'Aqiydah Ya Ahlus Sunnah Wal Jama'ah

 

'Aqiydah Ya Ahlus Sunnah Wal Jama'ah

 

Imekusanywa na: Muhammad Faraj Salim As-Sa’y (Rahimahu Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

‘Aqiydah ya Ahlus Sunnah ni sahili na nyepesi, haina tabu kufahamika wala haina mikanganyo. Haina tabu kuisherehesha. Bali inafahamika na mtu wa kawaida kama inavyofahamika na mtaalamu. Mtu yeyote anaweza kuifahamu kwa wepesi kabisa.

 

Vitabu vyao vya Hadiyth kama vile Al-Bukhaariy na Muslim na vingine, pamoja na mafundisho ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) yaliyonukuliwa ndani ya vitabu hivyo na kuenezwa kila mahali ulimwenguni kwa njia ya isnadi yenye kufuata mfumo na elimu ya hali ya juu, vitabu hivyo vinakubaliwa na sehemu kubwa sana ya umma huu na vinatumiwa katika kuitimiza na kuisherehesha sheria ya Allaah.

 

'Ulamaa wake kama vile Imam Abu Haniyfah na Imam Maalik na Imam Shafi na Imam Ahmad bin Hanbal na Ibnul Mubaarak na Ibnu Taymiyah na wenzao wengi wengine wanapendwa na kufuatwa na asilimia zaidi ya 95 ya Waislamu ulimwenguni, kutokana na elimu yao kubwa na masharti yao mepesi. Walikuwa daima wakisema: “Ukikuta katika mafundisho yetu yanayokubaliana na Qur-aan au Sunnah sahihi, basi yafuateni. Na kama hayakubaliani na hayo basi yapigeni na ukuta.”

 

Watu wamedurusu sira zao na mwenendo wao na elimu yao heshima yao, wakawakubali kama ni Maimamu wao walioisherehesha Qur-aan tukufu na mafundisho ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kwa njia ya kitaalamu na kwa uhodari mkubwa.

 

Viongozi wao walipambana na maadui wa Waislamu, wakaweza kuzifungua nchi nyingi sana na nyoyo nyingi. Walitayarisha majeshi na wapiganaji walioweza kuziteka nchi kubwa kubwa kuanzia Uturuki, sehemu kubwa ya Uchina na Urusi. Afghanistan na Afrika na Asia na sehemu kubwa ya Ulaya, na kwa njia hiyo mamilioni kwa mamilioni ya watu waliingia katika dini hii tukufu.

 

Walifanikiwa kote huko kuwatoa watu katika giza la kumkufuru Allaah na kuwaingiza katika nuru ya Uislamu, kuwatoa katika jeuri ya watawala wao, na kuwaingiza katika uadilifu wa Uislamu, kuwatoa katika kuipenda dunia, na kuwaingiza katika kuipenda akhera yao, na juu ya kuwa wao ndio walioziteka nchi hizo, lakini wananchi wake wanandelea mpaka leo kuwapa watoto wao majina ya wafunguzi wale wa Kiislamu.

 

Utamkuta mtoto wa Kirusi au wa Kituruki au wa Ki Africa au Asia au Ulaya au hata Marekani akipewa jina la Abu Bakr au ‘Umar au ‘Aliy au ‘Uthmaan au Mu’aawiyah au Khaalid (Khaalid bin Waliyd) au Haarun au Salaahud-Diyn, n.k.

 

Kutokana na mafundisho ya 'Ulamaa wao yaliyo mepesi yanayokubalika na akili ya mwanadamu yeyote wa kawaida, madhehebu haya yalipendwa na kufuatwa na asilimia kubwa sana ya Waislamu duniani.

 

Kuthibitisha Sifa Za Allaah

 

Kwa mfano katika kuzithibitisha sifa za Allaah, Ahlus Sunnah wanakubali na kukithibitisha kila Alichokubali na Kukithibitisha Allaah bila ya kuchelewesha wala kubadilisha.

 

Allaah Anaposema kuwa Anao Uwezo, na sisi tunaamini kuwa Anao Uwezo.

 

Anaposema kuwa Anaona, na sisi tunaamini kuwa Anaona Subhaanahu wa Ta’ala.

 

Anaposema kuwa Anasikia, na sisi tunaamini kuwa Anasikia.

 

Na anaposema kuwa Anayo macho, na sisi tunaamini kuwa Anayo Macho, Subhanahu wa Taala.

