwa Wakati:
Mila inakwenda sambamba na wakati kwani muda unayoyoma na mila zinapotea. Kwa mfano, kutokana na karne ya sayansi na teknolojia, mikataba kadhaa inafungwa ndani ya mitandao tofauti.
Mfano tu wa mila zilizofanya kubadilisha kanuni kutokana na wakati ni utoaji wa tarjisi za ndoa, kizazi, talaka na kifo. Hili halikuwepo wakati wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), lakini hili linatendeka kwa sababu ya kuweka vizuri kumbukumbu kwa mahitaji ya sasa na baadaye. Hivi sasa, hati hizi zinatolewa ndani ya Uislamu.
Pia kuna simulizi ya Abu-Bishr Qabisa bin al-Makhaariq aliyesema kwamba: kuomba kunaweza kuruhusiwa ikitegemea na wakati, ingawa kiuhalisia kuomba fedha (bila ya sababu ya msingi) ndani ya Uislamu hakujaruhusiwa.
Wakati pia umesababisha kuwepo mfungo mmoja wa Swawm ya Ramadhwaan. Pamoja na sababu nyengine, hili limesababishwa na kuwepo njia bora za mawasiliano. Kanuni hii inakubaliwa kwani hakuna nchi yenye kupishana na nyengine kwa masaa 24[iv]
Mfano mwengine ni kwenye utoaji wa bima kwa vyombo vya usafiri, makaazi na biashara. Jambo ambalo hapo awali halikuwa likiruhusiwa na wanazuoni wetu. Lakini kutokana na kubadilika wakati, Waislamu wamefanyiwa wepesi na wameruhusiwa kuingia ndani ya mikataba ya bima yenye kufuata misingi ya haki na uadilifu.
Wakati pia umeruhusu ufunguzi wa benki ambazo hazina riba na zenye kufuata mifumo ya kanuni sahihi za Uislamu. Hili linatofautishwa na njia ya kale ya kumpatia amana mtu kuhifadhi fedha.
3- Kubadilika Kwa Mazingira:
Haya ni mabadiliko ya kitu kisawasawa bila ya utata au kutetereka. Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inatueleza kwamba maswahaba (Radhwiya Allaahu ‘Anhum) walikuwa hawali nyama ya Budn iliyohifadhiwa zaidi ya siku tatu. Lakini, kutokana na ugumu pamoja na mazingira, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliruhusu kuhifadhiwa na kuliwa nyama zaidi ya siku tatu[v].
Hadiyth nyengine zinatuambia ya kuwa, Swahaba mmoja alimuuliza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni matendo gani bora; Nabiy alimjibu kumuamini Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na Nabiy na kwenda jihaad. Mwengine alimuuliza suala hilo hilo akamjibu kuwatendea wema wazee na jirani yake na kutosema uongo. Mwanamke alipouliza suala hilo hilo, alijibiwa na Nabiy; kumuamini Allaah na Nabiy, kwenda Hijjah na kumtii mumewe.
Hivyo, kutokana na mila za Uislamu, mwanamke hashajihishwi kwenda vitani isipokuwa ni bora kuhitimisha Hijjah yake kabla ya kipande chake cha muda hakijavunjika.
Hitimisho
Ukweli ni kwamba, sasa ni tofauti mno miaka alfu iliyopita. Halikadhalika, amri ni lazima zitofautiane. Hivi sasa Waislamu hawaangalii jua tu kuelewa wakati wa Swalaah. Lakini wanatumia saa, kalenda, simu, mtandao na kadhalika. Kama hatutafungua akili zetu kuruhusu fafanuzi mpya, Shari'ah itatambulika kuwa jiwe, dhaifu na isiyofaa.
Hivi leo, viongozi wa Kiislamu sio tu maimamu au walimu wa Madrasah, lakini ni wahandisi, matabibu, majaji, wahadhiri na kadhalika; ambao wanafanya kazi ndani ya mifumo isiyokuwa ya Kiislamu na wana hamu kubwa ya kusimamisha Uislamu ndani ya sehemu zao za kazi. Hawa ni wataalamu ambao muono wao wa Uislamu hivi sasa na baadaye ni kuona Uislamu unakwenda pamoja na wakati kwa vigezo vya dini yao tukufu ya Kiislamu.
Kinachoweza kufanyiwa marekebisho, kifanyiwe sasa, fatwa zinaendelea kutolewa kutoka kwa wanazuoni tofauti, vivyo hivyo kwenye uandishi wa vitabu, ambavyo ni vyanzo vizuri vya marejeo kwa Waislam wa sasa na baadaye.
Marejeo:
- Muhammad Hashim Kamal, Istihsan And Its Application To Contemporary Issues – Istihsaan Na Matumizi Yake Kwa Masuala Ya Kisasa.
- Imran Ahsan Khan Nyazee, Islamic Jurisprudence – Maarifa Ya Sheria Ya Kiislam.
- Dr. Liquadati Ali Khan Niazi, Islamic Law Of Contract – Sheria Ya Kiislam Ya Mikataba.
[i] Mahathir bin Muhammad, Waziri Mkuu mstaafu wa Malaysia (1981-2003), Risala yake kabla ya kustaafu mbele ya OIC, 16/10/2003.
[ii] Mafundisho ya Uislamu, Sura ya XIII, uk. 150
[iii] Fiqhus Sunnah, uk. 406-411.
[iv] Ibnu Taymiyyah, amezaliwa mwaka 661 na kufariki mwaka 728 H.
[v] Swahiyh al-Bukhaariy, Kitabu namba 26, Hadiyth ya 777.