Mashairi: Kujengea Makaburi

                    

 

                     Abdallah Bin Eifan

                 (Jeddah, Saudi Arabia)

 

 

Salaam zangu natuma, zifike kwa ikhwani,

Mungu Awape uzima, tuwe tunatumaini,

Twaomba Zake rehema, Atubariki Manani,

Kujengea Makaburi, Dini yetu inapinga.

 

Sheria ya yetu dini, inakataza jamani,

Kaburi si bustani, kulipamba kwa majani,

Wala sio maskani, kulijengea kwa fani,

Kujengea Makaburi, Dini yetu inapinga.

 

Na majina kuandika, kuonyesha ni ya nani,

Inakatazwa hakika, ni tabia ya kigeni,

Uhakika ukitaka, nenda Madina mjini,

Kujengea Makaburi, Dini yetu inapinga.

 

Ukishafika Madina, tembea makaburini,

Maswahaba utaona, walivyozikwa zamani,

Huwezi ona majina, wala majengo fulani,

Kujengea Makaburi, Dini yetu inapinga.

 

Pia wake wa Mtume, majina yao huoni,

Na binti yake Mtume, Fatma yumo kundini,

Na Swahibu ya Mtume, Uthman Bin Affani,

Kujengea Makaburi, Dini yetu inapinga.

 

Na pia Abu Hurayra, na wengine Waumini,

Majina hawakuchora, kashuhudie machoni,

Hawakujenga minara, wala maua pembeni,

Kujengea Makaburi, Dini yetu inapinga.

 

Hatukuzwi binadamu, Ukubwa wa Rahmani,

Na Mungu Awarehemu, Awaingize peponi,

Dini yetu ni timamu, ipo kamili yakini,

Kujengea Makaburi, Dini yetu inapinga.

 

Maiti anachotaka, dua zenu kwa makini,

Msisahau sadaka, hata kidogo toeni,

Kaburi ya kusifika, faida yake ni nini ?

Kujengea Makaburi, Dini yetu inapinga.

 

Kaburi weka alama, iwe ndogo wastani,

Watu wapate tazama, wasikanyage miguuni,

Maiti ana heshima, ingawa yupo shimoni,

Kujengea Makaburi, Dini yetu inapinga.

 

Beti kumi zinatosha, kalamu naweka chini,

Tutazidi kukumbusha, na kupeana maoni,

Tupate kurekebisha, mengi yenye walakini,

Kujengea Makaburi, Dini yetu inapinga.

 

 

Share