 

Anaposema kuwa Anayo Mikono na sisi tunaamini kuwa Anayo Mikono, na

 

Anaposema kuwa Anao Wajihi, na sisi tunaamini kuwa Anao Wajihi Subhaanahu wa Ta’ala.

Lakini macho Yake na mikono Yake na Wajihi wake na Kuona Kwake na kusikia Kwake hauna mfano wowote na kitu chochote.

 

'Ulamaa wetu wametufundisha kuzikubali sifa zote za Allaah bila ya kukisia kwa akili zetu namna yake au mfano wake. Kwa sababu kuzikataa sifa ambazo Mwenyewe Amejipa Subhaanahu wa Ta’ala, ni makosa, na kuzifananisha sifa hizo pia ni makosa.

 

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ﴿١١﴾

Hakuna chochote kinachofanana Naye, Naye Ndiye Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote. [Ash-Shuwraa: 11]

 

 

 

Allaah Anaposema:

 

  يَدُ اللَّـهِ فَوْقَ أَيْدِيهِمْ ۚ

Mkono wa Allaah Uko juu ya mikono yao [Al-Fat-h: 10]

 

Sisi tunaamini kuwa Allaah Anao Mkono. Kwa sababu Yeye Mwenyewe Subhaanahu wa Ta’ala Amesema hivyo. Lakini hatuufananishi Mkono Wake na vijikono vyetu.

 

Tutoe tu ushahidi katika vitabu wa wapinzani, anasema mwanachuoni wa Kishia As-Sayed Muhammad Al-Husayniy Ash-Shiraziy katika tafsiri yake inayoitwa; Taqriyb al Qur-aan fiy Adh’haan katika kuifasiri Aayah hii:

 

 يَدُ اللَّـهِ فَوْقَ أَيْدِيهِمْ ۚ

Mkono wa Allaah Uko juu ya mikono yao” 

 

Aayah hii inazungumza juu ya Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) waliofungamana na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) (chini ya mti), na katika kufungamana, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akiutandaza mkono wake huku matumbo ya vidole yakielekea juu, na wanapokuja wenye kufungamana naye walikuwa wakiweka mikono yao juu ya mkono wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).”

 

 

Aayah hii iliteremshwa baada ya Swahaba kufungamana na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) walipokuja chini ya ule mti na kuiweka mikono yao juu ya mkono wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), ndipo Allaah Aliposema:

 

 يَدُ اللَّـهِ فَوْقَ أَيْدِيهِمْ ۚ

 

 “Mkono wa Allaah Uko juu ya mikono yao” [Al-Fat-h: 10]

 

'Ulamaa wanasema: ‘Mguu wa meza hauwezi kufanana na mguu wa Seremala aliyeichonga meza hiyo na kutengeneza miguu yake, kama vile mkono wa fundi aliyetengeneza simu hauwezi kuwa sawa na mkono wa simu. Siku zote sifa za mtengenezaji haziwezi kufanana na sifa za bidhaa yake.

 

Na Allaah Ndiye Mwenye mifano mikubwa.

 

 

Kwa hivyo Anaposema Subhaanahu wa Ta'ala kuwa Anao Mkono, na sisi tunakubali kuwa Anao Mkono lakini hatuufananishi na mikono wetu, kwa sababu sifa za Muumba haziwezi kufanana na sifa za viumbe

 

Na katika Aayah nyingine Allaah Anamuuliza Ibilisi:

 

 

 قَالَ يَا إِبْلِيسُ مَا مَنَعَكَ أَن تَسْجُدَ لِمَا خَلَقْتُ بِيَدَيَّ ۖ أَسْتَكْبَرْتَ أَمْ كُنتَ مِنَ الْعَالِينَ ﴿٧٥﴾

(Allaah) Akasema: “Ee Ibliys! Nini kilichokuzuia usimsujudie Niliyemuumba kwa Mikono Yangu? Je, umetakabari, au umekuwa miongoni mwa waliojitukuza?” [Swaad: 75]

 

Sisi tunaamini kuwa; kwa vile Allaah Amesema kuwa Amemuumba Aadam kwa mikono yake basi haiwezekani kuwa Amekusudia kuwa Amemuumba kwa njia nyingine.

 

Ndani ya Qur-aan tukufu Allaah Anazungumza na watu wa kila aina, wenye elimu na wasiokuwa na elimu. Na kusudi Lake Subhaanahu wa Ta’ala ni kuwafundisha watu hao waijuwe dini yao, juu ya hitilafu ya ufahamu wao. Kwa hivyo haiwezekani Azungumze nao kwa njia ya mafumbo au majazi akawa Anasema neno huku Akikusudia jambo au neno lingiine.

