Qur-aan Ni Maneno Ya Allaah Na Si Kiumbe
Qur-aan Ni Maneno ya Allaah
Na Allaah Ameyateremsha Kwa Rasuli Wake Kama Ni Wahyi
Shaykh Fawzaan (Hafidhwahu Allaah)
Imetarjumiwa na: Naaswir Haamid
Na Kwamba Qur-aan Ni Maneno Ya Allaah
Ufafanuzi Wa Nukta [45]
Baada ya kuwa na iymaan (ya kweli) kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), na ukawa na iymaan (ya kweli) kwa Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), basi utakuwa na iymaan (ya kweli) kwamba Qur-aan ni Maneno ya Allaah; kwa sababu hichi ndicho alichokuja nacho Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na Allaah Ameiteremsha Qur-aan kwake yeye. Na hii Qur-aan haikutokana na maneno ya Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wala si kutoka maneno ya Jibriyl (‘Alayhis-Salaam); isipokuwa ni Maneno ya Allaah tu, (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Allaah Amezungumza nayo, na Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) akaichukua kutoka kwa Allaah, na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaichukua kutoka kwa Jibriyl (Alayhis-Salaam), na Ummah (taifa hili) likaichukua kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Hivyo, haya ni Maneno ya Allaah; asili yake imetoka kutoka Kwake, Yeye ni Mmoja Aliye mbali na kasoro zote. Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) hakuichukua kutoka Al-Lawhul Mahfuudhw (اللوح المحفوظ – Ubao Uliohifadhiwa) kama ambavyo watu wapotofu wanavyosema. Na wala haitokani na maneno ya Jibriyl au Muhammad (‘Alayhimaa Swalaatu was Salaam); isipokuwa inatoka kutoka Maneno ya Rabb wa viumbe vyote. Na kwa Jibriyl na Muhammad (‘Alayhimaa Swalaatu was Salaam) basi hawa wawili ni Wajumbe ambao wameiwasilisha kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Kwa maneno yanayozungumzwa, na kuhusishwa kwake, ni kwa yule aliyeyazungumza; si kwa yule aliyeyatamka tu kama ni anayeyafikisha na anayeyawasilisha.
Hivyo, kwa wale wanaosema kwamba Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) ameyachukua kutoka katika Ubao Uliohifadhiwa au wanaosema kwamba Allaah (‘Azza wa Jalla) Ameiumba ndani yake kwa kitu fulani na kisha Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) akaichukua kutokana na hicho kitu, basi yeyote anayesema hivi ni kaafir (asiyemuamini) Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), ni ambaye amekufuru kwa ukafiri ambao unamtoa nje ya Diyn. Ni mfano wa matamshi ya Jahmiyyah na Mu’tazilah na wale waliofuata njia yao.
Hivyo, hiyo (Qur-aan) ni Maneno ya Allaah – kwa herufi zake na maana zake; Allaah Ameizungumzia kwa namna Aliyoitaka.
Hivyo, tunamueleza Allaah kwa Sifa Yake ya Kuzungumza; na Al-Kalaam (Maneno) ni kutoka kwenye Sifa za Allaah ambazo ni za vitendo (swifaatuhul-fi’liyyah). Na kwa “vipi’ (kayfiyyah) au namna ambayo Alizungumza nayo, basi katika hilo tunasema: “Allaah Anajua zaidi kuhusu hilo.”
Hivyo, hii ni kama ilivyo kwa Sifa Zake nyingine, tunaziamini lakini hatufahamu zipo vipi. Hivyo, kwa maana inafahamika lakini kwa namna “vipi”, basi hilo halifahamiki kwetu sisi.
Mwisho Wa Ufafanuzi Nukta [45]
Imetoka Kutoka Kwake Kama Ni Kitu Kilichozungumzwa Bila Ya Sisi Kufahamu Namna Gani; Na Akaiteremsha Kwa Rasuli Wake Kama Ni Wahyi
Ufafanuzi wa Nukta [46]
Maana: Kwamba Qur-aan imeremshwa kutoka kwa Allaah; Allaah Akaizungumzisha na kuishusha chini. Haikushuka kutoka kwa yeyote mwengine zaidi Yake, na wala haikutoka kutoka kwa yeyote isipokuwa ni Yeye. Sivyo kama wanavyosema, kwamba imetoka kwa Jibriyl c au kutoka kwenye Ubao Uliohifadhiwa au kutoka sehemu iliyo katikati ya hewa. Badala yake, imeanza kutoka kwa Allaah na Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) akaisikia na kuifikisha kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa njia ya wahy (uteremsho) na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akaifikisha kwa watu.
