Zingatio: Mie Simo
Zingatio: Matamasha Ya Ibilisi
Naaswir Haamid
Shukurani zote ni za kwake Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Aliyetujaalia kuwa miongoni mwa wanaoitamka kalimah. Hatuna budi kuelekeza nia, kauli na vitendo vyetu vyote kwa ajili Yake Muumba Pekee. Yote mazuri tuyatendayo yanatokana na Allaah na mabaya yote yanatokana na kasoro zetu.
Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ndiye Ajuaye yaliyomo ndani ya nafsi zetu na wala sisi hatujui yaliyomo ndani ya nafsi Yake. Tunakuomba Rabb wetu Utujaalie kheri kwa wanayotudhania, usituchukulie makosa kwa yanayosemwa juu yetu na utusamehe kwa madhambi ambayo hawayafahamu.
Amma ba'ad:
Kuna mchezo maarufu miongoni mwa watoto ambao huchezwa sana sehemu za mwambao wa Afrika Mashariki. Ni ule mchezo wa kuonesha vidole vitano vya mkono. Kidole cha mwanzo kikatoa rai ya kusema 'twende', cha pili kikauliza 'wapi?', cha tatu kikasema 'tukaibe', cha nne kikawa na wasiwasi na kikauliza 'tukija kukamatwa jee?', kidole cha tano kikakubaliana kubeba mawazo ya wote lakini kikamalizia 'mie simo!'. Huyu wa tano ndiye Ibilisi ambaye atakuwa nasi ndani ya maisha yetu yote ya kumuasi Rabb lakini ataruka kwa hatua zote Siku ya Hesabu:
وَقَالَ الشَّيْطَانُ لَمَّا قُضِيَ الْأَمْرُ إِنَّ اللَّـهَ وَعَدَكُمْ وَعْدَ الْحَقِّ وَوَعَدتُّكُمْ فَأَخْلَفْتُكُمْ ۖ وَمَا كَانَ لِيَ عَلَيْكُم مِّن سُلْطَانٍ إِلَّا أَن دَعَوْتُكُمْ فَاسْتَجَبْتُمْ لِي ۖ فَلَا تَلُومُونِي وَلُومُوا أَنفُسَكُم ۖ مَّا أَنَا بِمُصْرِخِكُمْ وَمَا أَنتُم بِمُصْرِخِيَّ ۖ إِنِّي كَفَرْتُ بِمَا أَشْرَكْتُمُونِ مِن قَبْلُ ۗ إِنَّ الظَّالِمِينَ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٢٢﴾
Na shaytwaan atasema itakapokidhiwa jambo: Hakika Allaah Alikuahidini ahadi ya haki (na Ameitimiza); nami nilikuahidini kisha nikakukhalifuni. Na sikuwa na mamlaka juu yenu isipokuwa nilikuiteni mkaniitikia. Basi msinilaumu, bali laumuni nafsi zenu. Mimi siwezi kukusaidieni kukuokeeni wala nyinyi hamuwezi kunisaidia kuniokoa. Hakika mimi nilikanusha yale mliyonishirikisha zamani. Hakika madhalimu watapa adhabu iumizayo. [Ibraahiym: 22]
Ibilisi amechukua ahadi mbele ya Muumba kwa kusema kwamba atawapotosha wanaadamu ili wasiione nuru ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), waache kutekeleza maamrisho ya Nabiy Wake pamoja na kutofuata njia sahihi ya diyn ya Kiislamu.
Atawakalia mbele yao waione dunia tamu wasahau mauti, atakuwa nyuma yao kuwapulizia upepo wa kila anasa wasitake kusikia shida za masikini. Bado Ibilisi huyu hatatosheka, bali atawakalia wanaadamu kuliani mwao na kuwafanya vibaraka vya ujinga hadi kufikia kumshirikisha Rabb, atamalizia kwa kuifunga milango ya kushotoni mwao wasiamini ghayb na hivyo kuwakosesha iymaan ya Uislamu.
Rafiki mwema ni yule ambaye atakufaa duniani na akhera. Huyu si mwengine bali ni ndugu yako wa Kiislamu asiyependa ukhasirike:
إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ ﴿٣﴾
Isipokuwa wale walioamini na wakatenda mema na wakausiana haki na wakausiana subira. [Al-'Aswr: 3]
Munakutana kwenye madarasa mukishindana kuisaka elimu ya Kiislamu pamoja na kusaidiana kutekeleza yaliyoamrishwa na Muumba. Tofauti kabisa na Ibilisi pamoja na jeshi lake, ambao wana usuhuba wa kunyunyizia marashi juu ya kichwa tu kama kwenye harusi. Hata ukifika kwako harufu haipo nawe.
Tujitahidi kufuata Qur-aan na Sunnah ya Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwani hizo ndio kinga kuu za kumzuia Ibilisi kutuhadaa.