 

Allaah Angelitaka kusema kuwa Amemuumba mwanaadamu kwa Kudra Yake, kwa mfano; basi Angelisema tu, pasingekuwa na haja ya kuutaja mkono.

 

Na katika Aayah nyingine pia Allaah Anasema:

 

أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّا خَلَقْنَا لَهُم مِّمَّا عَمِلَتْ أَيْدِينَا أَنْعَامًا فَهُمْ لَهَا مَالِكُونَ ﴿٧١﴾

 Je, hawaoni kwamba Sisi Tumewaumbia kutokana na yale iliyofanya Mikono Yetu; wanyama wa mifugo basi wao wanawamiliki? [Yaasiyn: 71]

 

 

Na hivi ndivyo ilivyo katika sifa Zake zote Allaah Subhaanahu wa Ta’ala, kila Anapozitaja, ni juu yetu kusema: ‘Sam’an wa twa’an’, tuzikubali bila kubabaisha maana yake wala kubadilisha wala kufananaisha sifa hizo na sifa za viumbe.

 

Kwa mfano Allaah Anaposema:

 

إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَن يَقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ ﴿٨٢﴾

 Hakika amri Yake Anapotaka chochote hukiambia: “Kun! (Kuwa), nacho huwa.” [Yaasiyn: 82]

 

 

 

Tunapoisikia kauli hiyo ya Allaah Subhaanahu wa Ta’ala, hatuna budi kuikubali na kuiamini. Kwa nini? Kwa sababu Allaah Mwenyewe Amesema hivyo. Ikiwa Allaah Subhaanahu wa Ta’ala Hasemi, kwa nini basi alisema kuwa; hukiambia tu:

 

كُن فَيَكُونُ

Kuwa! Na kikawa?

 

Na katika Aayah nyingine Allaah Anasema:

 

  ۚ وَكَلَّمَ اللَّـهُ مُوسَىٰ تَكْلِيمًا ﴿١٦٤﴾

Na bila shaka Allaah Alimsemesha Muwsaa maneno moja kwa moja. [An-Nisaa 164]

 

 

Bali hata Qur-aan Tukufu ni maneno ya Allaah Subhaanahu wa Ta’ala. Allaah Anasema:

 

وَإِنْ أَحَدٌ مِّنَ الْمُشْرِكِينَ اسْتَجَارَكَ فَأَجِرْهُ حَتَّىٰ يَسْمَعَ كَلَامَ اللَّـهِ ثُمَّ أَبْلِغْهُ مَأْمَنَهُ ۚ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَوْمٌ لَّا يَعْلَمُونَ﴿٦﴾

  Na ikiwa mmoja wa washirikina akikuomba umlinde, basi mlinde mpaka asikie Maneno ya Allaah (Qur-aan), kisha mfikishe mahali pake pa amani. Hivyo kwa kuwa wao ni watu wasiojua.  [At-Tawbah: 6]

 

 

Wengine wanasema kuwa Allaah Hakusudii hivyo, bali hayo ni majazi tu. Na maana yake ni kuwa Anaposema kuwa Anasikia, hakusudii kuwa Anasikia kweli bali hayo ni majazi tu, na Anaposema kuwa Anaona hakusudii kuwa Anaona kweli bali hayo ni majazi tu, na Anaposema kuwa Anayo macho, hakusudii kuwa Anayo macho, bali hayo ni majazi tu, na Anaposema kuwa Anayo mikono hakusudii kuwa Anayo mikono bali hayo ni majazi tu, na anaposema kuwa Anao wajihi hakusudii kuwa Anao wajihi kikweli bali hayo ni majazi tu… Subhaana-Allaah!

 

Sisi tunasema; Majazi yapo, lakini majazi ni kwa mfano mtu shujaa akaitwa simba, au mtu muovu akaitwa nyoka nk. Haya ni majazi. Lakini maneno ya Allaah Aliyotuletea waja wake kwa ajili ya kutufundisha dini yetu na kutujulisha sifa Zake Subhanahu wa Ta'ala, hayawezi kuingia katika mfumo huu. Ni maneno ya Kiarabu yasiyokwenda upande. Lugha ya Kiarabu safi kabisa.

Allaah Anasema:

 

قُرْآنًا عَرَبِيًّا غَيْرَ ذِي عِوَجٍ لَّعَلَّهُمْ يَتَّقُونَ ﴿٢٨﴾

Qur-aan ya Kiarabu isiyokuwa kombo ili wapate kuwa na taqwa. [Az-Zumar: 9]

 

 

 

 

 

 

Share