Na iwapo hii Qur-aan ingelikuwa inatokana na maneno ya wana Aadam basi mtu kutoka kwenye kundi la watu angeliweza kutoa suwrah mfano wake. Hivyo, kwa vile hawakuweza kufanya hili, basi inaonesha kwamba hakika haya ni Maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).
Yeye Mtukufu Amesema:
وَإِن كُنتُمْ فِي رَيْبٍ مِّمَّا نَزَّلْنَا عَلَىٰ عَبْدِنَا فَأْتُوا بِسُورَةٍ مِّن مِّثْلِهِ وَادْعُوا شُهَدَاءَكُم مِّن دُونِ اللَّـهِ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٢٣﴾
{Na ikiwa mko katika shaka kutokana na Tuliyoyateremsha juu ya mja Wetu (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), basi leteni Suwrah mfano wake, na waiteni mashahidi wenu pasipo na Allaah mkiwa ni wakweli}. [Al-Baqarah: 23]
Na Yeye Mmoja Aliye mbali na kasoro zote na Mtukufu Zaidi Amesema:
أَمْ يَقُولُونَ افْتَرَاهُ ۖ قُلْ فَأْتُوا بِعَشْرِ سُوَرٍ مِّثْلِهِ مُفْتَرَيَاتٍ وَادْعُوا مَنِ اسْتَطَعْتُم مِّن دُونِ اللَّـهِ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿١٣﴾
{Je, wanasema ameitunga (hii Qur-aan)? Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Leteni Suwrah kumi mfano wake zilizotungwa, na iteni muwawezao (wakusaidieni) pasina Allaah mkiwa ni wakweli}. [Huwd: 13]
Hivyo, Allaah Amewafanya kutokuwa na uwezo wa kufanya hivyo, ingawa walikuwa ni Waarabu na wenye ufasaha wa lugha. Na hii Qur-aan iko kwenye lugha ya Waarabu na ni herufi zake ambazo wanatumia kuzungumzia, na walikuwa na shauku ya kumpinga Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam); na yareti ingelikuwa ndani ya uwezo wao kuipinga na kuifanyia upinzani Qur-aan hii, wasingeliacha kufanya juhudi hata ndogo ya kufanya hivyo. Hivyo pale waliposhindwa kufanya hivyo, basi hili linaonesha kwamba hakika haya ni Maneno ya Allaah, ambayo hayayafikiwi na uongo mbele yake wala nyuma yake.
Mwisho wa Ufafanuzi Nukta [46]
Na Kwa Msingi Huo, Waumini Wanashuhudia Kwayo Kuwa Ni Ukweli Mtupu
Kwa hivyo, kwa wale wenye iymaan (waumini wa kweli) kwa Allaah na Rasuli Wake, wanaamini kwamba Qur-aan ni Maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), na kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa si zaidi ya (Rasuli) anayefikisha (Ujumbe) kutoka kwa Allaah.
Ama kwa maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), Anasema:
إِنَّهُ لَقَوْلُ رَسُولٍ كَرِيمٍ ﴿١٩﴾
{Hakika hii (Qur-aan) bila shaka ni kauli (ameifikisha) Mjumbe mtukufu (Jibriyl)}.
ذِي قُوَّةٍ عِندَ ذِي الْعَرْشِ مَكِينٍ ﴿٢٠﴾
{Mwenye nguvu na cheo kitukufu kwa (Allaah) Anayemiliki ‘Arsh}. [Takwiyr: 19-20]
Hivyo, kile ambacho kinamaanishwa kwa kumuhusisha Jibriyl (‘Alayhis-Salaam), ni kutokana na kipengele cha kuifikisha; kwani haiwezekani kwamba hii Qur-aan iwe inatokana na Maneno ya Allaah na (wakati huo huo) yawe ni maneno ya Jibriyl (‘Alayhis-Salaam). Kawaida ya maneno hayatoki isipokuwa kwa mtu mmoja; hivyo haiwezekani kuielezea kuwa ni Maneno ya zaidi ya mmoja. Na kuihusisha kwa Allaah ni haqiiqiyyah (uhakika na uhalisia) na ama kuihusisha kwa Jibriyl (‘Alayhis-Salaam), basi ni kutokana na kipengele cha kufikisha (kulingania). Na katika aayah nyengine, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:
إِنَّهُ لَقَوْلُ رَسُولٍ كَرِيمٍ ﴿٤٠﴾
{Hakika hii (Qur-aan) bila shaka ni kauli ya Rasuli mtukufu}.
وَمَا هُوَ بِقَوْلِ شَاعِرٍ ۚ قَلِيلًا مَّا تُؤْمِنُونَ ﴿٤١﴾
{Na hiyo si kauli ya mshairi; ni madogo sana yale mnayoamini}. [Al-Haaqah: 40-41]
Maana: Ni kumhusu Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo, kuhusishwa kwake ni kwa mantiki ya kufikisha (kulingania). Hivyo Yeye, Mmoja Pekee Aliye mbali na kasoro zote, baadhi ya wakati huinasibisha Kwake, na baadhi ya wakati kwa Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) na baadhi ya wakati kwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na maneno yaliyo sawasawa kutoka kwa mtu mmoja hayawezi kuwa yamezungumzwa na zaidi ya mtu mmoja. Kwa hivyo, kuhusishwa kwa Allaah ni kwa mnasaba wa asili yake na kwamba hayo ni Maneno Yake, na kuhusishwa kwa Jibriyl na Muhammad (‘Alayhimaa Swalaatu was Salaam) ni kwa mnasaba wa kuifikisha.
Mwisho wa Maelezo ya Nukta [47]
[At-Ta’liyqatul Mukhtaswarah ‘Alaa Matn Al-‘Aqiydah Atw-Twahaawiyyah, uk. 66-68 Nukta 45-47)]
Miongoni mwa nukta zilizojadiliwa katika makala hii ni:
Qur-aan ni Maneno ya Allaah na imetoka kutoka Kwake Yeye; haijaumbwa
Yule anayesema kwamba Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) ameichukua kutoka Ubao Uliohifadhiwa amekufuru kwa kufr ambayo inamtoa nje ya Diyn.
Imetoka kutoka kwa Allaah kama ni kitu kilichozungumzwa bila ya sisi kujua namna gani; na Ameishusha chini kwa Rasuli Wake kama ni wahyi.
Iwapo Qur-aan ingelikuwa inatokana na maneno ya Wana Aadam basi angeliweza mtu japo mmoja kuleta suwrah mfano wake. Lakini hawawezi; hivyo hii inaonesha kwamba hakika haya ni Maneno ya Allaah.
Jibriyl na Muhammad (‘Alayhimaa Swalaatu was Salaam) walikuwa tu ni wafikishaji wa Ujumbe (Qur-aan) kutoka kwa Allaah.
Maneno yaliyo sawa hayawezi kuwa yamezungumzwa na mtu zaidi ya mmoja. Pale Allaah Anapotaja:
إِنَّهُ لَقَوْلُ رَسُولٍ كَرِيمٍ ﴿١٩﴾
{Hakika hii (Qur-aan) bila shaka ni kauli (ameifikisha) Mjumbe mtukufu (Jibriyl)}. [Takwiyr: 19]
Na Anaposema:
إِنَّهُ لَقَوْلُ رَسُولٍ كَرِيمٍ ﴿٤٠﴾
{Hakika hii (Qur-aan) bila shaka ni kauli ya Rasuli mtukufu}. [Al-Haaqah: 40]
Basi, kuhusishwa huku kwa Jibriyl na Muhammad (‘Alayhimaa Swalaatu was Salaam) ni kwa mnasaba wa kuifikisha na sio asili ya kuweza (kwao) kuyazungumzia hayo Maneno (ya Qur-aan).
[At-Ta`liyqaat Al-Mukhtaswarah `Alaa Matn Al-`Aqiydah Atw-Twahaawiyyah, uk. 66-68, nukta 45-47]